ATCL Yazindua Ndege Nyingine Mpya Aina ya CRJ - 100
Shirika hilo ambalo kwa sasa linalotoa huduma zake katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Mtwara na visiwa vya Komoro limejipanga kufanya safari za kila siku kati ya mikoa ya Dar es Salaam na Kigoma huku pia likiwa tayari kufanya safari za Mtwara na visiwa vya Komoro mara sita kwa wiki katika siku za Jumatatu, Alhamisi na Jumamosi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara tu baada ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Meneja wa shirika hilo katika kiwanja hicho, James Mbago alisema ndege hiyo imekodiwa kutoka nchini Afrika Kusini kwa jitihada za Serikali ya Tanzania na sasa ipo tayari kuwahudumia wateja wa shirika hilo.
“Kuja kwa ndege hii kunaongeza idadi ya ndege zetu hadi kufikia mbili na tunashukuru kuona kwamba imepokelewa vizuri na abiria wetu. Ndege yetu nyingine aina ya De-Havilland Dash 8 Q300 kwa sasa inapata matengenezo makubwa kwenye karakana yetu iliyopo hapa hapa uwanja wa ndege,’’ alisema Mbago.
Kwa mujibu wa Mbago kupona kwa ndege hiyo inayofanyiwa matengenezo kiwanjani hapo kutalifanya shirika hilo lianzishe tena safari zake za ndani kwa mikoa ya Mwanza, Tabora, Arusha na Mbeya.
“Muda si mrefu mambo yatakuwa mazuri zaidi…inafurahisha zaidi tunapopata mrejesho mzuri kutoka kwa wateja wetu wanaofurahia huduma za shirika lao mama,’’ aliongeza Mbago. Zaidi, Mbago aliongeza kuwa shirika lake linatarajia ongezeko kubwa la abiria kutokana na ukweli kuwa ndege yao hiyo mpya inauwezo wa kusafiri kwa haraka zaidi ikilinganishwa na ndege nyingine huku safari zake zikiambatana na huduma nzuri inayotolewa kwa wateja wake.
Wakizungumza mara tu baada ya kushuka kwenye ndege hiyo, baadhi ya abiria waliotoka Kigoma walisema licha ya kutumia muda mfupi zaidi lakini pia walifurahia huduma nzuri walizozipata kutoka kwa wahudumu wa ndege hiyo.
“Kwa kweli hii ilikuwa ni moja ya safari zangu za ndege ambayo nimeifurahia sana. ATCL wanahitaji pongezi kwenye hili na zaidi wafikirie kuboresha huduma zaidi ya hapa…sisi abiria tupo tayari kuwaunga mkono kwa sababu ndio wanabeba nembo ya taifa letu,’’ alisema mmoja wa abiria hao aliyejitambulisha kwa majina Gaudence Kashoka.
0 comments:
Post a Comment