Dk. Abdallah Omar Kigoda - kuwa Waziri Mkuu
Mwigulu Lameck Madelu Nchemba - kuwa Waziri wa Fedha
Celina Ompeshi Kombani - Mazingira
Jenista Joachim Mhagama - Utumishi
WAKATI siku 64 za mtifuano wa kampeni zinatarajiwa kuanza Agosti 22 kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), watakaounda Baraza la Mawaziri la Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 wamekwishaanza kutajwa, imefahamika. Duru za siasa kutoka chama hicho kikongwe kabisa barani Afrika zinasema, licha ya vuguvugu kubwa la mageuzi lililopo nchini, lakini wana uhakika wa kukamata tena dola na sasa wanapanga mikakati madhubuti ya kutetea majimbo yao na kuyarejesha yaliyotwaliwa na upinzani.
Baraza hilo linaelezwa kuwa na uwiano sawa wa jinsia katika harakati za CCM kutimiza malengo ya “nusu-kwa-nusu” katika uongozi, kama alivyofanya mgombea urais Dk. John Magufuli alipomteua Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.
Kwa mujibu wa duru hizo, wakati tayari mgombea urais na mwenza wake wamejulikana, hivi sasa wanaangalia ni nani kati ya makada wake ambaye anaweza kuwa waziri mkuu baada ya chama hicho kurejea madarakani.
“Baada ya Oktoba Rais ni Dk. (John) Magufuli na makamu wake ni Samia (Suluhu Hassan), sasa tunaangazia nani atakayeweza kuwa mtendaji mkuu wa serikali ingawa tayari tumemuona,” kinasema chanzo kimoja ndani ya CCM.
Ingawa chanzo hicho kimegoma kumtaja mtu wanayedhani atakuwa waziri mkuu, lakini taarifa zinasema, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Omar Kigoda, ndiye anayelengwa kushika wadhifa huo.
“Huyu jamaa ndiye waziri mkongwe kuliko wote, ameshika wizara nyingi na anaweza kusimamia vyema utendaji wa serikali,” kilieleza chanzo kingine.
Mbali ya Dk. Kigoda, mwingine anayetajwa kukabidhiwa wizara nyeti ya fedha ni Mwigulu Lameck Madelu Nchemba, ambaye kwa sasa anatetea kiti chake katika Jimbo la Iramba Magharibi.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Nchemba, ambaye ni naibu waziri wa fedha anayeshughulikia uchumi, anafaa kupewa nafasi hiyo kwani katika kipindi cha wiki mbili tu baada ya kuteuliwa aliweza kukusanya kodi zaidi ya Shs. 3 bilioni kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa ambao wanatajwa kwamba wamekuwa wakwepaji sugu wa kodi.
“Huyu jamaa ndiye hasa anayestahili kukaa kwenye ofisi ile, amewahi kufanya kazi Benki Kuu na zaidi ni mtendaji, ukiangalia utendaji wake katika kipindi cha tangu Januari 2014 hadi sasa unaweza kuamini kwamba ndiye hasa anayefaa,” kilisema chanzo kingine.
Hata hivyo, licha ya baraza hilo kuwa na uwiano sawa wa jinsia, lakini taarifa zinasema litakuwa na sura nyingi ngeni na wachache wa zamani.
Ifuatayo ni orodha pendekezwa ya baadhi ya wizara za sasa:
Waziri katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora): George Huruma Mkuchika, Mbunge wa Newala ambaye kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi).
Waziri Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma): Jenista Mhagama.
Waziri katika Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu): Profesa Jumanne Maghembe ambaye kwa sasa ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge): Steven Masatu Wasira ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.
Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi): Aggrey Mwanri, Mbunge wa Siha mkoani Kilimanjaro ambaye kwa sasa ni naibu waziri katika wizara hiyo na utendaji wake umekuwa ukimfunika hata waziri mwenyewe.
Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira): Celina Ompeshi Kombani, ambaye amekuwa kwenye baraza la mawaziri kwamuda mrefu.
Kwa baraza kamili tafuta gazeti lako la wajibika leo hii
0 comments:
Post a Comment