Mapendekezo ya CAG Yanapuuzwa

Ushauri unaotolewa mara kwa mara kwa Serikali, taasisi zake na mashirika ya umma umekuwa ukipuuzwa na kusababisha Serikali kuendelea kupoteza fedha nyingi kwa njia ya ufisadi huku Deni la Taifa likizidi kukua, kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ripoti ya CAG imeweka bayana ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha na ripoti hiyo maalum inaonyesha kuwa uovu huo umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa uchanganuzi wa Mwananchi, Sh600 bilioni zilizofanyiwa ufisadi, zingeweza kusaidia kupunguza nakisi kwenye bajeti ya Serikali kwa kuelekezwa kwenye wizara tatu ambazo ni Ofisi ya Rais, iliyopangiwa Sh587 bilioni, Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh68.8 bilioni) na Ofisi ya Makamu wa Rais (Sh112 bilioni).
Pia, fedha hizo zingeweza kujenga vyumba 8,000 vya madarasa kwa gharama ya Sh75 milioni kila kimoja au kuwezesha vijana zaidi ya mara 12 ya fedha zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete, au kujenga kilomita 600 za barabara kwa kiwango cha lami.
Ukaguzi huo maalumu ulifanywa ili kuangalia kama rasilimali zilizotengwa zimetumika kwa ufanisi kwa kuzingatia kiwango cha fedha kilichowekezwa, tija na ufanisi kama ilivyotarajiwa na kupitishwa na Bunge kwenye maeneo kadhaa, inaeleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapendekezo ya CAG yalitolewa katika ripoti tano za ukaguzi wa ufanisi za miaka ya nyuma kwenye maeneo ya usimamizi wa udhibiti wa athari za mafuriko kwa Serikali, mikoa na serikali za mitaa uliofanyika kwa kutumia mafuriko yaliyowahi kutokea Babati (2007).
Vilevile, mapendekezo hayo yalilenga katika kuboresha usimamizi wa utoaji wa huduma ya afya ya msingi, ukaguzi uliofanyika kwenye vituo vya afya (2009); programu za ukaguzi wa shule za sekondari nchini (2009) na usimamizi wa udhibiti wa taka ngumu nchini na usimamizi wa ujenzi wa barabara (2010).
Sehemu nyingi za matokeo ya uchunguzi kwenye ripoti hiyo zinaonyesha kuwa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG ulifanywa chini ya asilimia 50.
Mapendekezo hayo yalikuwa kwenye utunzaji wa kumbukumbu za miradi na kuwapo mfumo wa ufuatiliaji, miradi kuchelewa kumalizika na kuongeza gharama, ukusanyaji mapato, utoaji wa fedha kwa taasisi za Serikali kama Bohari ya Madawa ili kusaidia kupunguza ongezeko la Deni la Taifa, halmashauri kuwa na mifumo bora ya utoaji kandarasi, mfumo wa ufuatiliaji wa taarifa za wakaguzi wa elimu wa shule za sekondari na ugawaji na usimamizi wa dawa na vifaa tiba.
Wizara ya Ujenzi, ambayo mwaka jana iliidhinishiwa Sh1.22 trilioni, inaelezwa kutofanya tathmini ya kutosha kabla ya kuanza miradi ya ujenzi wa barabara na kusababisha ichukue muda mrefu kukamilika kutokana na makandarasi kusubiri kuondolewa kwa nyaya za simu, mabomba ya maji na miundombinu ya umeme.
Pia, wizara husababisha ongezeko la gharama za miradi kutokana na kuwapo na tofauti kubwa ya makadirio ya awali na gharama halisi. “Ufuatiliaji uliofanywa kwenye utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa umebaini kuwa kumekuwa na pungufu kwenye ufanisi wa udhibiti wa bajeti ambao ungeweza kusaidia kuzuia ongezeko la gharama kati ya bajeti ya mwanzo na bajeti iliyofanyiwa marekebisho kwenye miradi ya Ujenzi wa barabara nchini,” inasema ripoti hiyo.
Katika ukaguzi huo CAG anaonyesha jinsi kulivyokosekana ushahidi wa kuondolewa kwa mali zinazopita nchini kuelekea nchini jirani na kubakizwa na kisha kuingizwa sokoni, hivyo Serikali kukosa makusanyo ya kodi ya Sh835 bilioni.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment