Mbunge Amjia Juu DC Sakata la Wanawake wa Rombo

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amewajia juu Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Lemrise Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya hiyo, Anthony Tesha akiwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia sheria wilayani humo.
Selasini alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumzia taarifa ya wanawake wa Rombo inayodai kwamba wanakodi wanaume kutoka Kenya ili wafanye nao tendo la ndoa.
Juzi, gazeti hili liliripoti habari iliyomkariri Mkuu wa Wilaya kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo, hukodi wanaume kutoka Kenya kwa ajili ya kufanya nao tendo la ndoa baada ya waume zao kupoteza nguvu kutokana na ulevi.
Eneo ambalo limeathirika zaidi na unywaji wa pombe haramu na zinazotengenezwa kiholela bila viwango ni la Kikelelwa lililopo mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Taarifa hiyo ilimnukuu Kipuyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo na kuitaja Kikelelwa kama eneo linalohitaji kutazamwa kwa jicho la pekee.
“Imefikia mahali wanaume wengi wanashindwa kumudu kufanya tendo la ndoa na kuwalazimu wanawake wao kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya tendo hilo,” alisema Kipuyo.
Kauli hiyo iliungwa mkono na baadhi ya wanawake waliozungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya katika operesheni ya kukamata pombe haramu ya gongo kijijini hapo iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Jana, Selasini alikanusha vikali taarifa hizo akidai kuwa siyo sahihi kuwajumuisha wanaume wote wa jimbo lake na ulevi huo au wanawake wote.
“Hiyo kauli haina utafiti wala haijaonyesha ni wanaume wangapi Rombo wana tatizo hilo au ni wanawake wangapi waume zao wana shida hiyo. Siyo sahihi kutoa kauli ya jumla,” alisema.
Alisema, “Haiwezekani mtu mmoja aliyehojiwa akawakilisha wanaume au wanawake wenye matatizo hayo. Kauli hiyo imewadhalilisha wanaume na wanawake ambao hawahusiki na tatizo hilo.”
“DC ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama aliyepaswa kusimamia sheria. Mwenyekiti wa halmashauri, naye anawajibika. Kama wameshindwa kazi waachie ngazi.
“Siungi mkono unywaji holela wa pombe ambazo hazina viwango vya TBS. Kama kuna mtu ana tatizo la tendo la ndoa ajitokeza tumjue. Hili jambo limenifanya nipokea simu nyingi sana,” alilalamika Selasini.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment