Sarafu ya Sh 500 Yatengenezewa Mikufu

SARAFU mpya ya shilingi 500 inadaiwa kuhujumiwa na baadhi ya watu ambao huinunua kwa Sh 2,500 na baadaye kuiyeyusha kwa ajili ya kutengenezea mikufu ya fedha (silver).
Taarifa ambazo MTANZANIA imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza tangu sarafu hizo zilipotolewa kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka jana, baadhi ya watu wamekuwa wakizikusanya na kuzifanya kuadimika mtaani.
Imeelezwa kuwa tangu kutolewa kwa sarafu hiyo imekuwa adimu mitaani jambo ambalo si kawaida kwa fedha mpya zinazoingizwa kwenye mzunguko kuadimika kwa kiwango hicho.
“Nimekutana na watu watatu wakitafuta sarafu ya Sh 500 kwa Sh 2,500 hadi 5,000, mwanzoni nilipuuza lakini baada ya kutulia na kufanya utafiti nimegundua kwamba kwanza hii sarafu imekuwa adimu na inatafutwa kwa udi na uvumba,” kilisema chanzo chetu cha habari jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu hujuma hizo, Meneja Sarafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Jovent Rushaka, alisema taarifa hizo wanazo na wanazifanyia kazi.
“Taarifa hizo tumezipata juzi na tunalifanyia kazi suala hilo, kwa sasa tunafanya uchunguzi zinakofanyiwa kazi, zinakouzwa ili tuweze kwenda katika maduka hayo na kufanya uchunguzi,” alisema Rushaka.
Katika hatua hiyo, meneja huyo aliwataka Watanzania kwa yeyote atakayebaini sehemu zinakotengenezwa na kuuzwa atoe taarifa.
Alipoulizwa kuhusu aina ya madini iliyotengenezewa sarafu hiyo ya Sh 500, alisema imetengenezwa kwa madini ya chuma kwa asilimia 94.
“Asilimia sita iliyobaki imetengenezwa kwa madini aina ya nickel plated silver ambayo kidogo unaweza kutengenezea mikufu ya ‘silver’. Sasa ni mtu gani anayenunua madini ya chuma ni vigumu kuwezekana sasa, maswali ya kujiuliza ni je, imetengenezwa na hiyo nickel plated silver?” alihoji Rushaka.
Alipoulizwa sababu za sarafu hiyo kuadimika imetokana na nini, alisema BoT ilitoa sarafu hiyo tangu Oktoba mwaka jana na kwamba bado wanazo nyingi.
“Tangu Oktoba mwaka jana tumezitoa nyingi kupitia Commercial Bank (benki za biashara) na kama kuna mtu anahitaji aende kwenye benki hizo halafu atapewa kwa sababu sisi tunasambaza kupitia benki hizo,” alisema Rushaka.
Hata hivyo taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na BoT jana ilisema asilimia 94 ya madini katika sarafu ya Sh 500 ni chuma na asilimia 6 ni Nickel.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki BoT, Marcian Kobello ilieleza kuwa hadi sasa sarafu za Sh 500 zenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni moja zimesambazwa kote nchini.
Pia aliongeza kuwa Nickel sio miongoni mwa madini maarufu kwa ajili ya kutengeneza vidani vya thamani.
“Hakuna kabisa madini ya fedha katika sarafu ya shilingi 500,” alisema Kobello na kuongeza kuwa haitegemewi kwamba mfanyabiashara yeyote anaweza kununua sarafu hiyo kwa bei ya juu kuliko thamani yake halisi.
“Kwa hiyo, tunapenda kuwafahamisha wananchi kwamba kuna kiasi cha kutosha cha sarafu za shilingi 500 nchini na kwamba kununua sarafu hiyo kwa bei ya juu kuliko thamani yake ni kujiingizia hasara,” alisema mkurugenzi huyo.
Credit: Mtanzania
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment