KURA YA MAONI: Ukawa Wavutana Dar

Kitendo cha Chama cha Wananchi (CUF) kufanya uchaguzi wa Kura za Maoni katika majimbo ya Kawe na Ubungo yanayoshikiliwa na wabunge wa Chadema, kimeibua hisia tofauti miongoni mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mvutano huo unatokana na kinachoelezwa ni makubaliano ya vyama hivyo kuwa kila kimoja kiandae wagombea wake katika majimbo yote ambao watashindanishwa katika Ukawa, bila kuhusisha majimbo ambayo tayari yana shikiliwa na vyama vinavyounda umoja huo.
Mbali na kigezo hicho, mgawanyo wa majimbo unazingatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya madiwani kwa kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014, mtandao wa chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Juzi, CUF ilifanya uchaguzi wake wa kura za maoni katika Mkoa wa ya Dar es Salaam ambapo pamoja na majimbo mengine, iliwapitisha Leila Hussen kukiwakilisha chama hicho katika Jimbo la Kawe na Mashaka Ngole katika Jimbo la Ubungo.
Mvutano wenyewe
Kutokana na hatua hiyo, vyama vya NCCR-Mageuzi na NLD vimesema CUF imeanza kwenda kinyume na makubaliano ya Ukawa, ingawa CUF na Chadema wameeleza kuwa haikuwa kosa kufanya kura ya maoni kwenye majimbo hayo.
Ingawa viongozi hao wametofautiana kimtazamo kuhusu hatua hiyo ya CUF, wamesisitiza kuwa kuweka mgombea mmoja wa upinzani kupitia Ukawa bado ni njia sahihi na pekee itakayowezesha kuiondoa CCM.
Kauli ya NLD
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema Ukawa haijafikia uamuzi wa kuiachia Chadema majimbo ya Ubungo na Kawe, lakini CUF imekosea kuwasimamisha wagombea katika majimbo hayo kwa kuwa vikao vya kuwapata wagombea wa upinzani  bado vinaendelea.
“Ukweli ni kwamba hakuna kikao cha Ukawa kilichopitisha kuyaacha majimbo hayo kwa Chadema, ila CUF wamefanya kosa moja tu, kutangaza wagombea wake hadharani. Kama ni mchakato wa maandalizi, walipaswa kuwaanda wagombea hao ndani ya chama chao ili kusubiri uamuzi wa vikao vya Ukawa,” alisema Dk Makaidi na kuendelea;
“Hata sisi NLD tuna wagombea wetu  Dar es Salaam, lakini hatuwezi kuwatangaza kwa sababu tunasubiri vikao vya Ukawa.”
Alipoulizwa kuna tatizo gani kumtangaza mgombea sasa huku wakiendelea kusubiri vikao vya Ukawa alijibu, “Huku ni kuwachanganya wananchi. Kama kila chama kitatangaza mgombea wake sasa halafu Ukawa ikaja na mgombea mmoja, huku ni kuchanganya watu.”
Crdt: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment