Lissu Funga Kazi , Bunge laweka Rekodi Mpya

Hoja 22 za kupinga vifungu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 zilizotolewa juzi na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu jana zilisababisha kikao cha 14 cha Bunge kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6.15 usiku.

Marekebisho yaliyowasilishwa na Lissu yaliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye pia alikuwa na marekebisho yake katika muswada huo, hivyo wote wawili kuichachafya Serikali bila mafanikio baada ya muswada huo kupitishwa kwa sauti kubwa ya “Ndiyooo” ya wabunge wa CCM.


Kuanzia saa 12.30 jioni, Bunge lilikaa kama kamati kupitisha muswada huo baada ya kumaliza kuupitisha muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ambao haukuwa na mvutano mkali.


Mvutano wa kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, naibu wake, January Makamba ulianza saa 12.30 jioni hadi saa 5.30 usiku na baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.


Mpaka inafika saa 5.00 usiku wabunge wa upinzani waliokuwapo bungeni walikuwa 12 tu, akiwamo Lissu na Mnyika na hivyo kufanya idadi ya wabunge wote kuwa 86, wakiwamo wa CCM na mawaziri.


Kuna wakati Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alilazimika kusimama kutoa ufafanuzi wa kina, ikiwa ni pamoja na namna ya kuvitamka kwa ufasaha vifungu vya sheria ili kukubalika na pande mbili zilizokuwa zinavutana.


Mapendekezo yote yaliyotolewa na Chenge ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaliungwa mkono na Lissu pamoja na Masaju na Wizara ya Mawasiliano.


Wakati mnyukano huo ukiendelea, Pinda alikuwa kimya akisubiri kusoma hotuba yake ya kuahirisha Bunge.


Pinda alianza kusoma hotuba hiyo saa 5.30 usiku mpaka saa 6.00 usiku, ikiwa ni baada ya Bunge kuupitisha muswada huo. Baada ya dakika 15 za kutoa matangazo mbalimbali na kuwashukuru wabunge, Spika Makinda aliahirisha mkutano huo.


Kuna wakati Lissu aliwataka wabunge kutochoka kutokana na hoja anazozitoa kusababisha kikao hicho kuwa kirefu, huku Makinda naye akiwaeleza wabunge kuwa ‘zege halilali’, akimaanisha kuwa Bunge haliwezi kuahirishwa mpaka muswada huo upitishwe na Pinda atoe hotuba ya kuahirisha Bunge.


Kati ya marekebisho 22 yaliyowasilishwa na Lissu, ni matano tu yaliyokubaliwa na Serikali huku Lissu akikubali vifungu viwili tu vilivyofanyiwa marekebisho na Serikali, akivisifia kuwa vimeandikwa kama sheria inavyotaka, lakini vingine akiviita vya ovyo na sheria inayotungwa ni mbaya yenye malengo ya kuwakomoa baadhi ya watu.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment