Mbio za Urais 2015: Hoja ya Upimaji Afya Urais Yaibuka Tena

BAADHI ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamesema hoja ya Jukwaa la Katiba nchini (JUKATA), kutaka wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao wapimwe afya kabla ya kuingia katika kinyang'anyiro hicho ni ajenda ya msingi inayopaswa kuungwa mkono na chama hicho.

Wakizungumza na Majira mwishoni mwa wiki, makada hao walisema ushauri uliotolewa na JUKATA utakiwezesha CCM kumpata mgombea anayeweza kuhimili mikiki ya kampeni za urais na kunadi sera za chama hicho bila wanachama kuwa na mashaka naye juu ya afya yake.

Makada hao walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa, chama hicho kisifanye makosa ya kuchagua mgombea anayetumia nguvu ya pesa kuwanunua watu wa kumshabikia ili jamii iamini kuwa mgombea huyo ndiye anayestahili.

Walisema mgombea wa aina hiyo ni mtu hatari ambaye nyuma yake ana kundi kubwa la watu wenye fedha ambao ameingia nao mkataba wa kuwalipa fadhila akipitishwa kugombea urais katika chama na kushinda nafasi hiyo.

"Mgombea wa aina hii akiingia madarakani, kazi ya kwanza ni kulipa fadhila kwa marafiki waliotumia fedha zao kumwezesha
aingie madarakani, atatumia rasilimali za nchi kujinufaisha yeye binafsi na marafiki zake hivyo kusababisha uchumi wa nchi kuyumba na umaskini kuongezeka," walisema.

Waliongeza kuwa, mgombea urais ambaye ataweza kukivusha chama hicho na kukipa ushindi wa kishindo lazima awe msafi, mwadilifu, mzalendo, asiye na kashfa, mwenye uwezo wa kutatua kero za wananchi na kufanya maamuzi.

Miongoni mwa makada ndani ya CCM wanaotajwa kutaka kuwania nafasi hiyo ambao baadhi yao tayari wametangaza nia ni pamoja na Bw. Edward Lowassa ambaye alijiuzulu Uwaziri Mkuu kutokana na kashfa ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond Development (LLC).

Wengine ni Mbunge wa Nzega, Dkt. Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Stephen Wassira na Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye.

Makada wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, Mbunge wa Sengerema, Bw. William Ngeleja, Naibu Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

"Nafasi ya urais ni nyeti, mgombea wake lazima apimwe afya, nchi ya Zambia imepata fundisho baada ya marais wake wawili kufariki dunia wakiwa Ikulu katika kipindi cha miaka sita akiwemo marehemu Michael Satta.

"Nchi hiyo iliingia gharama za kuchagua marais mara mbili wakaamua kuwa na mtazamo wa kupima afya za wagombea urais kabla ya kuingia Ikulu, nasi tunapaswa kuiga mfano huo kwa sababu wapo baadhi ya wagombea wanaotajwa ambao hatuamini kama wataweza kuivusha nchi hapa ilipo kwa sababu za kiafya," walisisitiza makada hao.

Wakimnukuu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, makada hao walisema kiongozi huyo aliwahi kutoa msimamo wake juu ya hoja hiyo akivitaka vyama vyote vya siasa, kuhakikisha haviteui wagombea dhaifu kiakili, kimwili, kimaadili na mchakato wa kuwachuja uzingatie vigezo hivyo katika vikao vya uteuzi.

Makada hao walisema uteuzi wa wagombea ndani ya CCM, baada ya kuchukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo, wanatakiwa kutafuta wadhamini katika mikoa 10 na kuzirudisha katika chama.

Majina ya wagombea hao yatapelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itayapitia na baadaye kupelekwa Kamati Kuu kwa ajili ya uteuzi wa majina matano ambayo yatapelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili majina hayo yaweze kupigiwa kura na kupatikana majina matatu.

"Baada ya kupatikana majina matatu, yote yatapelekwa katika Mkutano Mkuu wa chama ambao utapiga kura ili kumpata mgombea mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu ujao," walisema.

Wakizungumzia juu ya makundi mbalimbali ya watu kumshawishi Bw. Lowassa achukue fomu za kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, walisema hawaamini kama watu hao walikwenda nyumbani kwa Mbunge huyo kwa utashi wao bali waliandaliwa mazingira ya kufanya hivyo.

Walisema pamoja na Bw. Lowassa kujitetea baada ya chama kutoa tamko akisema kinachofanywa na makundi hayo ni utashi wao, majibu hayo hayana mashiko ndani ya chama kwa sababu mchakato wa kumpata mgombea unafahamika.

"CCM haichagui mgombea urais kwa utashi wa kikundi cha watu wachache walioandaliwa kupiga kelele ili umma uamini kile wanachokitaka wao...kuna vikao vinavyokaa kufanya maamuzi yanayostahili ili kumpata mgombea," walisema.

Hivi karibuni, Bw. Lowassa alikuwa akitembelewa na makundi mbalimbali ya watu nyumbani kwake Monduli, mkoani Arusha na Dodoma ili kumshawishi achukue fomu ya kugombea urais ambapo CCM kilitoa tamko la kumtaka asitishe kuyapokea kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni, taratibu na Katiba ya chama.

Katika majibu yake, Bw. Lowassa alisema hawezi kuzuia mafuriko kwa mikono lakini aliyataka makundi hayo yasubiri utaratibu utakaotolewa na chama jambo ambalo lilipongezwa na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Bw.Naye Nnauye ambaye ndiye aliyetoa tamko la chama.

Bw. Nnauye alisisitiza kuwa, makada wote wenye dhamira ya kuwania urais, wanapaswa kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama si kuanza kampeni kabla ya wakati.

"Ni makosa makubwa kuanza kampeni kabla ya wakati, hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa, hiki ambacho nakisema ni msimamo wa chama si wangu binafsi kwa sababu mimi ndiye msemaji wake," alifafanua na kuongeza kuwa;

"Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu hivyo lazima nisimamie misingi ya itikadi, kanuni na Katiba ya chama chetu, siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea," alisema Bw. Nnauye.

Credit: Majira
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment