Membe- Wakati Ukifika Nitachukua Fomu

Siku mbili baada makada waliokuwa wamefungiwa kwa makosa ya kukiuka kanuni za CCM kuachiwa huru, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameeleza nia yake kuwa wakati ukifika atachukua fomu kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Membe alibainisha nia hiyo kwa mara ya kwanza juzi usiku wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na kuwa atatangaza azma hiyo muda wowote kuanzia sasa akiwa jimboni kwake, Mtama mkoani Lindi.
“Sasa ni rasmi kuwa nina nia ya kugombea urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitatangaza nikiwa kijijini kwangu… mahali nilipoanzia safari ya kwenda shule, safari ya kwenda usalama wa Taifa na safari ya kwenda Wizara ya Mambo ya Nje,” alisema.
Membe alikuwa miongoni mwa makada sita CCM waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi wakituhumiwa kuanza kampeni mapema kinyume na taratibu za chama hicho kilicholazimika kuwachukulia hatua za kinidhamu.
Makada hao walifungiwa tangu Februari, 2014 na pamoja naye ni mawaziri wakuu wa zamani; Frederick Sumaye na Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Akifafanua juu ya dalili za kutimia kwa ndoto yake za kuiongoza nchi, Membe alisema Mwenyezi Mungu ana namna nyingi za kufikisha ujumbe kwa mja ampendaye katika kumtumikia kwa mtindo autakao yeye. “Nimegundua kuwa unaposema naomba nioteshwe… naomba nioteshwe kumbe Mungu anayo namna nyingine. Anawaotesha wengine kwa ajili yako na ndivyo alivyofanya,” alisema.
Kuhusu hilo, Membe alisema kila mtu anasubiri kuona CCM inatoka vipi na hata vyama vya upinzani vinasubiri hilo na ndiyo maana navyo vimenyamaza.
Mpaka sasa ni chama cha Tanzania Labour (TLP), kilichokwisha teua mgombea wake wa urais katika uchaguzi huo, Macmillan Lyimo.
“Watanzania wote macho yao yapo CCM, wanasubiri kuona inafanya nini. Tunaona vyama vya vingine vimekaa kimya, wanasubiri CCM iseme ili nao wafuate. Wanapiga kelele za Ukawa…Ukawa lakini hawawezi kufanya chochote. Hata kama tutasogeza muda mbele bado wataendelea kusubiri,” aliongeza.
Hali ya usalama Burundi
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia hali ya usalama inayoendelea kuyumba nchini Burundi kwamba kikao cha mawaziri kinatarajia kuketi baada ya muda mfupi jijini Arusha ili kuona namna ya kutatua mzozo uliopo.


Alisema Tanzania isingekwa radhi kuona mapinduzi ya utawala wa Rais Pierre Nkuruzinza yanafanywa wakati akiwa nchini tena kwa mwaliko na gharama za nchi hii. Alisema hiyo ingemaanisha Tanzania inahusika nayo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment