Maswali ‘Yaliyowakimbiza’ Watangaza Nia ya Urais Yatajwa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kuahirishwa kwa mdahalo wa waliotangaza nia katika nafasi ya urais CCM, imebainika kuwa viongozi hao wangepaswa kujibu maswali magumu manane yanayohusu uchumi, utawala bora na utawala wa sheria. Hata hivyo mgombea Balozi Amina Salum Ali pekee ndiye aliyejitokeza.


Baadhi ya wagombea waliokuwa wametajwa kuhudhuria mdahalo huo wa moja kwa moja kupitia televisheni ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu na Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.


Akizungumzia utaratibu wa mdahalo huo ulioandaliwa na Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini ( CEOrt), Mwenyekiti wake Ali Mufuruki alisema, kila mtangaza nia alitakiwa kujibu maswali manne ya uchumi na manne ya utawala bora na utawala wa sheria na ya aina moja.


Maswali ya uchumi waliyotakiwa kujibu ni namna gani mgombea anaweza kupunguza ongezeko la vijana kukosa ajira, umaskini na uvunjifu wa amani.


La pili lilikuwa, ‘Ukitilia maanani kwamba sekta ya kilimo ndiyo tegemeo kuu la maisha kwa asilimia 80 ya Watanzania pia ina uwezo wa kipekee wa kubadilisha uchumi, ni hatua gani utachukua kama utateuliwa kuwa rais?’


La tatu liliuliza, ‘je, kama ukiteuliwa kuwa rais utafanya nini kuhakikisha uchumi wetu unakua na manufaa yake yanakuwa shirikishi na tofauti kati ya maskini na matajiri haiwi kubwa kiasi cha kuhatarisha amani katika nchi yetu?’


Jingine lilipaswa kuulizwa, Ukiwa kiongozi atakayekuwa ofisini wakati huu wa uwekezaji katika sekta ya gesi asilia, utachukua hatua gani kuhakikisha matumaini ya utajiri na maisha bora waliyonayo Watanzania kwa sekta hii yanatimia?’


Watangaza nia hao walitakiwa kueleza pia iwapo wanakubali kwamba Tanzania haiwezi kufikia malengo yake ya maendeleo bila kuwekeza katika miundombinu. ‘Kama unakubali, utatumia mbinu gani kupata fedha hizo nyingi zinazotakiwa katika kuwekezaji kwenye miundombinu?’


Kwa upande wa utawala bora na utawala wa sheria, walitakiwa kueleza ni vipi watachukua hatua kuhakikisha usimamizi mbovu wa masilahi ya nchi, rushwa na upuuzwaji wa sheria unadhibitiwa.


Pia, walitakiwa kueleza watachukua hatua gani kuhakikisha ujangili unatokomezwa nchini, watakomeshaje upotevu mkubwa wa mapato unaotokana na ukwepaji kodi na watatumia njia gani kuhakikisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanakomeshwa.


Hata hivyo, Mufuruki alisema kuwa hadi kufikia juzi mchana watangazania watatu pekee ndiyo walikuwa wamethibitisha ushiriki wao na baadaye Sumaye na Nyalandu wakitoa udhuru.


Watangaza nia wengine, walionekana kuomba radhi kupitia mitandao ya kijamii wakidai kuvurugwa na ratiba ya mdahalo huo ambao awali walielezwa ungefanyika asubuhi kabla ya kuahirishwa.

Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment