Filimbi ya kuanzisha mbio za urais kwa tiketi ya CCM itapulizwa Mei 23 baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho tawala, huku makada sita walio ‘kifungoni’ wakitarajia kujua hatima yao kwenye mbio hizo Mei 20.
CCM imekuwa kimya kuhusu mchakato wake wa uchaguzi, unaohusisha ratiba ya chama hicho, kupitishwa kwa Ilani ya Uchaguzi na taratibu nyingine za kugombea uongozi, kiasi cha kutia wasiwasi baadhi ya wanachama wake, wakiwamo makada sita ambao walifungiwa kwa zaidi ya miezi 12 kujihusisha na kuwania madaraka baada ya kubainika kukiuka taratibu.
Makada hao waliopewa adhabu na Kamati Kuu ni mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine Steven waziri, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula, January Kamamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia) na William Ngeleja, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.
Mbali na makada hao, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba aliwahi kupewa barua ya katazo la kufanya ziara na mikutano ya kibinafsi yenye viashiria vya kampeni za urais.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuthibitisha kuwapo kwa vikao vya vyombo hivyo viwili wiki mbili zijazo.
“Kwanza habari hizo siyo za kweli, nazisikia kwa mara ya kwanza kutoka kwako,” alisema Nape alipoulizwa kuhusu tarehe za vikao hivyo.
“Kwanza umeshaandika stori yenu halafu ndiyo mnanipigia kuthibitisha. Inakuwaje msemaji wa chama hana habari, halafu nyinyi Mwananchi muwe nazo?” alihoji Nape.
Hata hivyo, habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20, kuandaa taratibu zote za uchaguzi na siku inayofuata, yaani Mei 21 iwasilishe kwenye kikao cha Halmashauri Kuu kitakachokuwa cha siku mbili.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment