Nape: CCM Itashinda tu Hata kwa Goli la Mkono

CCM imesema kuwa itahakikisha inarudi Ikulu hata “kwa bao la mkono” wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye viwanja vya Nyehunge wilayani hapa.
Neno “bao la mkono” hutumiwa kama goli lililofungwa kwa kuupiga mpira kwa mkono kinyume cha taratibu za mpira, lakini hukubaliwa kwa kuwa mwamuzi anakuwa hajaona kitendo hicho.
“Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono… bao ni bao tu ili mradi refa hajaona,” alisema Nape.
Nape, aliye kwenye ziara ya katibu mkuu wa CCM, aliwataka wananchi wa Sengerema kusubiri ushindi wa chama hicho na kuwakumbusha kuwa wanapaswa kuiweka CCM kuanzia udiwani mpaka ubunge kwa nafasi ya urais tayari kuna uhakika.
Katika mkutano huo, Nape alisema ana uhakika CCM itashinda baada ya kushuhudia mwitikio wa Watanzania tangu alipoanza kuongozana na Kinana katika ziara zake za kuizunguka nchi na kuzungumza na wananchi pamoja na kusikiliza kero zao.
Amebainisha kuwa amejifunza na kujiridhisha kuwa chama chake bado kinapendwa miongoni mwa wapigakura waliofikiwa tofauti na vyama vya upinzani.
“Tumefika maeneo mengi ambayo upinzani haujafika. Huko tuna hazina kubwa ya wanachama. Hakuna namna Ukawa wanaweza kuingia Ikulu mwaka huu,” alisisitiza.
Wapinzani waja juu
Kauli hiyo ya Nape ilipingwa na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani waliosema kuwa mtendaji huyo anamaanisha kuwa CCM itaiba kura.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa hakutaka kabisa kuzungumzia kauli ya Nape zaidi ya kusema watakutana Oktoba.
“Kwa bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana, ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba,” alisema Dk Slaa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu suala hilo.
Chanzo: Mwananch
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment