Watu nane wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa vibaya baada ya kupigwa na radi ambayo chanzo chake kimeelezwa kuwa ni kunyesha kwa mvua kubwa iliyodumu kwa takribani saa tatu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Taarifa za awali zimeeleza kuwa miongoni mwa watu waliofariki ni pamoja na wanafunzi sita, mwalimu mmoja na raia mmoja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Bangwe mkoani Kigoma.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Dk Fadhili Kibaya ambaye ni Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Maweni amesema, Tukio hilo limetokea leo majira ya saa saba ambapo alipokea majeruhi 15 na miili 8 ikiwemo 6 ya wanafunzi, mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibilizi na mkazi mmoja wa Bangwe.
Dk. Kibaya amewataja marehemu hao kuwa ni Focus Ntahaba(35), Elieza Mbwambo mwalimu (25) Yusuph Athumani (8), Hassani Ally (9), Fatuma Sley (7), Zamda Sefu (8), Shukrani Yohana (7) na Walupe Kapupa (10) wote wanafunzi wa shule ya Msingi Kibirizi.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni Mwalimu wa darasa la kwanza shuleni hapo, Melina Sililo amesema, wakati alipokuwa akiendelea na kufundisha aliona wingu likitanda na Mvua ikaanza kunyesha jambo lililosadabisha giza.
Amesema hali hiyo ilimfanya ashindwe kufundisha na wakati huohuo radi zilipigwa na moto ukatanda darasa zima ambapo yeye pamoja na watoto zaidi ya kumi walianguka.
“ Nilipata ufahamu na nikajikokota ofisi ya mwalimu mkuu kuomba msaada, tukawabeba wanafunzi na kuwapeleka ofisi ya mwalimu mkuu, tulijaribu kuwapa huduma ya kwanza kwa kuwapaka chumvi bahati mbaya katika hao nane wanafunzi sita wakawa tayari wamefari” Asema Mwalimu Sililo.
Aidha amesema mwalimu Mbwambo alizimia kwa muda kidogo na baada ya kuhangaika kumpatia msaada walimkuta amekwisha fariki hali iliyowalazimu kuomba msaada wa gari la kuwafikisha maiti hao pamoja na majeruhi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo Maweni.
Pamoja na hayo majirani wa shule hiyo ambao ni James Leonard na Rucia Mathiasi wameeleza kusikitisha na tukio hilo ambapo walisema matukio hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara hasa wakati wa Mvua na kwamba mara nyingi yamekuwa yakihusishwa na imani za Kishirikina.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment