UTANGULIZI;
Habari ndugu msomaji,
ninaamini uko sawa na unayo afya ya mwili na akili. Kwa kuishi kwangu, japo kwa
miaka hii michache ya ujana, kwa kuzunguka kwangu huku na kule, ndani na nje ya
nchi na kwa kufanya kazi mbalimbali za ushauri wa biashara, kufundisha vijana,
kufanya ucheshi wa kujitegemea (Stand Up Comedy), Ushereheshaji pamoja na
Utafiti wa uwekezaji, nimekutana na kukumbana na mambo mengi sana ya
kufurahisha na kuogofya, ya faida na ya kuyasikitikia, lakini kwa vyovyote vile
yalivyo, yanafaa kwa fundisho na maonyo kwa jamii ya leo. Ndio maana mimi
ninajiona nina wajibu wa ktumia vipaji vyangu, waledi na kalamu yangu
kukushirikisha wewe yale yafaayo kukushirikisha ili kabla hujapatwa na lolote
uwe umejifunza na kuonywa na wale yaliowakuta.
KIMINI
CHA MTOTO WA ASKOFU ni simulizi halisi, ya mambo yaliyotokea katika maisha na
simulizi inakusanya matukio halisi ama yanayosimamia ama kujengwa katika
uhalisia. Hakuna hata tukio moja linalomlenga mtu moja kwa moja na wala hakuna
Askofu ambaye binti yake ndio anatajwa humu. Ikitokea kuna sehemu ya simulizi
hii inaonyesha kugusa au kuwiana na habari ya kweli ya mtu yeyote, basi
ichukuliwe kama mfanano tu ama mgongano tu wa simulizi hii na matukio halisi!
Mimi
Fredy Erasto Chavala ndio nimezungukwa na kukutana na haya katika simulizi hii,
Nimegharimika, nimeumia na kujikuta katika maswaibu mengi na msingi wa haya
yote ni kimini cha mtoto wa askofu, fuatana name sasa…..
Sehemu ya 1;
Nilitua
uwanja wa ndege saa mbili na nusu ya usiku badala ya saa moja na dakika kumi,
nah ii ilisababishwa na hali ya hewa kuwa mbaya na hivyo kulazimika kwenda
kutua uwanja mwingine wa jirani kabla kurejea tena pale ambapo safari yetu
ilikuwa inakusudiwa.
Kutoka
uwanja wa ndege mpaka mjini pana umbali kiasi, na hivyo ilinibidi aitha
nichukue teksi, bajaji au pikipiki, ama nitembee sana mpaka nje na kusubiri
vibasi vidogo maarufu kama daladala, Lakini kwa bahati nzuri kuna mama mmoja
aliyekuwa na watoto wawili na mizigo ambaye nilimsaidia wakati tunapanda ndege,
na pia nikajikuta ninamsaidia tena wakati wa kushuka. Huyu mama alikuja
kuchukuliwa na mwenyeji wake na hivyo nikajipatia lift ya gari hilo.
Siku
hiyo ilianza kwa maluwe luwe maana dereva aliyekuwa ametumwa na mwenyeji wa
yule mama, nadhani alikuwa amelewa ama alikuwa hajafuzu kukaa kuendesha gari
katika barabara kubwa, maana kilometa tatu kutoka uwanja wa ndege, alikuwa
anataka kumtangulia mtu mbele na kukata kona kulia, kitendo hicho alikifanya
kwa uzembe sana kiasi cha kumkwangua aliyekuwa mbele yake na ile kutaka kukata
kona haraka mbele ya yule aliyemkwangua, tulijukuta tunagongwa ubavuni, mlango
wa nyuma, tena sehemu ya mataa na hivyo kusababisha msongamano mkubwa sana wa
magari. Gari tulilokuwemo lilikuwa ndogo aina ya Verossa na lile lililotugonga lilikuwa Toyota Prado. Ndani ya Prado
alishuka dada mmoja akiwa amevaa viatu virefu na kimini cha bluu pamoja na
blauzi iyoacha maziwa yake nje kidogo na miwani ya jua ikiwa hapo katikati ya
mfereji inabembea. Nwyele nyingi zilimfunika hadi mgongoni na umbile matata
sana. Alishuka kwa jazba na akaanza kutukana hapo kwa mdomo na kuongezea na
yale matusi ya kuonyesha vidole. Dereva wetu alikuwa akitetemeka sana na hivyo
alikuwa hajibu kitu. Mimi sikutoka nje
haraka maana kesi ile ilikuwa hainihusu sana kama mgeni, lakini baada ya muda
niliamua kutoka na kujaribu kuleta mwafaka kwa mabishano yale. Nilipotoka na
kuuliza tatizo ni nini hata jambo hili lisimalizike, ndipo yule dada
alinigeukia kwa hasira sana, ninaamini alitaka kutamka tusi, lakini kwa bahati
tu kugeuka kwake kuligongana na sauti moja nzito iliyotoka kwenye gari nyingine
iliyokuwa inapita ikisema “Hey Rosemary Hujambo?
Umepatwa
na nini?” Basi aligeuka na kuwa mpole ghafla na nikamsikia akisema “Sijambo
Mchungaji, Shikamoo! Bwana asifiwe?” Basi yule baba kama bahati tu tukagongana
macho na japo sikumfahamu kwa haraka ila alinisalimia “King Chavala ni wewe? Au
nimekufananisha?” Ni mimi mkuu! “Oh basi sawa, ninaamini jambo hilo litaisha
vema, ninaamini katika hekima zako, kadi yangu hii hapa, Ninaomba tuwasiliane
tafadhali!” Basi nikapokea ile kadi na kumuuaga na niliporudi kwenye tukio yule
dada aliamua kuchukua namba za simu za yule mama, maana aliomba kulipa gharama
za matengenezo, na basi yule dada akanitazama kama alitamani kunisemesha jambo
ila alijawa na aibu, maana alishajionyesha kama mshari na mkorofi na hapo
ikajulikana kuwa ni binti wa kanisani.
Aliamua
kuondoka akiwa anajiuliza hivi mimi ni nani hasa niliyeshuhudia udhihirisho wa
tabia yake ya kweli. Na mimi pia nikaamua kuwaaga wale ndugu na hivyo
nikatafuta pikipiki hapo ikanipeleka mpaka mitaa ile ambapo nilikuwa na kazi
kesho yake.
Sikutaka
kufikia kwa watu wala mbali sana na eneo nililoelekezwa kuwa ndio yatafanyika
yale yaliyonileta katika mji huu.
Basi
tulienda mpaka maeneo yale, nikafika mpaka ulipo ukumbi na hapo nikaachana na
yule aliyenipeleka, hivyo ikanibidi nianze kuulizia maeneo hayo kama kuna
hoteli ama mahali pa kufikia, hivyo nikaanza kuzunguka hapo mtaani kuona
zilizopo, lakini mara nilijikuta kwenye mtaa fulani ambao nilielekezwa hoteli
moja hivi ambayo ilikuwa ni ghorofa na kwa maeneo hayo hiyo ndio ilikuwa na
hadhi ya kujielewa, basi nikawa natembea kuelekea kwenye hoteli hiyo,
nilipoikaribia hiyo hoteli nilishtuka sana maana yalisikika mayowe makubwa sana
toka chumbani, na hakuna aliyekuwa na hakika hasa kuna nini au kuna nani humo
ndani!
Nilisimama
kwa muda nione kama watu wengine wanaopita wanasikia ninavyosikia ama ni mimi
peke yangu ndio naona maluweluwe!
Ni
ajabu na kweli kuwa kila aliyekatisha maeneo hayo, aligeuka huku na kule na
kuendelea na safari, na wengine walionesha kama kusonya vile ama kupuuzia kana
kwamba wamezoea kusikia!
Nimezoea
kusaidia watu na hivyo hapa ikanipa tabu sana, nawezaje kwenda wakati kuna mtu
anahitaji msaada? Basi nikabaki njia panda kama nisogee vile au nisimame au
niondoke vile!
Kwa
kuwa nilikuwa mgeni maeneo hayo,basi nikaendelea na ile azma ya moyoni mwangu
ya kutafuta mahali pa kulala, na nilipomuuliza mama mmoja aliniambia kuna hoteli maeneo haya, akasema "Ni hiyo hapo, ila
zunguka kule mbele ndio kuna geti" basi nikaanza kujongea mbele na akili
ikawa inanituma kuniambia nikiwa hapo nitajua siri ya makelele hayo!
Nimechoka
sana na safari na natamani kupumzika aisee; Nikaona mlango wa mapokezi,
nikatembea mpaka kwake, Nikamuuliza kaka napata chumba, akadakia haraka
"Poa kaka, karibu, nafasi zipo...Je unataka full au passport?"
Mmh! Ndio nini sasa? "Namaanisha unataka usiku mzima au unaondoka muda sio
mrefu?" Maswali gani hayo kaka ya kishenzi? Unaona nina begi, huwezi
kuhisi mimi ni mgeni? Na unataka niondoke baada ya muda mfupi, unaona nafanana
na majambazi au wanga? "Aah samahani kaka, basi keti hapo subiri wahudumu
wakifanyie usafi fasta, Ni 30,000 tu" Nilikaa pale kando nikiwa nawaza,
haya maeneo ni gani? Kwanza nimesikia mayowe na watu hawaonyeshi kusaidia na
hapa napewa hadithi za kishenzi...ina maana hapa chumba kinaandaliwa mgeni
akifika tu au? Ama chumba kinaandaliwa kutokana na muda unaokaa, basi
nikaendelea kusubiri!
Basi
mara nikiwa kama nasinzia vile, nikashituliwa na yule mhudumu kaka tayari,
naomba mfuate huyo dada akuonyeshe chumba hapo ghorofa ya pili, basi nikaainuka
nakuanza kupanda, nikiwa napanda ngazi, nikapishana na mtu kama namfahamu vile,
sijui ni nani! Ila nahisi ni mtu mmoja maarufu na yamkini nimewahi kumuona
mahali, sema sina hakika sana yamkini nimefananisha maana alikuwa amevaa Kofia,
wakati namwazia huku naendelea kutembea mara juu kabisa kwenye ile korido ya kuelekea chumbani kwangu,
nikagongana uso kwa uso na binti mmoja aliyekuwa anajaribu kujifunika ili
asifahamike akifika chini, na aliponiona akaishiwa pozi, nikasikia tu
"Aaah Uncleee, Shikamooo, mambooo, Bwana asifiwe!" Sasa nikiwa bado
nawaza huyu ni nani vile, basi nikatabasamu tu, na kusema Okeeeey Poa!
"Kaka
chumba chenyewe ndio hiki" Alisema yule mhudumu,basi nikajikuta namwambia
yule binti "Haya naona uko na yako, basi sawa..mimi ndio nimefika,nimeona
nipumzike hapa leo, Wewe uko chumba gani
uncleee?"
Aaah
hapana mimi aaaah bye bwana!
Basi
akashuka haraka akiwa kama amepaniki vile na mimi nikamwangalia akishuka chini
na nikaangia ndani na kuweka mizigo yangu, Lakini mle chumbani nikagundua
hakuna taulo wala sabuni na nilipojaribu kupiga simu nikaona kama ni mbovu basi nikaamua nishuke chini niombe taulo, sabuni kisha nichukue chakula
na kulipa pia kuandika taarifa zangu pale mapokezi!
Basi
wakati nashuka nikamkuta tena yule binti pale mapokezi akidai mzigo wake, sasa
ikanibidi nipitilize kwanza kwenda wanakouza chakula, kisha nimalizie hapo...
ninaporudi akawa ameshaondoka, sasa nikiwa pale mapokezi nikamsikia yule kijana
wa mapokezi akisema "Mabinti wengine jamani! Sijui wanakosa nini
aisee?" basi nikadakia "Kwa nini kaka?"
Basi
akashusha pumzi na kusema "Kaka wewe acha tu, mambo mengine ni magumu sana
kuamini ila hapa wanakuja watumishi mbalimbali, wahubiri na hata waimbaji
kadhaa wa injili na watu wengine maarufu, hapa ndio kijiwe chao....Na hata huyu
binti aliyetoka hapa, nasikia ni Mtoto wa mtumishi wa Mungu..........Itaendelea toleo lijalo!
(c)King
Chavvah,2015
+255
713 883 797
Instagram;
kingchavvah
Twitter
@kingchavala
E-mail:
lacs.project@gmail.com
0 comments:
Post a Comment