***KIMINI
CHA MTOTO WA ASKOFU***
Sehemu ya 2;
Kwa wasomaji wapya, ‘KIMINI
CHA MTOTO WA ASKOFU’ ni simulizi halisi ya mambo yaliyotokea katika maisha
inayokusanya matukio halisi ama yanayosimamia ama kujengwa katika uhalisia.
Juma lililopita nilielezea jinsi nikitoka uwanja wa ndege gari letu
lilivyogonga gari la binti mmoja
aliyekuwa amevaa kimini. Binti huyo baada ya kuona gari lake limekwanguliwa
alimtukana sana dereva aliyekuwa ananiendesha. Katika purukushani hilo,
akatokea mtumishi wa Mungu kumbe anamfahamu yule binti. Naye binti baada ya
kumwona alibadilika ghafla na kujifanya mwema kisha wakasalimiana na yule
mtumishi ‘Bwana Yesu asifiwe’, wakachangamkiana na maelewano yakatokea kila
mmoja akaenda safari yake. Nami nikapelekwa hotelini. Baada ya kupewa chumba,
nilipokuwa napanda ngazi macho yangu yakagonga na binti ambaye alikuwa si mgeni
kwangu. Nikaweka mizigo yangu chumbani nikaamua kushuka pale mapokezi. Sasa
endelea…,.
Basi
wakati nilivyokuwa nashuka nikamkuta tena yule binti pale mapokezi akidai mzigo
wake, sasa ikanibidi nipitilize kwanza kwenda wanakouza chakula, kisha nimalizie
hapo...basi ninaporudi akawa ameshaondoka. Sasa nikiwa pale mapokezi nikamsikia
yule kijana wa mapokezi akisema "Mabinti wengine jamani! Sijui wanakosa
nini aisee?" basi nikadakia "Kwanini kaka?"
Basi
akashusha pumzi na kusema "Kaka wewe acha tu,mambo mengine ni magumu sana
kuamini ila hapa wanakuja Watumishi mbalimbali, wahubiri na hata waimbaji
kadhaa wa injili na watu wengine maarufu, hapa ndio kijiwe chao....na hata huyu
binti aliyetoka hapa, Nasikia ni Mtoto wa
mheshimiwa mmoja serikalini, tena ni mtu mashuhuri sana na huyu binti huwa
anakuja mara nyingi tu hapa wazee mbalimbali! “Mmh sasa amekosa nini kwao binti
huyu?” Niliuliza! Kwa kweli ni vigumu kujibu hilo lakini unajua kaka, watoto
wengi ambao kwao wana kila kitu wengi hawajatulia.
Nadhani
walikuwa wanafungiwa geti kali sana wakati wanakua hivyo wanataka kuwaonyesha
wazazi wao kuwa wana uhuru na maisha yao au ni kufuata mkumbo au ujinga tu
maana hata mimi sioni sababu! Alijibu yule kaka wa mapokezi kwa urefu.
“Mimi
nafikiri haya ni mapepo tu wala hakuna kingine, amefungwa ufahamu wake,
anaendeshwa moyo wake na mwili wake unatumikishwa,” basi akaniangalia na
kusema, labda kweli, maana kwao nasikia wana kila kitu ambacho mtu angetamani
kuwa nacho!, Lakini hapa duniani kuna mengi huwezi kujua, kama je alipatikana
kwa dawa ama labda utajiri na umaarufu wa baba yake ndio unaugharimu usichana
wake je? Aliuliza yule mhudumu! Oooh kumbe! Nikatamani kuuliza jina la yule
binti ila nikajiambia moyoni, haina haja sana, basi nikapatiwa vile
nilivyoviomba na kisha nikapanda zangu juu chumbani kwangu kwenda kula na
kulala!
Nilipofika
chumbani kwangu baada ya kula niliamua kupumzika kidogo, baadae kidogo niliamua
kwenda bafuni kuondoa uchovu, nikaoga na kukaa ili angalau nijiburudishe,
nikawasha televisheni ili kujaribu kuangalia ulimwenguni kunaendelea nini.
Nilipowasha kwenye umeme, televisheni haikuwaka, nadhani ni kwa sababu ilizimwa
kwa rimoti, hivyo ikanibidi nitafute rimoti, nilitupia macho huku na kule
sikuiona mezani wala kwingine haraka, ikanibidi nianze kutafuta huku na kule,
nilipofungua droo zote za kitanda na makabati sikuipata ila nikakuta lundo la
mipira ya kiume ya kila aina, Kha! Nikashtuka kiasi, lakini nikajiambia moyoni
labda ndio sera za nyumba za wageni za
mjini, kuwalinda wateja wao dhidi ya maambukizi, lakini pia nikahisi kuna mtu
ama watu huwa wanapendelea sana chumba kile na kwa kuwa wanakuja mara nyingi,
basi hujiwekea akiba. Kwenye droo
nyingine nikakuta jarida la picha za wanawake wa kizungu wako uchi kabisa. Bila
shaka jarida lile lilikuwa linahusiana na mitandao ya biashara za ngono za huko
ughaibuni, Tanzania haliwezi kuuzwa kwa sababu ya sheria, hivyo aliyelileta ama
kulisahau, lazima amelitoa mbali huko kwa njia magendo! Mmmh! Nikasikia hasira
ndani yangu! Nikajiuliza maswali mengi bila majibu hivi leo ndio nimeibukia
wapi huku!
Nilichoka
nikaa kitako na kuanza kujikuta nikiomba rehema maana nimeingia mahali ambapo
sikukusudia kabisa, Nilimsihi sana Mungu akili yangu isivurugike na mapepo na
maagano yote katika chumba na nyumba ile yasiambatane nami kamwe. Ni muhimu
kujitenga na madhabahu na maagano ya kishetani mahali popote unapokuwepo, maana
huwezi kujua kabla ya wewe ni nani alikuwepo na alikusudia nini na alifanya
agano maagano gani yanayoweza kukugusa na wewe kama usipokuwa na ulinzi
mwingine….Nikayakumbuka maneno ya mtumishi mmoja niliyewahi kumsikia!
Nilijitahidi
kubaki mstarini bila kupoteza dira na kwa hakika niliweza, ukizingatia kesho
yake nilikuwa nina harusi ya mpendwa mmoja hivi wa kule kanisani, hivyo
niliendelea na maombi na maandalizi ya rohoni kwa habari ya kazi nilizokuwa
nazo mbeleni na kwa upande wangu. U-mc ni Utumishi kabisa, nimekuwa naamini
katika furaha, mafanikio na kibali cha Mungu katika shughuli yeyote
ninayokuwepo. Jumamosi nilikuwa nina harusi na Jumapili nilikuwa ninaongoza
Ibaada ya kuwekwa wakfu kwa mkanda wa video wa mwimbaji fulani maarufu wa
injili katika kanisa fulani la Pentekoste hapa mjini...Sasa nikaona haya
matakataka nionayo yanayotaka kunikumbusha enzi zile za kale, kabla sijamgeukia
Mungu na kuwa mtumishi. Sasa ndio nini? lakini nikajiambia moyoni, neema ya
Mungu inatosha, ngoja niwe mtulivu yamkini kuna jambo la kujifunza hapa maana
kuna jambo la kujifunza kwenye kila litokealo maishani mwetu kama tukiamua
kujifunza!
Nilihisi
mazingira haya sio rafiki sana na hivyo kabla sijavurugikiwa zaidi, ikanibidi
nitoe kompyuta mpakato (Laptop) yangu niweke mezani, angalau humu nitasikiliza
nyimbo za kuabudu na kujenga mazingira ya Ibaada nikiwa humu hotelini. Basi nikaiwasha na kuweka nyimbo hapo, maana
nilikuwa na nyimbo zaidi ya elfu moja. Zikiwa zinaendelea nikajikuta naaanza
kutafakari maneno ya yule mhudumu na yule binti aliyenisalimia kikristo wakati
nafika. Mhudumu alisema hapa wanakuja watumishi wengi tu! Sasa wanakuja kufanya
nini hapa kama ndio kumekaa kidhambidhambi namna hii? Nikawa na maswali mengi
kichwani, inawezekanaje watumishi wapende mahali hapa penye uchafu namna hii?
Basi
nikiwa natafakari bila kupata majibu, na mara usingizi ukanichukua!
Nikiwa
ndani ya lindi la usingizi niliota
ndoto, siikumbuki yote kwa usahihi ila angalau yako mambo ninayakumbuka katika
mojawapo ya ndoto zile hata leo;
Ndoto yenyewe ilikuwa
hivi:
NILIKUWA
NATEMBEA MAHALI FULANI NA NIKAONA JENGO MOJA KAMA UKUMBI ILA WATU WALIO MAENEO
HAYO NI KAMA WATUMISHI HIVI NA KAMA VILE KULIKUWA NA SEMINA, BASI NA MIMI
NIKASEMA NGOJA NIULIZIE HAPA KUNA NINI,YAMKINI NIKAPATA UKUMBI WA KUFANYIA
MATAMASHA YANGU,
NILIPOSEGEA KARIBU NIKAONA KAMA NI NYUMBA YENYE VYUMBA VINGI
SANA NA INA KORIDO MOJA NDEFU YENYE GIZA GIZA....NIKIWA NATEMBEA KUUKARIBIA
MLANGO WA KWANZA NIKIAMINI LABDA NDIO MAPOKEZI, NIKASIKIA KAMA SAUTI YA
MAOMBI,KAMA VILE WATU WANANENA,NILIPOFUNGUA MLANGO NIKAONA
MWANAUME MMOJA YUKO
NA WANAWAKE KAMA SITA HIVI WAKIWA WATUPU NA WANAFANYA MAPENZI NA YULE MWANAUME
NI KAMA NINAMFAHAMU,BASI NIKAFUNGA KWA KUSHTUKA SANA....MMMH! NIKAJIAMBIA
YAMKINI NIMEKOSEA MLANGO,BASI NIKAPIGA HATUA ZAIDI KUUKARIBIA MLANGO WA PILI,
HUMO NIKASIKIA SAUTI YA MAHUBIRI TOKA KWENYE RADIO AU
TELEVISHENI,NILIPOFUNGUA
MLANGO NIKAWAONA WATUMISHI KADHAA WAMEKAA WANAANGALIA NGONO...YAANI SAUTI NI
MAHUBIRI ILA PICHA NI NGONO, BASI NIKAWAULIZA SASA HUO NDIO UPUUZI GANI
MNAOFANYA? MMOJA AKANIJIBU USIJALI MTUMISHI,TUKO HAPA TUNAANGALIA JINSI GANI
SHETANI ANAVYOUHARIBU ULIMWENGU, MMH NIKAUFUNGA ULE MLANGO NIKAKIMBIA
KWENYE
ILE KORIDO ILI NIPATE CHUMBA NIPUMZIKE...NIKAONA MLANGO MBELE YANGU NIKAUFUNGUA
NA NIKASIKIA SHINDWA KWA JINA LA YESU,NIKAUFUNGA, NILIPOCHUNGULIA NI KAMA VILE
WAKRISTO WAMEJITENGA HUMO KWA UOGA NA HAWATAKI KABISA KUSIKIA CHOCHOTE,HIVYO
KILA KINACHOINGIA WAO
WANAKEMEA KABISA...BASI NIKAFUNGUA MLANGO MWINGINE NA
HAPO NIKAONA KAMA MADHABAHU ILA IMEJAA VUMBI MNO,NA NILIPOANGALIA
VIZURI,NIKAONA KAMA KANISA LA MIAKA MINGI SANA AMBALO LIMETELEKEZWA, NIKAONA
KITI,NIKAKIFUTA ILI NIKAE,NACHO KIKAVUNJIKA MAANA KIMEOZA, BASI
AKAINGIA MTU
MMOJA MSAFI SANA ILA NI KAMA HAJAPIGA MSWAKI,NAYE AKANIAMBIA...WENZAKO HUMU
HUWA HAWAKAI,TAFUTA VYUMBA VIZURI HUKO NJE UKAKAE NA WATUMISHI WENZAKO! NDANI
YANGU NIKAJISIKIA HASIRA NA NIKAMWAMBIA..WEWE NI NANI HATA UNIHOFIE MIMI KUKAA
HUMU? AKACHEKA! BASI NAMIMI NIKAMWAMBIA YESU NINI YOTE HAYA NIONAYO?
NIKASHANGAA AMEBADILIKA SURA MTU YULE NA KUTOKA HARAKA, WAKATI ANATOKA
ALIBAMIZA MLANGO KWA NGUVU
na hapo nikashtuka kumbe na Dirisha sikufunga na
lenyewe ndio lilijibamiza kwa nguvu kwa upepo pia!
Basi
niliposhtuka nikaangalia saa, ilikiwa saa tisa na dakika arobaini...nikawaza
hivi hii ndoto maana yake nini? Dirisha likaendelea kujibamiza ndio hapo
nikasogea ili nifunge dirisha na hapo nikaiona rimoti dirishani, kwamba
imefikaje dirishani hata mimi sijui ila nikaichukua na kufunga dirisha...na
kisha nikajaribu kuwasha televisheni, anagalau nijue nini kinaendelea huko.
Chaneli ya
kwanza nikaona Mpira, ya pili nikaona muziki, ya tatu nikaona mieleka, basi
nikaendelea ya nne nikaona kama filamu, ya tano nikaona ngono, ya sita ngono, ya
saba ngono, ya nane muziki, ya tisa wanyama na ya kumi chenga, nikaendelea
mbele nikaona zinajirudia duh! Basi nikazima maana nilitamani nione angalau BBC
au Aljazera au kingine chochote ila sio hayo matakataka!
Jamani! Sasa
hao watumishi, hao waimbaji, na yule niliyepishana naye na yule binti pia humu
ndani wamevutwa na kitu gani hasa?
Nikarudi kwa
kompyuta mpakato yangu tena maana huku tu ndio kumebaki salama, Na kwakuwa
ilikuwa imewashwa muda mrefu, chaji ilikuwa imekwisha kabisa, hivyo nikatoa
chaja kwenye begi na kutafuta mahali pa kuchomeka ili angalau nifanye
maandalizi ya ratiba ya kesho yake.
Soketi ama
Sehemu za kuchomeka zote zilizokuwa zinaonekana, za Umeme zilikuwa zimejaa, hivyo
ikanibidi niangalie kama ipo nyingine upande mwingine na hapo nikaiona kwa
mbali ukutani, mahali ilipokuwepo nisingeweza kuchomeka mapaka kwanza kitanda
kisogee kidogo na hiyo ikanibidi nivute kitanda ili niweze kuchomeka chaja ya
kompyuta ile, Nilipovuta tu Kitanda mara
nikasikia kitu kimeanguka chini, Nikasogea, nikainama na kukiokota kitu hicho!
Khaaa! Kumbe
ni pochi ya kiume, nikaikota na kuifungua ili nijue ni ya nani hasa!
Yaani
sikuamini nilichokiona Duh! Nilipoifungua tu nikaka kitandani n ahata kusahau
nilichokuwa ninakifanya kabla ya kuiona pochi ile.
Kwa ushahidi wa
vitambulisho, kadi mbili za benki, hela laki moja na ishirini na tatu, pesa
tasilimu, kadi za mawasiliano za watu mashuhuri, yaani kusema ukweli niliishiwa
pozi, Sitaki kuamini kama ile pochi ilikuwa ya..........ITAENDELEA
(c)King Chavvah, 2015
+255 713 883797
Instagram; kingchavvah
Twitter @kingchavala
0 comments:
Post a Comment