Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Karagwe imebatilisha ushindi wa wenyeviti 36 wa vitongoji, Kata ya Kiruruma kwa tiketi ya CCM, baada ya kuridhika kuwa mwenendo wa uchaguzi haukuwa huru na haki.
Hatua hiyo imetokana na kesi iliyofunguliwa na wagombea 36 wa Chadema waliopinga kuenguliwa kuwania nafasi za uenyekiti wa vitongoji katika kata hiyo.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Victor Bigambo alisema kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa, Mahakama imeridhika pasi na shaka kuwa utaratibu uliotumika kuwatangaza washindi hao wa CCM haukufuata kanuni na sheria zilizokuwa zinaongoza Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Desemba 14, mwaka jana.
Katika uchaguzi huo, wagombea wote Chadema katika kata hiyo, walienguliwa baada ya kuwekewa pingamizi la kutumia muhuri wa Katibu wa Chadema kwa madai kuwa haukuonyesha jina la tawi.
Hakimu Bigambo alisema kutokana na ukiukwaji huo wa kanuni, uchaguzi huo ni batili hivyo nafasi hizo zitangazwe upya na kumwagiza msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Karagwe kuitisha uchaguzi kuzijaza. Pia, alisema walalamikiwa wanatakiwa kulipa gharama za uendeshaji kesi hiyo.
Wanachama hao Chadema walikuwa wakitetewa na Wakili Revocutus Mathayo ambaye aliieleza Mahakama hiyo kuwa kutokana na kuenguliwa, wateja wake walipata madhara makubwa ikiwamo ya kisaikolojia na kutoweka kwa amani kwenye jamii.
Wakili Mathayo alidai kuwa kutokana na kutowasilisha vielelezo vya kuthibitisha ushindi wa waliotangazwa kutoka CCM, ni dhahiri kuwa kanuni na sheria zilikiukwa kuwapata washindi hao. Kesi hiyo hiyo ni miongoni mwa nyingine kadhaa zilizofunguliwa baada ya uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo mbalimbali nchini kwa ukiukaji wa taratibu.
Katika maeneo hayo mamia ya wagombea wa CCM walipita bila kupingwa kutokana na kilichoelezwa kuwa wenzao wa Chadema walikosa sifa kwa kukosea kujaza fomu au kuidhinishwa na maofisa wa chama wasioruhusiwa kikanuni.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment