ILIPOISHIA Sehemu ya
3…..
Akaniambia
"Chavala! Kazi ni nzuri sana, Hongera! Nakufuatilia sana, ila samahani,
kuna wakati huwa majaribu yanatusonga kwa upesi ila Nakuahidi nitajirekebisha!
Mmh! Jamani mbona sijakuelewa kwani kimetokea nini? Nikamuuliza, Akasema
Chavala watu huwa wanakosea,hata mimi huwa nakosea, nikamtolea macho!
Akawa kama
anashindwa kuongea na kushindwa kujiamini...Lakini kwa kujikaza akasema Chavala
mimi ni.......
ENDELEA...
Sherehe ile iliendelea vizuri, keki ikakatwa na maharusi
wakalishana kwa staili walioichagua wenyewe na watu wakagoganisha maglasi kwa
furaha, wageni waalikwa wakacheza sana pamoja na maharusi na hatimaye ikafika
saa ya kusikia Maneno ya Hekima toka kwa wazazi wa pande zote mbili na hapo
ndio niligundua yalikuwepo mashindano na majivuno kwa hiyo sherehe, alianza
Baba mkubwa wa Bwana harusi na akasema yafuatayo ninayoyakumbuka;
Mwanangu sasa umekua, umecheza sana imetosha, umeruruka
imetosha na nafurahi ukaamua kuanza kusali, Hongera sana na huko Mungu
amekupatia zawadi ya mke, (Vikasikika vigelegele) Najua Mungu hana upendeleo, kama
ni yeye amekupa mke huyo ninaamini utayafurahia maisha yako, Ninaamini
hautamwacha Mungu baada ya kufikia hapo, Sisi kama familia tutakuzawadia gari
ya kutembelea lakini wakati wa sherehe yenu ya kutimiza mwaka mmoja wa ndoa!
(Nilifikiri ni masihara au mbwembwe) basi nikapanga kumuuliza akimaliza, lakini
mara nikamsikia mtu mmoja akisema “Huyu mzee anawapenda sana watoto wake na
nasikia ana hela zake, sema watoto wake wengi wasumbufu, ila huyu ndio
ameonyesha njia kwa kwenda kanisani na kufunga ndoa rasmi, na si umemsikia
ameahidi gari, wala hatanii, amewema atawapa baada ya mwaka mmoja maana
inawezekana haamini kama kwasasa litawafaa” basi hapo nikaelewa, nikaendelea
kulitafakari na kulimezea tu.
Aliendelea….Mchungaji kanisani amewahubiria vizuri usiache
kuyashika hayo, ndoa ni kama mtihani na kufaulu kwake kunategemea na umakini
wako mwenyewe hivyo mkawe makini kwenye ndoa yenu....Nimalizie kwa maneno ya Mc
Chavala aliyosema wakati fulani hapa kuwa....Kuwa alisoma shule msingi akapewa
cheti alipohitimu, akaingia sekondari na pia akapata cheti alipohitimu na hata
chuo kikuu pia alipata cheti chake mwishoni baada ya kuhitimu lakini cheti cha
Ndoa alipewa wakati ndio anaanza maisha ya ndoa,maana yake hata aliyetoa cheti
hawezi kusema wala kutabiri maisha yaliyo mbele...hivyo najua na ninyi ndio
mmpewa cheti cha ndoa leo hivyo kufaulu ama kufeli kwenu kunategemea na ninyi,
Mungu awabariki na tuwatakie maisha mema, Ahsante sana Mc!
(Akanirudishia kisemeo na kurudi kwenye kiti chake)
Yakapigwa makofi hapo na nikawapa wimbo mmoja wa asili yao
na hapo wakacheza kwa raha zao na hapo ikafuata nafasi ya upande wa kike kutoa
maneno ya hekima, ingawa mengi walishayasema wakati wa kumuaga binti yao huko
kwao, basi nilipokaribisha mtu kutoka upande ule wa binti aliinuka Mama yake
mzazi na Bibi harusi, nilimtambua kwasababu niliona alivyotambulishwa hapo
kwanza na hapo nikaona kama watu kadhaa wakiinama chini kwa minong'ono,
sikueelewa haraka, kuwa hakupangwa kuongea yeye ama sio mzuri kwenye kuongea
ama lah! basi nikampatia nafasi ili aseme hekima zake kwa maharusi;
Na hapo mimi nikarudi nyuma, nikajipa nafasi kuanza
kutafakari maneno ya yule mtumishi, yaani yule Mtume aliyeniambia kuwa yeye
ameitwa kwa ajili utumishi mgumu, kwahiyo huwa anakwenda sehemu walizo wanawake
wanaojiuza na hapo akimwona mmoja ambaye amekusudiwa siku hiyo, basi huenda
naye kwenye nyumba za wageni na huko kwasababu ya Utulivu hukubali kumlipa
kahaba huyo na kuanza kumhubiria habari njema za Mungu na kumshawishi aachane
na biashara hiyo, na ndio maana siku ile nilimwona pale akiwa anaondoka! (Hayo
maneno yalikuwa yake kwangu)
Kichwani mwangu maswali yamekuwa mengi kuliko majibu, Najiuliza
hivi ana mke au watoto? Je kanisa lake linaitwaje? Na Je waumini kanisani
wanajua utumishi wa Mtume wao? Je kuna waumini wangapi huko waliopatikana kwa
huduma hiyo? Basi nikiwa nafikiria kuwa itabidi sasa hivi au wakati wa chakula
nikakae nae mezani angalau nijue zaidi mawili matatu, nikajikuta navutwa
usikivu na hekima za mama mzazi wa bibi harusi, Nazo zilikuwa njema ila za
kutisha pia,Mimi nimesherehesha harusi nyingi na nimekumbana na vimbwanga
kadhaa ila wakati huu nilijikuta hata mimi mgeni sana mitaa hii!
Mama alianza kwa maneno ya shangwe utasema yeye ni Mc
pia,lakini wa sherehe za uswahilini labda; Na hapo akamfagilia yule Mtume kuwa
mambo yake safi na hivyo akawataka hawa maharusi wasiache kutaka ushauri na
maombi kwake,na kwa maneno yale na mengineyo nikajua kuwa yule mtumishi alikuwa
mdogo wake kabisa.
Maneno ya mama yule yalikuwa mengi sana ila haya ni machache
tu yaliyobaki vichwani mwa watu wengi, nikiwepo na mimi hata leo;
Mama alisema “Binti yetu tumekulea, tumekutunza na
tumekusomesha ili uwe na maisha mazuri,tena Baba amekusomesha nje ya nchi hivyo
najua huna ulimbukeni wa mambo kama watu wengine, mkwe wetu usichoke wala
usimzuie mkeo anapotaka kusafiri kwenda nje maana unajua amezoea na hata
akitaka kusoma zaidi mruhusu akasome tu maana akisoma ndio mafanikio yenu.
Mwanangu usikubali kabisa kunyanyasika maisha ya manyanyaso yalipitwa na
wakati. Mwanangu nataka ukaishi na mume wako vizuri, mkapendane sana, mkapate
watoto mapacha na mapacha. Hatutaki mtoto wetu azeeke mapema hivyo tumekununulia
mashine kufulia, tumekutafutia mpishi aliyesomea tutamlipa sisi, na
tumewatafutia kitanda, Tv mbili kubwa ya chumbani na sebuleni, sofa ,makabati
ya vyombo na nguo,jokofu Mama samahani sasa hivi ni maneno ya hekima tu zawadi
ni baadae(Nilidakia kama Mc)
Mc wala usijali na mimi wala aikabidhi zawadi sasa hivi ila
nataka tu Bwana harusi ajue binti yetu hana shida kihivyo, tumegharimia harusi
hii ili iwe nzuri sana na pamoja kuwa maisha ya bwana harusi ni ya kawaida
sana, bado tulimruhusu binti yetu aolewe na kijana maana ni chaguo lake! Kuhusu
nyumba mkwe wangu usipate shida ipo, gari binti yangu lipo na tumwekuwekea
kwenye Akaunti yako Milioni 50 kwa ajili ya kuwasaidia kama akiba mnapoanza
maisha na mume wako...ila mkwe usije ukabweteka ukaacha kutafuta hela hata kama
ni hizo hizo za kubangaiza ukifikiri vitu vyote ni kwa ajili yako
hapana...Mwanaume majukumu!
Hapo sikusikia makofi wala vigelegele, ila ndugu wa Bwana
harusi wamekasirika kama mbogo na wale wa bibi harusi wengi wameinamisha vichwa
vyao chini, na yeye mama anaendelea kujimwaga tu....nikiangalia pale mbele
niliona sura ya Bwanaharusi inabadilika taratibu na hapo akili ya haraka
ikanijia nikamfuata Mhazini wa kamati ya maandalizi haraka ili animalizie pesa
yangu ile nusu iliyobaki....Unajua ilipasa anipatie tu mara ile walipofika
ukumbini lakini kwakuwa niliwaamini sikufanya haraka, na nilivyomfuata kwa
bahati mzuri alikuwa nayo mfukoni, hivyo akanipatia bahasha yangu hapo, nikafungua
tu kuchungulia, "Chavala Milioni moja hiyo!" Alisema kwa tabasamu,
nikamwambia ngoja nitahesabu nikitulia na Ole wako ziwe pungufu hata elfu kumi
tu utalipa faini, basi nikawa nakimbia mbele kuchukua kisemeo maana yule mama
asingemaliza maneno yake, kama nisingesogea pale mbele
.....Huo ni ukweli na hayo ndio nilitaka niseme ili kila
mmoja ajue kuwa tumemtunza binti yetu, tumemsomesha, tunampenda na tumefanya
kila tuwezalo kuhakikisha haendi kuteseka, kutaabika, kunyanyasika wala kwenda
kuishi maisha ya tabu huko aendako, tunawatakia maisha mema ua ndoa....Akanipa
kisemeo na wakati anakwenda kukaa hakuna alipiga makofi wala kigelele ila
misunyo na minong'ono na hapo kabla sijakaa vizuri, nilishtuka kuona Bwana
harusi ananyanyuka kwa hasira na kuja kwangu! (Sio jambo la kawaida hilo, hivyo
kila mtu alikuwa amehamaki kuona kinachoenda kutokea, najua hata wageni
waalikwa pia walitibuka na maneno ya majivuno ya mama yule)
Alininyang'anya kisemeo huku machozi yakimtoka na akaanza
akasema hasira na uchungu "Niliamua kumwoa mtoto wenu kwasababu niliamini
anafaa kuwa mke wangu, pamoja na ugumu wa mchakato na manyanyaso wakati naleta
mahari, niliamini ni ugumu ulionipasa kupitia ili kupata mke bora, lakini
maneno haya ya mama yameonyesha majivuno kupita kiasi, majigambo na dharau na
kwakuwa ninyi mnajiona mna kila kitu kwa ajili ya mwanenu basi nafikiri mimi
sio mume wake sahihi, I am sorry baby! (Aliomba msamaha kwa mke wake huku akiwa
na jazba yenye hasira na baada ya hapo akatoka ukumbini)
Ukumbi wote ukatahayaruki, wengine wanalia, wengine
wanasikitika, Bibi harusi akawa anatoka kumkimbilia pamoja na wale wapambe,
Wazazi wa Bwana harusi nao wakawa wanatoka nje na huku upande wa Bibi harusi
nikaona kama mzozo, wengi wakimlalamikia mama mtu kwa maneno yake yale!
Kisemeo ninacho mkononi,sijui niseme nini,Dj wangu
ananishangaa pia,wahudumu nao kila mmoja ana lake, na wageni waalikwa wengine
wakawa wanaendelea kunywa juice zao mezani na pombe walizoingia nazo kimaficho huku
wakijadili kadhia hiyo na ukweli kila mmoja alikereka, maana sio kwamba familia
ya Bwana harusi walikuwa masikini kiasi cha maneno yote yale, ni kweli familia
ya bii harusi ni matajiri sana tu ila ndio wameshaharibu sasa. Watu wengine
wakawa wanaelekea nje ya ukumbi kuangalia hatma zao za kuelekea makwao!
Na ilikuwa ni tu baada ya Maneno hayo ya hekima twende
tukapate Chakula cha siku ile maalum!
Wengine waliwaendea ndugu kufariji, wengine walisema bora
imekuwa hivyo,wengine walisema walijua tu,wengine walibaki walikilia na kuomba
na wengine walikuwa wakiondoka kimyakimya, basi na mimi nikaona ni vema
nimwendee Bwana harusi, yamkini kuna jambo ningeweza kumshauri, Basi nikiwa
naenda nje kwa kasi, nilitoka nje na kuanza kuangalia huku na kule sikuwa na
muona, basi ikanibidi niende kuangalia kwenye eneo la maegesho ya magari kama
gari yao bado ipo yamkini akawa huko, basi kwenye kona hivi niliteleza na kuanguka.
Sikuumia sana maana
nilijidaka kwenye ukuta mpaka kukaa chini, Sasa nilihisi chini kuna kama
majimaji hivi maana niliteleza na mkono mmoja ulilowa maana ulitua chini, Sasa
nikawa ninajiuliza haya maji yametoka wapi na hii ni njia tu, Nilipochukia simu
yangu na kuwasha kurunzi na kumulika, nikagundua yale hayakuwa maji bali ni ilikuwa
ni Damu, nilishtuka sana na kujaribu kumulika pande zote pale nilipokuwa na
hapo nikaona damu imetapakaa mahali pakubwa, pale chini ilijaa na hata mimi
nilikuwa nimekaa juu ya damu.......ITENDELEA!
(c)King
Chavvah, 2015
+255 713 883
797
Instagram:
kingchavvah
Twitter
@kingchavala
E-mail; lacs.project@gmail.com
0 comments:
Post a Comment