Ni Simanzi na Vilio Dar, Miili ya Watu Sita Waliofariki Dunia kwa Kuungua Moto

Huzuni, simanzi na majonzi jana vilitawala maeneo ya Kipunguni A na baadaye kwenye Makaburi ya Airwing Ukonga, Ilala wakati miili ya watu sita waliofariki dunia kwa kuungua moto Jumamosi alfajiri ilipozikwa.
Shughuli zilisimama kwa muda katika maeneo hayo kati ya saa saba na nane mchana wakati msafara mkubwa wa waombolezaji ulipokuwa ukielekea makaburini.
Wananchi wengi waliokuwapo katika maeneo ambayo msafara huo ulipita, waliacha kwa muda shughuli zao na kujongea pembeni mwa barabara kushuhudia umati wa watu waliokuwa katika magari, pikipiki, baiskeli na wengine wakitembea kwa miguu wakielekea makaburini katika mazishi ya watu sita; Kapteni mstaafu, David Mpilla, mkewe Celina, mtoto wao Lucas, Shemeji wa Mpilla, Samwel Yegeya na wajukuu wa Mpilla Paulina na Celina Emmanuel.
Katika tukio hilo la Jumamosi, ni mtu mmoja pekee, Emmanuel Mpilla wa familia hiyo alinusurika kwani wakati moto huo ulipoteketeza nyumba yao hakuwapo.
Waombolezaji walianza kuwasili Kipunguni A kuanzia saa tatu asubuhi. Ilipotimu saa tano asubuhi, idadi yao iliongezeka kiasi cha wengine kukosa mahali pa kukaa na kuwafanya waratibu wa mazishi hayo kuwataka waanze kuelekea eneo la makaburi.
Miili ya marehemu iliondolewa nyumbani saa 7.20 mchana kwa gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Wakati inapakiwa kwenye gari hilo, vilio na simanzi vilitawala huku baadhi ya waombolezaji, wengi wao wakiwa kina mama, waligaragara na kulia kwa uchungu.
Hali ilivyokuwa
Kutokana na umati wa waombolezaji, ilipotimu saa 9.20 alasiri, askari wa JWTZ, walifunga barabara inayoelekea eneo la makaburi.
Baada ya miili hiyo kufikishwa makaburini, askari wa JWTZ waliipanga kwenye meza maalumu zilizokuwa zimepambwa kwa maua na picha za marehemu hao zikiwa mbele ya majeneza yao tayari kuanza kwa ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu Msaidizi Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa.
Askofu Nzigirwa, aliwaongoza waombolezaji akiwamo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kuaga miili hiyo ambayo, tofauti na ilivyo kawaida kwa waumini wa Dini ya Kikristo, majeneza yao hayakufunguliwa kutokana na miili ya marehemu kuharibika.
Katika tukio hilo la kuaga, baadhi ya waombolezaji walipoteza fahamu kutokana na uchungu hasa walipopita mbele ya majeneza yaliyokuwa na picha ya watoto Celina na Paulina wakiwa wamekumbatiana huku wakitabasamu enzi za uhali wao.
Miongoni mwa waliopoteza fahamu ni mama wa watoto hao, Mwajuma Issa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment