Mahakama Yamhukumu Freeman Mbowe

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (53), amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Shilingi milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Nassir Uronu.
Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro jana.
Hata hivyo, Mbowe alifanikiwa kulipa kiasi hicho cha faini na hivyo kuepuka kwenda kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.
Mbowe alikuwa akikabiliwa na kesi namba 73 ya mwaka 2011 iliyofunguliwa na Nassir; aliyedai kushambuliwa kwa kipigo akiwa katika Zahanati ya kijiji cha Nshara kata ya Machame Kaskazini Wilaya ya Hai, mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya za Hai na Siha, Denis Mpelembwa, alisema mahakama hiyo imemtia hatiani Mbowe kwa kosa la kumshambulia Nassir kinyume cha kifungu cha 24 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 cha Sheria iliyofanyiwa Mrekebisho mwaka 2002.
“Mahakama imekuona una hatia katika kosa linalokukabili na inakuhukumu kulipa faini ya Shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela,” alisema Hakimu Mpelembwa.
Awali, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Issa Rajabu, aliyekuwa akisaidiana na Wakili Albert Msando; aliiomba mahakama hiyo kumpunguzia adhabu mteja wake (Mbowe), kwa madai kwamba ni kosa lake la kwanza.
Kesi hiyo ya uchaguzi mkuu uliopita, imekuwa ikivuta hisia za wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga hasa kutokana na nguvu ya kisiasa aliyonayo Mwenyekiti huyo wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Katika uchaguzi huo, Nassir alikuwa Mwangalizi wa Ndani wa Uchaguzi Mkuu akiliwakilisha Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata).
Hata hivyo, Mbowe aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Hai kwa tiketi ya Chadema, aliibuka mshindi kwa kupata kura 28,585, akifuatiwa na Fuya Kimbita (CCM), kura 23,349, Hawa Kihogo (UDP) 258 na Petro Kisimbo (TLP) kura 135.
Wakili wa Jamhuri katika kesi hiyo, Simon Feo, ambaye ni Mwendesha Mashitaka wa Polisi, aliieleza mahakama hiyo kwamba kutokana na ukubwa wa kosa, anaiomba mahakama impatie adhabu stahiki kwa vile makosa kama hayo yanaharibu taswira ya jamii na hasa ikizingatiwa kuwa Mbowe ni kiongozi wa kitaifa.
Baada ya Hakimu Mpelembwa kumaliza kusoma hukumu hiyo, Mbowe alitolewa nje ya mahakama chini ya ulinzi mkali wa Polisi waliokuwa wameimarisha ulinzi katika viunga vya mahakama hiyo na kumshikilia kwa zaidi ya saa mbili; hadi alipofanikiwa kulipa faini ya Shilingi millioni moja na kuachiwa huru.
Akiwa chini ya ulinzi wa Polisi, wanachama na wafuasi wa Chadema waliofurika mahakamani hapo, walilazimika kujichangisha na kisha kulipia faini hiyo kupitia Benki ya NMB na baadaye kuwasilisha mahakamani stakabadhi yenye namba 0317489.
Chanzo: ChademaBlog
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment