Lema: Zitto Hana Ubavu Kwetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimewatoa hofu wanachama wake mkoani Shinyanga kikidai propaganda zinazoenezwa na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, anayedai chama hicho kimepoteza mwelekeo si za kweli bali ni uongo.

Mbunge wa Arusha Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa, Bw. Godbless Lema, aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Shinyanga kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Mahakama ya Mwanzo.

Alisema chama chao bado kipo imara na hakitagawanyika kama inavyodaiwa na Bw. Kabwe ambaye CHADEMA kilimfukuza katika
chama baada ya kukisaliti hivyo kukiuka Katiba ya chama hicho.

"Ndugu zangu wana Shinyanga, CHADEMA tupo imara na tutaendelea kuwa imara hadi tukamate dola na kuwakomboa Watanzania ambao wanateseka tangu tupate uhuru.

"Zitto hana ubavu wa kukigawa chama chetu kama anavyofikiri na kuamini...anahangaika bure, alitaka kukiua tukamshtukia na mimi ndiye mtu wa kwanza kubaini njama zake na wenzake akiwemo Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo; hivyo hawatubabaishi kwa lolote," alisema.

Bw. Lemba aliongeza kuwa, Bw. Kabwe alikuwa chanzo cha kufifisha ushindi wa CHADEMA katika baadhi ya majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 baada ya kutoa taarifa za uongo kwa wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya Katavi, Musoma
Vijijini na Singida Mjini na kusababisha wagombea wa CCM wapite bila kupingwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama hicho Taifa (BAVICHA), Patrobass Katambi, aliwataka wanachama wa CHADEMA kusimama imara ili kukiimarisha chama chao na waachane na Bw. Kabwe aliyeonesha dhahiri usaliti wake baada ya kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo.

"Huyu Bw. Kabwe alikana katakata kujihusisha na Chama cha ACT-Tanzania kama kilivyofahamika awali; lakini siku chache baada ya kutimuliwa CHADEMA akajiunga nacho.

"Anawadanganya Watanzania kuwa yeye ni mjamaa na moja ya sababu iliyomtoa CHADEMA ni kutokuwepo demokrasia ya kweli...kama kweli anathamini demokrasia mbona baada ya kujiunga na ACT ghafla amejitangazia madaraka ya Kiongozi Mkuu wa chama," alihoji Katambi.

Katika hatua nyingine, CHADEMA kimetoa wito kwa wakazi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura waweze kupata haki yao ya kuchagua viongozi waadilifu katika Uchaguzi Mkuu.

Credit:Majira
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment