Makatibu wa Chadema kutoka mikoa 20 ya Tanzania Bara, wanatarajia kufanya operesheni ya kuing’oa CCM katika Jimbo la Mwanga linaloshikiliwa na Profesa Jumanne Maghembe.
Katibu wa Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema jana kuwa watalishambulia jimbo hilo kama nyuki na kuliondoa kwenye mikono ya CCM.
“Tutakutana pale kuanzia Machi 6 na baada ya makamanda hawa kukutana, watatawanyika kwenye vitongoji vyote 282 vya jimbo hilo kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi ya chini,” alisema.
Lema alisema lengo la operesheni hiyo ni kuunga mkono kazi iliyofanywa na Katibu wa Chadema, Mkoa wa Kinondoni, Henry Kilawo tangu mwaka 2011 na kukiletea chama mafanikio ya kisiasa.
“Tunataka kuweka historia ya kuondoa watu wanaotawala majimbo kifalme. Kazi tutakayoifanya ndiyo itakayofanyika katika majimbo mengine, uzuri wao (CCM) Mwanga hawaelewani,” alisema Lema.
Profesa Maghembe ambaye pia ni Waziri wa Maji alipoulizwa na gazeti hili kuhusu operesheni hiyo, alisema hatishiki kwa sababu amejenga misingi imara ya kukubalika.
“Wao waje tu kwa sababu nimewazoea kwa mbwembwe zao mwisho wa siku wanaondoka wameinamisha vichwa chini. Mimi najivunia rekodi yangu ya utendaji,” alisema Maghembe.
Katika hatua nyingine; Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo amesema kitendo cha Kamati Kuu cha kumuengua katibu aliyeshinda Moshi Vijijini, Emanuel Mlaki kitakuja kukigharimu chama baadaye.
Mwaka jana, wajumbe wa Baraza la Mashauriano walimchagua Mlaki kuwa katibu kwa kura tisa, huku Akwilin Chuwa akipata nne.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema kamati imerejesha jina la Chuwa na Mlaki ataendelea kubaki kuwa katibu wa jimbo.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment