Mbowe amesema hayo jana wakati akitoa maazimio ya mkutano wa Kamati Kuu ya Chama hicho iliyokutana jijini Dar es Salaam; Mbowe amesema kitendo cha kutoeleweka ni lini uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge utafanyika pamoja na mwelekeo wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ni moja ya sababu zinazochangia kuendelea kuzorota kwa hali ya uchumi.
Akifafanua kuhusu hoja hizo, Mbowe amesema wawekezaji hivi sasa wamekuwa wakiondoa mitaji pamoja na kupunguza uwekezaji wao nchini, sababu kubwa ikiwa ni kuhofia kuwa huenda nchi ikaingia katika matatizo na kwamba kuna haja ya serikali kuweka wazi mwelekeo wa mazoezi hayo mawili ili kurejesha imani ya wawekezaji kuwa hali ya kisiasa nchini siyo ya kutatanisha.
Kwa mujibu wa Mbowe, wawekezaji hao wamekuwa wakipeleka mitaji yao katika nchi nyingine wanazodhani zipo imara kisiasa na kwamba serikali iwe makini kwa kuweka wazi ratiba nzima ya lini uchaguzi utafanyika pamoja na kukamilika kwa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa upande wake, katibu mkuu wa chama hicho Dkt Wilbrod Slaa amezungumzia ushirikiano wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA na dhana nzima ya kuachiana maeneo ya kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.
Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa waandishi wa habari; Dkt Slaa amesema tofauti na inavyodhaniwa, UKAWA wanaongozwa na msimamo wa kuachiana maeneo ya kugombea kulingana na jinsi mgombea wa chama husika anavyokubalika katika eneo fulani na sio vinginevyo.
Aidha, mwanasiasa mkongwe na mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Profesa Mwesiga Baregu amesema kwa sasa hakuna mpango wowote wa kuviunganisha vyama hivyo ili kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba na kwamba mpango kama huo ni mtazamo wa baadaye iwapo vyama hivyo vitafanikiwa kuiondoa serikali ya CCM madarakani.
Crdt:Eatv
0 comments:
Post a Comment