Lipumba: Wanaostahili Jela Wanawania Urais CCM

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amechukua fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho na kuahidi kupambana na rushwa huku akishangaa kuwapo watuhumiwa wa ufisadi waliotakiwa kuwa mahabusu lakini wakichukua fomu za kuwania nafasi hiyo kupitia CCM.
Profesa Lipumba alisema iwapo atapatiwa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kupeperusha bendera ya umoja huo atahakikisha anaunda Katiba yenye maoni ya wananchi na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuwaunganisha Watanzania dhidi ya ufisadi.
Mwanasiasa huyo mkongwe katika upinzani aliwaambia wafuasi wa CUF waliomsindikiza kuchukua fomu hiyo jijini hapa jana kuwa ameamua kuwania kiti hicho kwa mara ya tano kwa kuwa kati ya viongozi wa juu wa Ukawa anaamini ana sifa, uwezo, uadilifu, uwazi, uwajibikaji wa kuwaunganisha Watanzania ili waondokane na rushwa na ufisadi uliokithiri nchini.
Profesa Lipumba aliyekabidhiwa fomu hiyo na Katibu wa CUF Wilaya ya Kinondoni, Mohamed Mkandu saa 6.55 mchana, alitaja vipaumbele vyake kuwa ni kujenga misingi ya kuhakikisha watoto wanapata fursa sawa ya maendeleo, ajira, afya, kulinda rasilimali za umma na kupambana na ufisadi.
Profesa Lipumba aliyeanza hotuba yake ya takriban dakika 45 kwa kutoa wasifu wa usomi na kazi mbalimbali za kiuchumi alizozifanya kwa takriban miaka 40, alisema anafahamu bayana matatizo mengi ya Watanzania kwa kuwa amezaliwa na kukulia kijijini.
Alisema matatizo hayo yamesababishwa na “siasa mbovu za chama cha mapinduzi” ukiwamo ufisadi, hivyo iwapo atapatiwa ridhaa ya kuwania kiti hicho cha juu, atakuwa na kazi kubwa ya kuleta uongozi makini utakaohakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa maendeleo ya watu wote.
Alisema iwapo atachaguliwa kuwa rais, hatakuwa na msalie mtume na mafisadi na wote wanaohusika watawajibika kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Inatisha sana kuona mafisadi wakubwa, wala rushwa wakubwa badala ya kuwa ndani ya jela, wanachukua fomu za urais. Tunahitaji kwa kufuata taratibu na haki, mafisadi hao watumikie vifungo na mali zilirudishwe kwa umma walikofisadi,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.
Iwapo atapatiwa nafasi ya urais, alisema katika utawala wake atahakikisha watoto nchini wanapatiwa fursa sawa ya maendeleo kwa kutoa huduma bora afya, lishe na elimu.
Alisema suala la ukuaji imara kwa watoto halijapatiwa kipaumbele na kusababisha udumavu unaowanyima uwezo mkubwa wa kufikiri pindi wanapokuwa wakubwa.
Kufumua Katiba inayopendezwa


Mwanasiasa huyo alisema anachukua fomu nchi ikiwa njia panda baada ya Katiba Inayopendekezwa kuacha masuala ya msingi ya uadilifu na uwajibikaji na kusababisha wachache kujinufaisha kwa rushwa.
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment