Chama cha ACT- Tanzania, kimesema hakina muda wa kufanya siasa za chuki na malumbamo dhidi ya vyama vingine vya siasa, badala yake kinajipanga vizuri na kuandaa mazingira ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti wa chama hicho Anna Mghwira, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa, baada ya chama hicho kuzinduliwa rasmi Machi 29 mwaka huu, nguvu yake sasa imeelekezwa katika kujijenga na kujiimarisha.
Alisema katika kujiimarisha, chama hicho kinatafuta wanachama, kwa kuwa kinatambua kuwa ni mtaji wa kujihakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu, pamoja na kuandaa wagombea kwa kuangalia uwezo wao kadri watakavyojitokeza.
“Mimi mwenyewe ni miongoni mwa wagombea ubunge, nitagombea Jimbo la Singida mjini na naamini kwamba nitaweza kupata nafasi hiyo kwa sababu ninafahamika kule ni nyumbani nilikozaliwa . Nimesoma huko, nimekulia huko na najua changamoto zinazotukabili wakazi wa kwetu na jinsi nitakavyoshiriki kukabiliana nazo nikiwa mbunge,”
Mghwira alieleza kuwa chama hicho kinajiimarisha, huku kikitambua kuwa kina wajibu wa kuendeleza ushirikiano na vyama vingine vya siasa, badala ya kujitenga na kuendesha shughuli zake kama kisiwa.
Mwenyekiti huyo, alitolea mfano siku ya uzunduzi wa chama hicho akisema kuwa kulikuwa na watu wengi kutoka vyama mbalimbali ambao walitaka kurudisha kadi za vyama hivyo hadharani na kuchukua kadi za ACT, lakini walisitisha shughuli hiyo kuepuka uhasama.
“Kuwa vyama tofauti haina maana kwamba tuwe maadui, kulikuwa na wanachama wapya siku ya uzinduzi (wa ACT) walitaka kuonyesha hadharani wanavyorudisha kadi za vyama vyao vya awali hatukuwapa nafasi hiyo, kwa sababu hatuoni kuwa hilo ni jambo la kuvutia kwetu,” alisema.
Kwa mujibu wa Mghwira siku hiyo walipokea wanachma wapya 2,000 na bado wanaendelea kupokea wanachama wengine kutoka vyama mbalimbali vya siasa lakini kwa siri.
Ingawa Mghwira hakutaja watu, asilimia kubwa ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, akiwamo Zitto Kabwe ambaye sasa ni Kiongozi Mkuu wa chama hicho na Katibu Mkuu Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo, wamejiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa na vyama vyao.
“Pia katika kuonyesha nia yetu ya kuhitaji ushirikiano mwema wa kisiasa tuliwaalika viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani, ikiwemo Chadema na CUF,” alisema. Alisisitiza kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) ni miongoni mwa wasomi na viongozi wa vyama vingine vya siasa walioalikwa kutoa mada katika uzinduzi wa chama hicho, lakini alipata udhuru hivyo hakufika.
“Hata hivyo tulifarijika kuona shughuli yetu ya uzinduzi wa chama ikifanyika vizuri na kwa amani,” alisema.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment