Prof. Lipumba: Apasua Jipu Jipya Kuhusu Ukawa Kinachoendelea

Profesa Ibrahim Lipumba
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu unawanyima demokrasia wananchi kwa kuwa watakuwa na wagombea urais wawili kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na kituo cha runinga cha Azam juzi baada ya vyombo kadhaa vya habari kuandika uvumi kwamba ametoweka nchini kwa shinikizo huku akiwa amefadhaika, Profesa Lipumba alikanusha taarifa hizo na kuonyesha masikitiko yake jinsi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulivyojichanganya kwenye suala la kupata mgombea urais.
Kuhusu uvumi kwamba CCM wanahusika na kujiuzulu kwake ili kuudhoofisha Ukawa na upinzani kwa ujumla, alisisitiza kwamba umoja huo umejichanganya wenyewe.
“Ukweli wa hili ni kwamba sisi ndiyo tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa na hatimaye sasa Tanzania tumebaki na mgombea urais wa CCM anayegombea CCM, huku Ukawa kukiwa na mgombea urais anayetoka CCM.
“Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais. Wakati sisi tulikuwa na viongozi, mimi mwenyewe nilitaka kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Dk. Slaa (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa) pia alitaka kugombea kupitia Ukawa pamoja na Dk. George Kahangwa (wa NCCR). Sasa sisi tumewekwa kando na badala yake amewekwa mtu wa CCM kugombea kupitia Ukawa,” alisema.
Kuhusu kuondoka kwake Dar es Salaam mara tu baada ya kutangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF, alisema tangu awali alikuwa na safari ya kwenda Rwanda kwa ajili ya utafiti.
“Niko hapa Kigali, lakini wiki ijayo (wiki hii) nitarudi Dar es Salaam. Niliondoka kuja huku kufanya utafiti kuangalia mambo gani nchi kama Tanzania inaweza kujifunza kutokana na maendeleo ya Rwanda; na kwa sababu sina nafasi ya uenyekiti, sikuwa na sababu ya kuueleza umma ninakwenda wapi, niliieleza familia yang utu,” alisema.
Katika mahojiano hayo, Profesa Lipumba aliweka bayana kwamba wagombea urais watatu ndani ya Ukawa walikutana nyumbani kwake, wakakubaliana na kuridhia kumuunga mkono Dk. Slaa katika kinyang’anyiro hicho.
Wiki jana Prof. Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa mambo ndani ya Ukawa, hasa suala la kupokewa kwa Lowassa ndani ya umoja huo.
CREDIT: RAIATANZANIA
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment