Breaking News: Utata Polisi Aliyejiua kwa Risasi Kituo cha Polisi Mkoani Tabora

Taarifa za kusikitisha zinaeleza kuwa polisi aliyetambuliwa kwa jina la Charles mwenye namba H 3416 wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, amejiua kwa kujipiga risasi akiwa ndani ya kituo.


Kwa mujibu wa taarifa, Charles alikuwa kazini na alijiua Jumamosi usiku na sababu za kujiua kwake hazijafahamika.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi walio jirani na kituo hicho, walisema tukio hilo lilitokea saa moja jioni.


“Nilikuwa nyumbani ghafla nikasikia mlio wa risasi katika kituo cha polisi na nilipokwenda nilimkuta askari Charles amekufa kwa kujipiga risasi,” alisema Furahisha Felix.


Wananchi hao walisema kutokana na hali hiyo walilazimika kuwauliza baadhi ya askari waliokuwa naye zamu, ambao nao walidai hawajui sababu za mwenzao kuchukua uamuzi huo.


“Haiwezekani polisi ajiue na isijulikane sababu, hilo halipo, lazima kuna jambo limejificha,”alidai mkazi mwingine Amani Ibrahim.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Suzana Kaganda alisema: “Ni kweli askari huyo amejiua wakati akiwa kituoni saa moja usiku, tunaendelea na uchunguzi kujua sababu za kifo chake,”alisema Kaganda.

Kamanda Kaganda alisema askari huyo hakuacha ujumbe wowote kueleza sababu za kujiua.

Kutokana na tukio hilo, alitoa wito kwa askari wote kwamba wanapokuwa na matatizo wayawasilishe kwa viongozi wao badala ya kujichukulia sheria mkononi.

Matukio ya polisi kujiua

Hili ni tukio la pili la askari kujiua ndani ya kituo kwa mwaka huu, huko wilayani Mbozi mkoani Mbeya, polisi mwenye cheo cha Sajenti, D 4179 Partick Gondwa (54), alijiua kwa kujipiga risasi akiwa ndani ya kituo.

Askari huyo ambaye, pia alikuwa ni mtunza vielelezo kwenye kituo hicho cha Polisi Wilaya ya Mbozi, inasemekana alijipiga risasi kwa kutumia bastola ambayo nayo ni kielezo kilichokuwamo ndani ya chumba hicho.

Chanzo: Mwananchi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment