Polisi Wamwagwa Muhimbili Kukabili Vijana wa JKT

Vijana waliopitia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jana walizua sintofahamu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati walipozuiwa kwa muda wa dakika 25 kuingia kumuona Mwenyekiti wao, George Mgoba, ambaye amelazwa katika wodi ya Mwaisela, akiendelea kupatiwa matibabu baada ya kuteswa, kutupwa kisha kuokotwa na wasamaria wema, maeneo ya Tumbi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani.

Ulinzi uliimarishwa jana na askari wa Jeshi la Polisi walitanda kila kona kuanzia geti ya kuingia hospitali hapo, kuanzia muda wa saa tano asubuhi, kabla ya umati na baadhi ya vijana hao kuruhusiwa kuingia hospitalini saa 6:50 badala ya 6:30 mchana ambao ni muda wa kawaida wa kuona wagonjwa.

Waandishi wa habari pia walikuwa ni miongoni ya watu waliozuiwa kabla ya kuingia hospitalini hapo, licha ya kujitambulisha.

NIPASHE ilipofika wodini na kukutana na muuguzi wa zamu katika wodi hiyo, ambaye hakuwa tayari kujitambulisha jina lake, alisema mgonjwa wake (Mgoba), hataweza kuongea na waandishi kwa kuwa hajisikii vizuri, kwa kuwa anaendelea na matibabu.

“Mimi ni ‘advocate’ wa mgonjwa huyu, nasimamia taaluma yangu na iwapo ninaona mgonjwa anastahili kupumzika ninaweza kulisimamia hilo, mwacheni apumzike kwanza,” alisema muuguzi huyo.

Akiwa amelala kitandani na kuongea kwa tabu, Mgoba alisema yeye yupo tayari kuzungumza iwapo atapewa kibali cha kuzungumza.

“Hapa kuna watu tofauti ambao wapo kazini hivyo wakinipa nafasi ya kuzungumza nipo tayari, ingawaje sijisikii vizuri sana, ” alisema Mgoba.

Pembeni mwa kitanda alicholazwa Mgoba, alionekana mtu ambaye alipoulizwa kuwa ni ndugu yake, alikana na kusema yeye yupo kwa ajili ya kuangalia usalama wa Mgoba.

“Nipo hapa kwa ajili ya kuangalia usalama wake,” alisema mtu huyo.

Alipotafutwa kwa njia ya simu Msemaji wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, hakupokea simu yake licha ya kupigiwa mara kadhaa.

Awali vijana hao wa JKT, walikutana na waandishi wa habari na kutoa kauli ya kutokuwa na imani na Jeshi hilo pia kulaani kitendo cha kuendelea kumshikilia mwenyekiti huyo na kutompatia huduma wala msaada wowote.

Pia, vijana hao walijadili hatma ya afya ya mwenyekiti huyo na hatua watakayoichukua baada ya kukutwa na tukio hilo.

Akizungumza, Makamu Mwenyekiti wa vijana hao, Parali Kiwango, alisema hawana imani na polisi, kutokana na kitendo alichofanyiwa mwenyekiti wao na kuendelea kumshikilia.

Alisema kutokana na kutekwa mwenyekiti wao matembezi waliyopanga kufanya jana hadi Ikulu wameyasitisha, ili kuangali hali ya afya ya kiongozi wao inavyoendelea.

Alipotafutwa kwa njia ya simu Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso, ili kuzungumza sababu ya kuendelea kumshikilia Mgoba, simu yake iliita bila ya kupokelewa.

Tukio la kuokotwa Mgoba na wasamaria wema, huku akiwa ameteswa na kutupwa maeneo ya Tumbi wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, na kupelekwa kituo cha Polisi cha Kibaha na baadae kupelekwa hospitali ya Tumbi lilitokea mwanzoni mwa wiki iliyopita.

Mgoba, alidai kuwa alitekwa na kuteswa na watu wasiofahamika huku wakimtaka kuwataja wanaowashinikiza kuandamana kwenda Ikulu.

Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment