SIKU moja baada wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, kutishia kuzifuta asasi za kiraia na kidini zinazohamasisha wananchi kupigia kura ya 'hapana' Katiba Pendekezwa, baadhi ya asasi mkoani Simiyu zimeshangazwa na tamko hilo.
Juzi waziri huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alisema atawashughulikia wote wanaotishia amani na usalama kuelekea kura ya maoni na Uchaguzi Mkuu pamoja na kutishia kuzifungia asasi za kiraia na kidini zinazohamasisha wananchi kupigia kura ya 'hapana' Katiba Pendekezwa.
Asasi hizo zimeeleza kushangazwa na tamko la Waziri linalodhihirisha kuwa na hofu ya utendaji kazi wake; na ndiyo maana anahoji jinsi ya upigaji kura unavyo hamasishwa na asasi hizo.
Kaimu Mchungaji wa dhehebu la Kilutheri Tanzania, Jimbo la Bariadi Usharika wa Tumaini Dayosisi ya Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria, iliyopo mkoani hapa, Mchungaji Israel Kimaro, alihoji ni kwa nini waziri asingetaja taasisi hizo.
Alisema kulingana na mamlaka aliyonayo alikuwa na uwezo wa kuchunguza kwanza ni asasi gani na maaskofu wapi wanajihusisha na kampeni hizo kwa waumini wao na si kukurupuka kutoa tamko la kuzifungia asasi za kidini.
“Endapo asasi hizo zitafungwa kuna uwezekano wa amani na utulivu uliopo hapa nchini ukatoweka,pia kama mtu yuko mahututi na ikashindikana kupatiwa matibabu; huyo ni mahututi tu na lazima atakufa,hivyo kama chama kinaonyesha ishara ya kufa basi kitakufa tu,” alisema Kimaro.
Naye Mwenyekiti wa Mtandao wa Asasi za kiraia wilayani Maswa, Nicodemus Luta,alisema kitendo cha waziri huyo kutoa tamko hilo ni kuwanyima wananchi pamoja na asasi haki ya kidemokrasia ya kuamua mambo katika nchi yao.
Aliongeza kuwa kuzifungia asasi za kiraia na kidini kuna taratibu zake, hivyo alimtaka waziri atoe ushahidi wa asasi zinazotuhumiwa kuliko kujumuisha asasi zote.
Alisema ni vigumu kutenganisha siasa na dini." Mbona Serikali imekuwa ikiwahimiza viongozi wa madhehebu ya dini kuhubiri amani na upendo hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu?" alihoji.
“Kwa nini Serikali inahamasisha kura ya ndiyo katika Katiba Pendekezwa huku upande wa pili ikiwakataza wasihamasishe kupigia kura ya hapana wakati Katiba Pendekezwa ni ya mwananchi kupiga kura ya ndiyo au hapana,”alihoji Luta.
Akizungumzia suala la asasi za kiraia na kidini kuchangisha fedha kwa ajili ya kumpa mmoja wa wagombea kuwania urais, alisema hilo si tatizo kwani wenye maamuzi ya kumchagua kiongozi wao ni wananchi.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment