Pinda Ashukiwa Ndani na Nje ya Bunge

Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa wanafunzi walioshiriki gwaride na halaiki kwenye sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea ni watoto wa wanachama wa chama hicho, imekosolewa na wananchi na wabunge ambao walifikia uamuzi wa kuomba mwongozo.
Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya Februari Mosi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, zikishirikisha makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walivalia sare za CCM na kuimba nyimbo za chama hicho huku wakicheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu kujifunza na kuielewa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo, mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea ushiriki wa watoto hao wapatao 500 kwenye sherehe hizo akisema ni sehemu ya mfumo wa wanachama wa CCM.
“Susan, utafikiri tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima litaulizwa. Ila ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’. Chama hiki kina mfumo wake ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi,” alisema akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia watoto kwenye shughuli zake za siasa wakati ina wanachama wapatao milioni 10 kote nchini.
“Chipukizi hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM, ndiyo maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana. Kwa kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina madhara lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa wanafurahia gwaride na kuvaa sare tu.”
Lyimo hakuridhishwa na jibu hilo la Waziri Pinda, akisema hakutakiwa kutoa majibu ya aina hiyo na kwamba katika mkusanyiko huo, kulikuwa na watoto ambao wazazi wao siyo wanachama wa CCM.
“Lengo la watoto hawa ni kusoma na siyo kufanya siasa. Iweje mfanye mambo kwa double standard (ndumilakuwili)?” alihoji na baadaye Pinda alitaka suala hilo lisiendelee kujadiliwa.
“Naheshimu maelezo ya Susan, lakini kiacheni chama kiendelee na utaratibu wake. Mfumo wake ndiyo huo, ndivyo ulivyo na sidhani kama kuna haja ya kuendelea kubishana katika suala hili,” alisema Pinda ambaye ofisi yake inasimamia elimu ya msingi na sekondari.
Kabla ya nchi kuruhusu tena siasa za vyama vingi mwaka 1992, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walikuwa wakitumiwa kwenye shughuli za chama tawala na za Serikali, lakini imekuwa ni nadra kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu uhuru wa kidemokrasia ulipoanza.
Hata hivyo, ili kufanikisha sherehe hizo za CCM ambazo zilifanyika Jumapili kutokana na siku ya kuzaliwa chama hicho (Februari 5) kuwa katikati ya wiki, maofisa wa elimu ya sekondari wa Manispaa ya Songea walielezwa kuwaandikia barua wakuu wa shule zilizopo karibu na Uwanja wa Majimaji, wakiwataka kuhudhuria pamoja na walimu na wanafunzi ambao waliagizwa kuvaa sare.
Mkosamali aomba mwongoza
Majibu hayo hayakuwaridhisha wabunge wengine na baada ya kipindi cha maswali ya papo kwa papo, Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo.
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment