Chama cha demokrasia na maendeleo Chadema mkoani Rukwa kimeshinda kwa kishindo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, uliofanyika jana kwenye kata tano za manispaa ya Sumbawanga, kwa kushinda viti 38 kati ya viti vya mitaa 44 vilivyokuwa vikipiganiwa kwenye uchaguzi huo, huku chama cha mapinduzi kikiambulia viti vitano tu, na kimoja kikisubiri uchaguzi kurudiwa baada ya wagombea kulingana kwa kura.
Akitoa matokeo hayo mjini Sumbawanga msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Bw Hamid Njovu, amesema uchaguzi huo ulikuwa ukifanyika kwa upya kabisa kwenye kata tatu baada ya kuvurugika Desemba 14, mwaka uliopita, na huku kwenye kata mbili za Izia na Sumbawanga asilia ukirudiwa katika mtaa mmojammoja kuchagua mwenyekiti wa mtaa husika, na kwamba uchaguzi huo umefanyika katika mazingira ya amani kabisa.
Akiongea na ITV mwenyekiti wa Chadema wa mkoa wa Rukwa Bw Zeno Nkoswe, amesema ushindi huo wa kishindo ni ishara njema kwa chama chake kufanya vyema kwenye uchaguzi mkuu ujao, kwa kushinda viti vingi kwenye ngazi za udiwani na ubunge, na hata rais ajaye kupatikana mwaka huu kutoka kwenye chama hicho.
Kufanyika kwa uchaguzi huo kunafuatia kuingia kwa dosari kubwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, uliofanyika nchini Desemba 14, mwaka uliopita.
Chanzo: ITV
0 comments:
Post a Comment