Urais CCM Waiweka Pabaya Kamati Kuu

Mbio za urais ndani ya CCM sasa zimefikia pabaya baada ya kuibuka hofu ya kuwapo kwa mpango wa kuivuruga Kamati Kuu kabla ya haijakutana kuchuja majina ya makada watakaotakiwa kupigiwa kura na Halmashuri Kuu ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu.
Hadi sasa CCM haijatangaza ratiba yake kwa ajili ya kuongoza wanachama wanaotaka kuwania uongozi wa ngazi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho.
Hata hivyo, Mwananchi ilitaarifiwa wiki hii kuwa Kamati Kuu ya CCM itakutana Mei 20 na kufuatiwa na vikao vya siku mbili vya Halmashauri Kuu Mei 21 na 22 kwa ajili ya kupitisha ratiba, ilani na taratibu nyingine za uchaguzi, ikiwa ni kuashiria kuanza rasmi kwa mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho kikongwe.
Wakati chama kikitafakari kuanzisha rasmi mchakato wa uchaguzi, tayari kuna habari kuwa moja ya makundi ya makada wanaowania urais limeonyesha kutokuwa na imani na mwenendo wa Kamati Kuu ambayo ina jukumu la kuchuja wanaowania urais na kupeleka majina Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura.
Taarifa ambazo gazeti hili imezipata zinaeleza kuwa kundi hilo linashawishi wanachama ili wakubali kuomba kupiga kura ya kutokuwa na imani na Kamati Kuu kwa madai kuwa inaonekana kupendelea baadhi ya waliojitokeza na kubana wagombea wengine.
Chanzo chetu cha habari kimeeleza kuwa kundi hilo limekuwa likifanya vikao mbalimbali vya kuweka mkakati wa jinsi gani ya kuivuruga Kamati Kuu kabla ya kuchuja majina ya wagombea urais kwa tiketi ya CCM.
“Kuna mkakati wa kuweka CC itakayowasaidia kwa kuwa ukishapita hapo, umeshakuwa Rais wa nchi hii. Uzuri ukishinda ndani ya chama na kutangazwa kuwa mgombea wao, basi makundi yote hurudi kukipigania chama na wengine kujipendekeza ili wapewe nafasi katika serikali ijayo,” alisema mpashaji habari wetu ambaye ni mmoja wa viongozi wa juu wa CCM.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mpango huo unafanyika kwa umakini mkubwa ili kuweza kuhakikisha Kamati Kuu haikati jina la mgombea wa kundi hilo kama ambavyo imewahi kufanyika kwa makada wengine ambao majina yao hayakupelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura kutokana na nguvu yao kwenye chama.
Kama hilo litafanikiwa itakuwa ni kwa mara ya pili kutokea baada ya mwaka 1995, Jakaya Kikwete kumlalamikia aliyekuwa katibu mkuu wa CCM, Lawrance Gama kuwa hawezi kumtendea haki baada ya kuonekana akiwa amevaa nguo yenye nembo ya mmoja wa waliokuwa wakiwania kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
Alipoulizwa kuhusu mkakati huo, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kuwa wamesikia na kuelezwa kuwa kundi hilo linagawa fedha kufanikisha jambo hilo kwa kuwa wanadhani sekretarieti ya chama haiwapendelei wao.
“Wanadhani kuna watu wanapendelewa, kama suala hilo lipo bila shaka chama hakiwezi kukaa kimya kwani huo ni uasi na usaliti kwa chama,” alisema Nape.
Alisema kuwa ndani ya chama viko vyombo vingi ambavyo kama mtu ana shida anaingia kwenye mikutano sahihi ya chama.
Crdt: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment