Yanga Kulipa Deni la Ngassa

Hatimaye klabu ya Yanga imekubali kulipa deni analodaiwa mchezaji wao, Mrisho Ngassa na klabu ya Simba, kwa masharti iwapo tu atakubaliana nao katika baadhi ya mambo likiwamo la mkataba au jambo lingine lolote.
Aidha, Ngassa ameahidi kucheza kwa kiwango katika michuano ya ligi na ya kimataifa na kuwa mchezaji bora iwapo tu uongozi wa klabu hiyo utamsaidia kulipa deni hilo kama ulivyoahidi.
Katika msimu wa 2013/2014, Ngassa alijiunga na Yanga akitokea Simba alikokuwa akicheza kwa mkopo akiwa ni mali ya Azam FC, katika uhamisho ambao Shirikisho la Soka Tanzania (TF), lilimuamuru awalipe Simba Sh milioni 30 walizomsajili kutoka Azam FC na Sh milioni 15 kama fidia baada ya kugundulika alisajiliwa timu mbili.
Kutokana na Yanga kuonesha nia ya kutaka huduma ya winga huyo, klabu hiyo chini ya Mwenyekiti Yussuf Manji uliamua kumlipia deni hilo kwa makubaliano atakuwa akikatwa Sh 500,000 katika kila mshahara wake wa mwezi.
Hivi karibuni, Ngassa alisema alishindwa kucheza kwa kiwango cha juu kutokana na kukatwa mshahara wake wote kwa ajili ya deni hilo katika benki kinyume cha makubaliano yake na Yanga aliyodai walimuahidi kumsaidia kulilipa.
Akitolea ufafanuzi suala hilo jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro alisema wamepata ombi la Ngassa kuwa anaomba kulipiwa deni hilo na wamelipokea na kuahidi kumsaidia ndani ya wiki moja, lakini awe tayari kutimiza masharti atakayopewa bila kuyataja ni yapi.
“Ngassa ni mchezaji wetu tutamsaidia kulipa deni kwa sababu bado tunamhitaji na yeye anatuhitaji,” alisema Murro na kuongeza kuwa mchezaji huyo alikuwa akikatwa mshahara wote kwa sababu alikiuka utaratibu waliowekeana na benki hiyo ambapo awali walikubaliana mshahara wake uwe unapitia benki.
Alisema wakati Ngassa anakopa fedha, Yanga ilisimama kama mdhamini tu na wakakubaliana mshahara wake uwe unapita benkiili awe anakatwa Sh 500,000, lakini baadaye akawa hafanyi hivyo kwani alikuwa akienda kuchukua mshahara wake chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu Beno Njovu bila kupitisha huko kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Alisema kitendo hicho kilisababisha benki hiyo kulalamika kwa barua kwa kukiuka makubaliano ya awali na ndipo uongozi mpya chini ya Katibu Mkuu Dk Jonas Tiboroha, ulipoamua kupitisha mshahara huo benki ili akatwe kama walivyokubaliana awali.
“Benki walikuwa na hasira kwa kutopata pesa zao kwa kipindi cha mwaka mmoja na ndio maana walikuwa wakikata kwa hasira mshahara wote wa Ngassa, sisi tulipoingia tukaona tufuate sheria kwani deni lile halikuwa la kiuongozi,” alifafanua Murro.
Alisema wao kama klabu hawana matatizo ya kimaslahi kwani kazi yao kubwa ni kutimiza majukumu ya mkataba na kwamba wanatambua kuwa Ngassa ni mchezaji wao, ana uhuru wa kuzungumza mambo yake, lakini sio klabu.
Kuhusu kumuongezea mkataba, alisema watafanya mazungumzo na mchezaji huyo kuona kama atasaini mkataba mpya kwa vile bado wanahitaji huduma yake, lakini ikiwa hatakubali na atataka kuondoka, itakuwa sawa.
Hata hivyo, Ngassa ambaye alikuwepo kutolea ufafanuzi madai yake, alisema anapenda kuendelea kuichezea Yanga ili kujenga heshima yake na kama basi, ataondoka sio kucheza katika timu za ndani labda nje ya Tanzania.
Pia, kuhusu kitendo chake cha kuwaomba msamaha mashabiki wa Simba na Azam FC kwa kujutia kujiunga na Yanga, alisema sio kwamba ameisaliti timu yake kwani hana mpango wa kurudi huko wakati huo akiwaomba msamaha mashabiki wa Yanga kwa kitendo hicho.


Kuhusu kujutia kutokwenda El Merreikh, alisema ni kweli alikataa kujiunga na timu hiyo kwa sababu ya mapenzi yake makubwa ilikuwa ni kuichezea Yanga na hata sasa anapenda kuendelea kuichezea timu yake hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment