SIASA: Vita ya Urais CCM Nje Nje

Wakati joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe, vita vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusema hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.


Mjumbe huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), pia alisema umoja huo haujafikia uamuzi wala kumtuma mtu kumdhibiti mwanachama anayetajwa kuwania urais.


Katika siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa ndani ya CCM juu ya mtu atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, na ilizidi baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa mwanachama ambaye atateuliwa na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa waliojitokeza na kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa wajitokeze.


Siku chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia wito wa Rais Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa kujitokeza.


Hadi sasa, wanachama waliojitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na Lazaro Nyalandu ambaye ni waziri wa Maliasili na Utalii.


Lakini pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini hawajatangaza ambao ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sita, William Ngeleja, Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen Wasira, Bernard Membe na Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya kambi yake na zinazompinga.


Mapema wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake vya kumshambulia Lowassa vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti, jambo ambalo limezidisha mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.


Kutokana na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM mkoani Arusha wametuma ujumbe wa maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa za chama hicho wakitaka wanachama wasifanyiwe kile wanachokiita kuchafuana na vitisho vya baadhi ya wagombea kukatwa kimizengwe.


Ujumbe huo ulitumwa juzi na mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole na mwenyekiti wa UVCCM, Robinson Meitinyiku ambao walitaka Sadifa Juma Hamis kueleza msimamo wa mkoa kwa vyombo hivyo viwili vya maamuzi, na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM aliwahakikishia kuwa hakuna mgombea atakayekatwa kwa “sababu za kijinga”.


Akijibu ujumbe wa viongozi hao, Sadifa aliyekuwa jijini hapa kumsimika kamanda wa vijana wa wilaya ya Arumeru, Mathias Manga, aliwaondolea hofu katika hafla hiyo akisema hakuna mgombea wa urais wa CCM ambaye atakatwa bila sababu za msingi, lakini akawataka vijana kusubiri zamu yao hadi 2025.


Kauli ya Sadifa


“Niwaombeni mwenyekiti wa mkoa na mwenyekiti wa UVCCM, msiogope. Hakuna mtu atakayekatwa kijinga ndani ya Kamati Kuu au Halmashauri Kuu. Kikubwa tufuate maadili. Mimi mchapakazi ndiye nitamtetea,” alisema bila kutaja mgombea anayekusudiwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment