Breaking News: Mabasi kugoma Tena Aprili 18 Endapo Hawatapewa Mkataba wa Ajira

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Bw. Zitto Kabwe, ameitaka Serikali kuhakikisha madereva wote wa magari ya mizigo na mabasi ya abiria, wanapewa mikataba ya ajira kabla ya Aprili 17, mwaka huu.

Bw. Kabwe aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Uwanja wa Ndege, mkoani Morogoro baada ya kushiriki mazishi ya watu zaidi ya 17 walioteketea kwa moto kwenye ajali ya basi la abiria la Nganga na Mitsubishi Fuso.

Ajali hiyo ilitokea kwenye eneo la Iyovi, Kijiji cha Msimba, Tarafa ya Mikumi, mkoani humo.

Mazishi hayo yalifanyika katika makaburi ya Msamvu, Kata ya Ruaha, wilayani Kilosa yakihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini, taasisi na wananchi.

Alisema vifo hivyo vinatia uchungu kutokana na marehemu hao kuzikwa katika kaburi moja na kufafanua kuwa, amefanya mazungumzo na viongozi wa madereva wa mabasi ya abiria na kudai kama ikifika Aprili 17, mwaka huu hawajapewa mikataba ya ajira, watagoma Aprili 18, mwaka huu,

"ACT-Wazalendo tunaitaka Serikali iwabane wamiliki wa mabasi ili hawa madereva wapewe mikataba," alisema.

Akiuzungumzia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Bw. Kabwe alisema wao hawaupingi umoja huo kwani kazi wanayoifanya ni kuiondoa Serikali ya CCM madarakani lakini hawahitaji vyama visivyo na uzalendo.

"Asilimia 50 ya viwanda vya sukari viko hapa Morogoro na hakuna kiwanda vipya zaidi ya vile alivyojenga hayati Mwalimu Nyerere; lakini vinawanyonya wakulima wa miwa na kusababisha kilimo chao kutowafaidisha," alisema.

Alisema mkoa huo ni wa sita kuchangia pato la Taifa upande wa Tanzania Bara, lakini upo chini kwa maendeleo ya watu ukishika nafasi ya 11.

Aliongeza kuwa, changamoto kubwa ipo kwenye elimu ambapo kati ya watu 100 mkoani humo, wanane ndio wenye elimu ya sekondari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bi.Anna Mghwira, alisema ACT itaondoa migogoro ya ardhi kwa kuhakikisha kuna mipaka ya wakulima, wafugaji.

Alisema watapiga marufuku wawekezaji kuwakodishia ardhi wakulima ili ardhi hiyo imilikishwe kwa wakulima.

"Kumuenzi Mwalimu ni kukataa ubinafsishaji holela na ujamaa ulijenga viwanda...mfumo wa sasa umeuza viwanda
na watu hawana ajira," alisema Bi. Mghwira.

Aliongeza kuwa, ujamaa ulikuwa na faida zaidi kuliko sasa; hivyo chama hicho kitamuenzi Mwalimu kwa kupinga sera za ubinafsishaji na watahakikisha mali za wananchi hazitaifishwi bali watarekebisha makosa ya ubinafsishaji kwa kurejesha mali zote za Taifa zilizouzwa.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu, Damiano Mkumbo kutoka Singida anaripoti kuwa, Bw. Kabwe na viongozi wengine wa chama hicho, kesho wanatarajia kuanza ziara ya siku mbili mkoani humo ili kuimarisha chama.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo, Bw. Wilfred Kitundu, alisema Bw. Kabwe atafungua matawi tisa na ofisi tatu za kanda, kuhutubia mkutano wa hadhara Mjini Singida.

"Ziara hii itaanzia katika Wilaya ya Manyoni kuanzia asubuhi ambako atafungua Tawi la Kitinku, pia atakwenda Mjini Singida ambako atafungua matawi matatu ya Kisaki, Utemini, Ukombozi.

"Bw. Kabwe pia atakwenda Wilaya ya Iramba Aprili 16, mwaka huu, atafungua matawi ya Ulemo, Misigiri na Sokoni Kiomboi, ofisi ya kanda na kwenda mkoani Shinyanga," alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment