Yaani
sikuamini nilichokiona Duh! Nilipoifungua tu nikaka kitandani n ahata kusahau
nilichokuwa ninakifanya kabla ya kuiona pochi ile. Kwa ushahidi wa
vitambulisho, kadi mbili za benki, hela laki moja na ishirini na tatu, pesa
tasilimu, kadi za mawasiliano za watu mashuhuri, yaani kusema ukweli niliishiwa
pozi, Sitaki kuamini kama ile pochi ilikuwa ya........
ENDELEA....
Basi
niliifunga pochi ile na kuiweka mezani, nami nikaendelea na Tafakari ya siku
pamoja na maombi ya asubuhi!
Baadae
niliswaki pamoja na kuoga na nilipokuwa tayari, nilikaa kitandani ili nifikiri
kidogo kama ni sawa kuondoka nihamie pengine kwa siku inayofuata au nibaki hapo
hapo tu!
Baada ya
kutafakari, nilikubali kubaki hapo hapo,nikiamini lipo jambo labda naweza
ng'amua na hivyo nikashuka mapokezi na kutoa taarifa kuwa bado nipo pamoja na
kuacha ufunguo hapo...lakini kabla sijauliza nilijaribu kumuuliza yule kijana
wa mapokezi kuwa Je kuna jina la fulani kwenye daftari lake la wageni kwa
chumba kile,akasita kidogo, ila ninashukuru aliangalia na kuniambia Wengi huwa
hawapendi kuandika na hata wanaoandika majina hapo,wengi huandika majina
wasiyoyatumia!
Mmh kumbe!
Basi nikamwaga na kumwambia nitarejea mchana ama alasiri, nikaacha funguo hapo
na kuelekea zangu mishemishe!
Nilitoka nje
na kujaribu kuzunguka kidogo maeneo yale na kwakweli mchana palionekana ni
mahali tulivu na patakatifu mno, mbele yangu niliona kiduka hivi,nikasogea hapo
jambo ninue juisi na muda wa maongezi...na wakati nakunywa juisi huku
nikisubiri yule muuzaji anikwangulie vocha,nilijaribu tu kumuuliza yule
ndugu.."Inaonekana maeneo haya ni hatari sana,hivi ninyi mnaishije?"
Aliangalia akacheka sana na kujibu, "Najua wewe ni mgeni tu hapa,ila
ukweli ni kuwa, maisha yanaenda tu na kila mmoja anafanya yake tu"
"Jana
nilisikia sauti ya mtu kama akilalamika hivi na sikuona yeyote aliyekuwa hata
na wazo la kutoa msaada...kwanini?" Nilimuuliza!
Basi
akanijibu namna hii "Ukimkuta mtu mahali anajinyonga na watu wanapita
kando huku wakimpiga picha wewe utafanyaje? Mmmh!
Niliduwaa
kidogo, kisha nikalipa hela na kuanza kuondoka maana alikuwa na wateja wengi wa
kuwahudumia. Nilienda nikitafakari, niliangalia huku na kule nikitembea na
kujifunza kila jambo kwa kadri nilivyoweza...hakika Ukizoea kulala
uvunguni,siku ukiiona dabo deka utahesabu makenchi!
Nilifika
kituo cha daladala na ilipofika tu gari ilikuwa inaelekea ninakokwenda
nikapanda, nilikuwa naelekea kunako maduka makubwa ili nijipatie mahitaji
muhimu kunifanya nadhifu kwa yale matukio muhimu yaliokuwa mbele yangu.
Nilipokuwa naingia tu kwa daladala macho yangu yaligongana na kijana mmoja
ambaye alishtuka kiasi, sijui ni kwanini ila wakati ninaingia alikuwa ameweka
mkono wake begani mwa binti mmoja aliyejichubua sana na kuvaa mahereni na
mapambo kibao kama vile yametundikwa! Shikamoo kaka Chavala, Mmh
marahaba,habari yako? Poa tu!
Umekuja mjini kwetu kimyakimya? Nikajikuta
nimemjibu...Ulitaka nipite na kipaza sauti barabarani kuwatangazia kuwa
Nimekuja? Akacheka, tukacheka basi nikakaa kiti cha nyuma yake...baadae kidogo
nilimsikia akimwambia yule dada, Aisee huyu kaka ni mkali Duh! Bonge la Mc na
mwalimu,yaani hapa naona amenistahi maana angeweza kunipa makavu,naomba tushuke
kituo kinachofuata! Nilijifanya kama
sijasikia na kimoyomoyo nikajiambia...Kama ameshatambua anakosea Inatosha!
Nilimwona yule dada akiniangalia kwa woga na mimi nikatazama mbele tu...na
kweli kituo kilichofuata wakashuka haraka haraka!
Basi nilikaa
na kutafakari peke yangu, hivi unawezaje kukaa juu ya tawi bovu na ukawa na
amani? Mawazo yangu yalikatishwa na makelele ya mama mmoja aliyekuwa anaongea
na wenzake watatu waliopanda basi pale wale vijana waliposhuka
Mazungumzo
yalikuwa hivi:
Yaani
wanawake wengine ni wa ajabu sana,sana huwezi kuamini yule mama,mke wa mzee wa
kanisa alikuwa analalamika kuwa mume wake anahisi alihujumu hela kazini kwake
(huyo mama anayeongea sana alikika) Sasa hata kama ni kweli kwanini kumwaibisha
mume wake hivyo? Tena mbele ya wale wamama wa kanisani....Yaani mimi kabisa
siwezi kabisa kumwaibisha au kumsema vibaya mume wangu mbele za watu...Ila
kweli aisee (wale wamama wengine
wakaitikia)...akaendelea...Mimi siwezi kabisa
nawambieni,kwa mfano Mimi mume wangu ni mwongo sana tu,mchafu mpaka
inakera,anaweza akavaa nguo za ndani hata siku nne kama usipogomba na ninahisi
amewahi kutembea na msichana wetu wa kazi...lakini kwasbabu ile ni ndoa,huwezi
kunisikia mimi ninamsema vibaya kwa watu,Jamani tuzitunzeni ndoa zetu,ndio
maana kiapo kilisema...Kwa shida na raha! Nakajisikia tu kucheka lakini
nikajikaza,na hapo ndio hapo nikawa nashuka...Naamini yule mama pamoja na
wenzake waliamini wako sawa,ila ukweli ni kuwa alikuwa anahubiri asichokiishi!
Basi huko
madukani nikafanya yaliyonipeleka na kujifunza mengineyo, mchana nikaona ni
wapi pameandikwa hoteli ama mahali panapouzwa chakula, nikaingia hapo kupata
mlo wa alasiri, maana mchana ulikuwa umekwisha pita. Baada ya kumaliza kula
nilianza safari ya kurudi hotelini, nilipofikia. Nilipofika hoteli, pale
mapokezi nikakuta funguo ya chumba change haipo na nilivyoangaza huku na kule
sikuwaona wahudumu na hivyo nikaamua kapanda mpaka juu na huko nikashangaa
mlango wa chumba changu uko wazi na ndani nina wageni pamoja na mhudumu mmoja
wapo, basi nikamuuliza mhudumu "Hawa ni wageni wangu?" akanitolea
macho kwa woga na hawa wageni wakawa wanainuka kwa aibu...Samahani kaka tulijua
utachelewa na hawa walitaka kupumzika tu mchana huu na kisha tungekufanyia
usafi! Whaat! Nilipatwa na hasira na nikamwambia "Wewe ni mpumbavu na hawa
wageni wako ni pia, mnawezaje kupumzika kwenye chumba cha mtu alichokilipia?
Hamuoni nguo na vitu vingine humu? Nikiwakata kwa vitu vyangu vilivyopotea
mtasemaje? ....na kwanza huu ni ushetani tu, mchana huu wametoka wapi mpaka
wapumzike na tena wapumzike mchana tu? Samahani sana kaka, tusamehe yaishe!
Nikawageukia
wale wapumzikaji wakiwa mlangoni na kuwaambia "Mnapoikaribia dhambi ni
tamu sana lakini saa madhara yake yatakapowatafuna ndio mtakumbuka kuwa chumvi
sio kiungo tu bali ni dawa pia!
Wakatoka na
kuendelea na mizozano yao hapo nje, mimi nikafunga mlango na kuendelea na mambo
yangu. Nikapumzika kidogo mimi kwa niaba yao, maana niko chumbani kwangu, kisha
nikaenda kuoga na kujiandaa kwa ajili ya ile harusi niliyokuwa nasherehesha
Usiku ule!
Nilitoka nimeulamba
kiasi cha kila mmoja kunikata jicho...najua vichwani mwao walikuwa wanafikiri
mimi mwenzao sema tu hawajui mimi nani. Nikatoka mpaka nje kabisa na nikachukua
bajaji na kwenda ukumbini, nilifika kwa wakati na kwenye ladi za mwaliko
walisema tutaanza saa kumi na mbili, basi kwasababu zao wenyewe wakachelewa
kuja na hivyo muda huo nikawa natafakari siku nzima ilivyokwenda tangu
nimeingia mjini hapa.
Majira ya
saa moja na nusu maharusi walifika na ikabidi niende kuwaona na kuongea nao
jinsi inavyopaswa kuwa na kusikia mapendekezo yao kama yapo ili kuifanya siku
yao njema sana. Nilipofika pale nikakuta bibi harusi anatapika,nikashtuka sana
nikidhani anaumwa...lakini yule msimamizi wa kiume akajikuta ameropoka
"Hata mke wangu yule mtoto wetu wa kwanza,miezi ile ya mwanzo mwanzo
alitapikaga sana yaani" Basi hapo nikawa na majibu na nikachefuka sana
maana sipendagi sana kuwa shahidi wa mambo haya, Ndio! Sijakosea, nimesema
sipendelei sana kusherehesha harusi zilitoka fungateni tayari,maana mimi ni
mtumishi na hata Ushereheshaji kwangu ni madhabahu!
Nikawauliza
hivi mmefungia ndoa yenu wapi vile? Akataja jina la kanisa fulani la
pentekosti....Nikawauliza mchungaji anakuja hapa ukumbini? na Je anajua ukweli
huu? Wakajibu kwa pamoja kwa kingereza No! No! No! Mfalme Chavala ni ajali hizi
za ujanani tu, hajui na isingekuwa rahisi hivi kama tungesema, Tunajua
tumekosea na tutatengeneza tu, utusamehe na wewe pia na tunaomba utusitiri!
Nikawaambia
mimi naweza kusema ndio lakini mnajua mmedanganya madhabahuni na mkala kiapo
katika uongo? Nikawambia maandiko katika Mithali 28:13 yanasema "Afichaye
dhambi zake hatafanikiwa, bali aziungamaye atapata rehema" Nikapiga Injili
kidogo hapo na kwakuwa nilikuwa siwahukumu wala kuwachukia, ila nilikuwa nasema
nao kwa faida ya maisha yao huko mbeleni, ninashukuru walinielewa na nikwaacha
watafakari kwa kina na kuona wanaona wafanye nini; Nikawasisitiza...
msipotengeneza hii kitu itawatafuna, ila ni bora dini iwatenge kwa muda kuliko
kwenda mafichoni na baadae mkajifungia mafanikio, wakaniambia poa Chavala,
tutaangalia hilo jambo, haya basi nikawaauliza yale mengine kuhusu sherehe na
tulipomalizana nikawambia wajiandae na mimi nikaanza kazi yangu, tena nikiwa na
amani moyoni kuwa niwaambia ukweli na lipi wanapaswa kulifanya!
Kama kawaida,
nikawakaribisha wazazi wa pande zote mbili,wakafuata wapambe na kisha maharusi
na nikawaacha wakacheza sana nyimbo walizochagua. Baada ya Ukaribisho wa
mwenyekiti wa kamati, nikaambiwa nimwite Mtume fulani aje kufungua sherehe
rasmi kwa maombi!
Basi
nikamwita kwa jina na mara akatokea ndugu mmoja ndani ya suti kali na akiwa
anakuja nikawa namwangalia vizuri...mbona kama mtu huyu ninamjua ila simjui
vizuri,nikampa kisemeo naye akaniangalia sana usoni na kisha akasema neno
kidogo na kuomba!
Aliporudi
kukaa bado nilikuwa napambana kukumbuka nimemwona wapi na nikajikuta kwenye
kisemeo nimesema…..Ahsante sana mtumishi wa Bwana, nafikiri tumeonana mahali
ila nitakuja nikusalimie tu mezani kwako Haleluya!
Basi baada
ya Utambulisho,keki na Shampeni,wageni waalikwa wakiwa wanacheza nikawa
napumzika kidogo,Nikashangaa tu mtu amenigusa begani na kunivuta mpaka nyumba
ya Ukumbi,Kumbe alikuwa ni yule mtumishi na hapo nikawa nahisi kama Je ni yule
niliyemwona pale nilipofikia jana au lah!
Akaniambia
"Chavala! Kazi ni nzuri sana, Hongera! Nakufuatilia sana, ila samahani,
kuna wakati huwa majaribu yanatusonga kwa upesi ila Nakuahidi nitajirekebisha!
Mmh! Jamani mbona sijakuelewa kwani kimetokea nini? Nikamuuliza, Akasema
Chavala watu huwa wanakosea,hata mimi huwa nakosea, nikamtolea macho!
Akawa kama
anashindwa kuongea na kushindwa kujiamini...Lakini kwa kujikaza akasema Chavala
mimi ni.......ITAENDELEA!
(c)King Chavvah, 2015
+255 713 883 797
Instagram: kingchavvah
Twitter @kingchavala
E-mail; lacs.project@gmail.com
0 comments:
Post a Comment