Mwenyekiti wa ‘JKT’ Akamatwa kwa Tuhuma za Uchochezi

Mwenyekiti wa Wahitimu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), George Mgoba ambaye alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya kutekwa na kuteswa na watu wasiojulikana, ameruhusiwa jana kisha kukamatwa na Polisi akituhumiwa kwa makosa ya uchochezi na mikusanyiko isiyo halali.


Akizungumza jana, Kamanda wa Kanda Maalumu wa Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema Mgoba ameunganishwa na wenzake wanne na wanahojiwa na polisi kwa makosa ya uchochezi na mikusanyiko isiyo halali.


Mgoba alikuwa amelazwa katika hospitali hiyo akiwa katika ulinzi mkali wa polisi.


Jana, Kova aliwataja wengine waliokamatwa juzi kuwa ni Linus Emmanuel mkazi wa Tabata anayetajwa kama Katibu wa wahitimu hao, Emmanuel Richard mkazi wa Kawe, Jacob Joseph mkazi wa Mabibo na Rizione Ngowi.


Alisema vijana hao walitaka kuandamana kwenda Ikulu kumuona Rais Jakaya Kikwete ili awape majibu ya tatizo la ajira ya kudumu. Kova alisema mara kwa mara vijana hao walikuwa na tabia ya kujikusanya katika kundi lisilopungua watu 300.


Kova alisema Februari 22, saa 11.45 jioni, mtuhumiwa Mgoba akiwa chini ya ulinzi alijaribu kutoroka wodini katika hospitali hiyo alimokuwa amelazwa, ndipo polisi walipombaini na kumkamata kabla hajafanikiwa kuondoka.


Kova alisema madai ya kutekwa kwa mwenyekiti huyo yanaendelea kuchunguzwa ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo na kuwajua wote waliomteka.


Kamanda Kova alisema Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Parali Kiwango anatakiwa kujisalimisha haraka katika ofisi ya mkuu wa upelelezi wa polisi kanda hiyo au kituo chochote cha polisi.


Kova alisema polisi itachukua hatua kali kudhibiti mikusanyiko na mikutano wa aina yeyote kwani haina uhalali wowote kisheria.


Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Eligaesha alithibitisha mgonjwa huyo kuruhusiwa na madaktari jana saa 5.45 asubuhi.


Wakati huo huo, polisi imebaini kuwapo kwa makundi yanayojitokeza kufanya mazoezi ya kareti na Kung Fu katika nyumba za ibada kwa ishara ya kuvunja amani .


“Unajua mwaka huu tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa viongozi hivyo tutafanya msako kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye nyumba za ibadakwa kuwa tumebaini kwamba kuna vikundi vinafanya mazoezi ya kareti na Kung Fu,” alisema Kamanda Kova.

Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment