Hatma ya Makada Sita wai CCM, Waliofungiwa kwa Kukutwa na Hatia ya Kuanza Kampeni za Kuwania Urais Yanukia

kiwa zimebakia siku tano tu kumalizika kwa mwezi huu, hatma ya makada sita wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliofungiwa kwa kukutwa na hatia ya kuanza kampeni za kuwania urais ndani ya chama chao kabla ya wakati wakiwamo mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe bado ni kitendawili.

Hali hiyo inatokana na kuendelea kutanda kwa kimya kizito kutoka kwa mamlaka za ndani ya chama hicho tawala zinazoshughulikia maadili.

Makada wengine waliofungiwa kwa takribani mwaka mmoja sasa kutokana na kosa hilo ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Mbunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.

Jana NIPASHE ilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye ili azungumzie suala hilo, lakini alieleza kwa kifupi tu kwamba, “taarifa kuhusiana na hatua zitakazochukuliwa juu ya suala hilo itatolewa”.

Nape ambaye hakuweka wazi endapo adhabu ya makada hao imefikia ukomo au laa, alisema Kamati Kuu ya CCM ndiyo itatoa maamuzi juu ya matokeo ya utekelezaji wa adhabu kwa makada hao baada ya kupelekewa ripoti kutoka kwa baraza la maadili la chama hicho ambalo ndilo lenye mamlaka ya kuthamini utekelezaji wa adhabu zao.

“Mara kadhaa mmeniuliza swali hili, CCM tunasema hivi, muda ukiisha taarifa mtapewa… kujua kama adhabu yao imeisha au laa. Na kamati itakaa lini, hiyo siyo kazi yenu. Na mimi mwenyewe sijui kwa sababu kazi ya kutathmini adhabu za watu hao haiko katika ofisi yangu. Inafanywa na taasisi nyingine ndani ya chama,” alisema na kuongeza:

“Na kifungo chao kitajulikana baada ya tathmini ya baraza hilo la maadili ambalo ikumbukwe kwamba kazi hiyo ya kutathmini haishi ndani ya siku moja. Inaweza kuwa siku mbili, wiki moja, au miezi kwa sababu kanuni haitubani. Na baada ya kumalizika itapelekwa kwenye Kamati Kuu ambayo ndiyo itatoa maamuzi.”

Nape aliongeza kuwa tathmini ndiyo itaamua juu ya adhabu hizo kulingana na utekelezaji wao katika adhabu walizokuwa wamepewa kama wametekeleza ipasavyo au laa.

Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu ya chama hicho Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni mapema za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, kinyume cha kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

Ilielezwa wakati huo kuwa baada ya kuhojiwa, wote walithibitika kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ndani ya chama hicho.

Adhabu hiyo, pamoja na mambo mengine, ililenga kuwachunguza makada hao pamoja na kutakiwa kujirekebisha.

Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.Februari 13, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete ilifanya kikao chake Kisiwandui, Zanzibar na kuagiza adhabu kali zichukuliwe dhidi ya wale watakaobainika kuwa walikiuka masharti ya adhabu waliyopewa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, ambaye kamati anayoiongoza ndiyo iliyopewa kazi ya kufanya tathmini hiyo, alipotafutwa na gazeti hili jana simu yake iliita mara mbili bila kupokewa na alipopigiwa kwa mara ya tatu, simu yake hiyo ilidhihirika kuwa imezimwa.

KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Wakati CCM ikibaki kimya kueleza hatma ya makada wake sita na pia kutangaza rasmi mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, tayari vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kila kimoja kwa nyakati tofauti kimeshatangaza ratiba na utaratibu wa makada wao kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba na kueleza utaratibu wa kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani ambazo zitaanza kutolewa Mei 3 kwenye ofisi za majimbo yote nchini.

Akitangaza utaratibu huo hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, alisema fomu zitaanza kutolewa Mei 3, hadi Agosti 9 na kwamba, uteuzi wa awali wa wagombea udiwani utafanywa na kamati tendaji ya Kata kati ya Julai Mosi na wakati uteuzi wa wabunge na wawakilishi utafanywa na kamati tendaji ya Jimbo kati ya Agosti 2 na 9 mwaka huu.

Tofauti na kipindi kilichopita, kazi ya uteuzi wa awali wa wagombea ubunge kupitia viti maalumu itafanywa na Baraza la Wanawake la Chama hicho(Bawacha), Agosti 8 mwaka huu na ambapo halmashauri kuu ya chama hicho itathibitisha majina ya wagombea ubunge wote Agosti 10 mwaka huu.

Dk. Slaa alisema Baraza Kuu la chama ndilo litakalopendekeza jina la mgombea urais, mgombea mwenza na mgombea urais Zanzibar.

Alisema uteuzi wa mgombea urais pamoja na ilani ya chama hicho vitathibitishwa Agosti 12 mwaka huu wakati ratiba ya kuchukua fomu na kurejesha itatolewa na Kamati Kuu itakapokutana tena.

Kwa upande wake, Chama cha Wananchi (CUF) mwishoni mwa wiki kilizindua mkakati maalum wa ushindi utakaotekelezwa na kamati za uchaguzi, kuanzia ngazi ya tawi, hadi taifa.Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema miaka yote ya uchaguzi mkuu wamekuwa wakijiandaa katika miezi ya Juni na Julai, lakini mwaka huu wameamua kufanya maandalizi ya aina yake mapema kwa kuwa wanaamini kuwa waklifanya hivyo watatimiza malengo na kupata ushindi .

Alisema ili kufanikisha ushindi huo, kuanzia sasa kazi za ofisini na za utawala wa chama chao hazina nafasi na kwamba, wajumbe wa kamati tendaji za chama wamebadilika na kuwa wajumbe wa kamati za kushughulikia uchaguzi.

Chama cha NCCR- Mageuzi kimetangaza rasmi kuanza kwa zoezi la uchukuaji fomu kwa wanachama wake wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe, alisema fomu hizo zitaanza kutolewa Machi 15 hadi Aprili 30 kwa nafasi za udiwani, ubunge na urais.

Nyambabe, alisema hatua hiyo haiendi kinyume cha misingi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na wagombea watakaopatikana baada ya kupigiwa kura za maoni watakwenda kupambana na wenzao wa vyama vingine kwa ajili ya kumpata mgombea mmoja. Alisema utaratibu wa uchukuaji fomu kwa nafasi ya udiwani utaanza Machi 15 na kumalizika Machi 30.

Alisema kwa upande wa ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar, fomu zitatolewa Machi 20 hadi 21. Kwa nafasi ya urais, fomu zitatolewa Aprili Mosi hadi 30.

Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment