Mbowe: Awaomba Radhi Wananchi Kwa Kuchelewa Kutangaza Mgombea Wao

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Magomeni, jijini Mwanza jana
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika Magomeni, jijini Mwanza jana
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama chake kimeshindwa kumtangaza mgombea wake wa urais kama ilivyotarajiwa jana, badala yake kikawaomba Watanzania kutokuwa na haraka, wasiwasi wala mihemko na kuwa muda ukifika kitamtangaza.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Magomeni jijini hapa, Mbowe aliwaomba wananchi kuuvumilia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa sababu viongozi wake wanaendelea na majadiliano na watakapokubaliana watamtangaza mgombea wao.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ilikuwa wamtangaze mgombea urais kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, lakini wenzao wa CUF wamewaomba kuwa wanaendelea na vikao vyao vya chama.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema: “Wengi wana hamu ya kutaka kujua mgombea urais wa Chadema, naomba niseme kwamba tumekuja Mwanza kwa mambo mawili, kuja kuwapokea makamanda hawa wawili na kuitokomeza CCM.
“Ukawa itamsimamisha mgombea urais ambaye Oktoba lazima aiondoe CCM madarakani, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Magdalena Sakaya) ametuomba tena tusubiri hadi tarehe 25 (Jumamosi), kwani watakuwa na kikao cha Baraza Kuu la chama hicho, hivyo tunawasubiri wenzetu.”
Mbowe aliyetumia mkutano huo kuwakabidhi kadi wanachama wapya waliotoka CCM na kujiunga Chadema, Mbunge wa Kahama, James Lembeli na Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, aliweka msisitizo:
“Muungano wetu wa Ukawa ni wa msingi sana, kuna changamoto, tunaomba wananchi muwe wavumilivu, tuache mihemko ili tufikie uamuzi sahihi.
“Tunaomba mtuvumilie, hatuwezi kumtangaza mgombea wetu kwa sababu tu CCM wametangaza wa kwao, hapana! Tutamtangaza mgombea wetu na nyote mtafurahi,” alisema Mbowe huku akishangaliwa na maelfu ya wananchi.
Alisema, Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alikuwa ahudhurie mkutano huo lakini kutokana na foleni za Dar es Salaam alishindwa kuwahi ndege na kwamba, viongozi wengine wa CUF na NCCR Mageuzi walialikwa lakini walikuwa na vikao vya vyama vyao.
Mbowe alisema Ukawa ni mpango wa wananchi, siyo wa viongozi na kwamba ulianzishwa Dodoma na viongozi wote wa upinzani na Kundi la Wabunge 201 wa Bunge Maalumu la Katiba walihudhuria, lakini baadhi yao walipenyezewa ‘kitu kidogo’ wakaondoka hivyo kubaki vyama vinne vya siasa.
Udini, ukabila wamkera
Mbowe alionyesha kusikitishwa na kauli alizodai kutolewa na viongozi wa CCM, kumnadi mgombea wao kwa ukabila na kuwataka wananchi kuwakataa wanaotumia mbinu hizo kwani hali hiyo inaweza kusababisha machafuko.
“Nafurahishwa sana na kauli zinazotolewa na viongozi wa CCM, tunampata kiongozi kwa ukabila! Ukawa hatutamchagua mgombea wetu kwa misingi ya ukabila wala udini, huo ni upumbavu,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Msikubali kurudisha ukabila wala udini, hapa uwanjani tupo makabila mengi, Wasukuma mpo! Wahaya, Wachaga, (Ezekiel) Wenje (Mbunge wa Nyamagana) ni Mjaluo yupo hapa.”
Alisema Watanzania wanataka mabadiliko na kwamba hali hiyo imeshuhudiwa wakati wa uandikishaji wa daftari la wapigakura.
Chanzo: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment