Polisi Wamtaka Gwajima Atoe Uthibitisho wa Uhalali wa Mali Anazozimiliki Mpaka Kanisa Analoliongoza

Sasa ni dhahiri kwamba polisi wamemshika pabaya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima baada ya kumhoji na kisha kumtaka arejee katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Aprili 16, mwaka huu akiwa na vitu 10 vinavyohusu usajili, umiliki, uongozi na mali za kanisa analoliongoza.
Hatua hiyo imekuja kinyume na matarajio yake na ya wengi kuwa kiongozi huyo angekuwa anahojiwa tu kuhusu matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa kuripoti polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu lakini kabla ya mahojiano yao kukamilika aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa na kuhojiwa taarifa binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.
Hata baada ya kutoka hospitalini, Gwajima aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia hadi Aprili 6 alipohubiri katika Ibada ya Pasaka.
Siku iliyofuata askofu huyo alitupa kiti hicho akidai kuwa amepona baada ya maombi ya wachungaji wageni waliofika kanisani hapo kutoka Japan.
Baada ya mahojiano ya jana, wakili wake, John Mallya alilalamikia hatua ya polisi akisema mahojiano kuchukua mkondo wa mambo binafsi badala ya kile alichoitiwa na kusema watakwenda kulalamikia hatua hiyo mahakamani.
Mambo 10
Wakili huyo alitaja mambo yanayotakiwa kuwasilishwa polisi kuwa ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Mallya alisema watalalamika suala hilo litakapofika mahakamani kutokana na mteja wake kuhojiwa masuala tofauti na kile kinachodaiwa kutoa lugha ya matusi.
Alisema mteja wake amehojiwa muda mrefu kwa sababu alikuwa akihojiwa masuala binafsi yakiwamo ya familia yake, watoto wake, ndugu zake hadi waliokufa.
“Mahojiano yamekuwa ya muda mrefu, cha kushangaza kaulizwa maswali binafsi badala ya kile anachodaiwa kukifanya, mahakamani tutahoji hilo,” alisema Mallya.
Alisema licha ya kuambiwa walete vitu hivyo ambavyo kimsingi vipo, hawajaambiwa watafanywa nini kama wasipoviwasilisha.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment