Matokeo ya Mtihani Kidato IV Kutangazwa Jumapili Fahamu Jinsi ya Kuyapata Kirahisi

Matokeo ya mitihani ya kidato cha nne nchini ya mwaka 2014, yanatarajiwa kutangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Jumapili wiki hii.
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde (pichani), alitoa ahadi hiyo kama zawadi kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpwapwa mkoani Dodoma, kufuatia ajali ya moto iliyotokea Januari  20, mwaka huu na kuteketeza mali zote zilizokuwa kwenye bweni la wasichana 64 wa kidato cha tano na cha sita.
Dk. Msonde alikuwa miongoni mwa viongozi walioongozana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi-Elimu), Kassim Majaliwa, kwenye ziara ya kutoa pole katika shule hiyo.
“Zawadi niliyowaandalia ni taarifa kwamba Februari 15, mwaka huu, tutatangaza matokeo ya mitihani iliyofanywa na watahiniwa wa kidato cha nne nchini. Nasema ni zawadi kwa sababu sijaitoa mahali kokote, nyie ndiyo wa kwanza kuipata,” alieleza Msonde.
Watahiniwa waliotarajiwa kufanya mtihani huo Novemba, mwaka jana ni 297,488 huku watanihiwa 245,030 wakiwa wa shule na watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 52,448. Watahiniwa wa shule walioandikishwa ni wavulana 132,244 (asilimia 53.97) na wasichana 112,786 (asilimia 46.03).
Kwa kawaida, matokeo ya kidato cha nne hutolewa Aprili, lakini mwaka huu yatatoka mapema kutokana na uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu. Walimu ni miongoni mwa watumishi wa serikali ambao hutumiwa kusimamia uchaguzi mkuu.
Kupitia ziara hiyo, Serikali imepeleka vitanda 64 ambapo magodoro 64 yalitolewa na Mbunge wa Kibakwe ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
Pamoja na misaada hiyo, aliahidi kupeleka madaftari, mikebe ya vifaa vya hisabati, kalamu na kumpa kila mwanafunzi aliyekuwa akiishi kwenye bweni lililoteketea fedha taslim ili anunue vifaa binafsi ambavyo havikupatikana kwenye misaada iliyotolewa na wasamaria wema.
Aliongeza kuwa shule hiyo itapelekewa vitabu vya aina zote kwa kiwango cha kila mwanafunzi kuwa na kitabu chake, vitakavyonunuliwa kutokana na Sh. bilioni 27 ambazo zimepatikana kutoka kwenye ‘chenji’ ya ununuzi wa rada.
Pamoja na misaada ya mahitaji binafsi ya wanafunzi inayopelekwa na watu binafsi, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, misaada mingine inayoendelea kupelekwa ni vifaa vitakavyowezesha kujengwa kwa bweni mbadala.
Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (LAPF), umepeleka mabati 92 yenye thamani ya Sh. milioni mbili.
Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment