Jumuia na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimesema kuwa zitahamasisha Wanajumuia wake kususia kupiga kura za maoni ya Katiba mpya hadi pale watakapopata uhakika wa kupata Mahakama ya Kadhi yenye meno.
Kauli ya Jumuia na Taasisi za Kiislamu zipatazo 11 imetolewa jana Jijini Dar es Salaam, na kusomwa na Naibu Katibu wa Jumuia ya Shura ya Maimamu Wilaya ya Kinondoni, kwa madai kuwa kinachoendelea katika mchakato wa kupatikana Mahakama hiyo ni hadaa za Serikali zinazofanyika miaka yote hasa kinapofika kipindi cha kupiga kura kwa lengo la kupata kura za waumini hao.
Akizungumza kwa niaba ya baadhi ya Jumuia 11 za Kiislamu zilizosajiliwa na kutambulika Kisheria ambazo ni Baraza Kuu, Tampro, Basuta, Jasuta, IPC, Haiyat Ulamaa na Shura ya Maimamu Tanzania, Shekhe Katiba alisema kuwa watawahamasisha Waislamu wanaounda Jumuia hizo kutopiga kura ya maoni wala kushiriki kwa namna yoyote ile katika mchakato wa kupatikana Katiba mpya kwa sababu haiitambui Mahakama yao yenye haki ya kuamua pindi kunapokuwa na tatizo upande wao.
Alisema kuna baadhi ya Taasisi za kidini, magazeti, kwenye mchakato wa kutoa maoni juu ya Muswada unaohusu Mahakama ya Kadhi, umepotoshwa kwa kuituhumu Mahakama hiyo kuwa italeta vurugu ikiwamo kuhukumu kwa kukata watu mikono, kuhukumu wasiokuwa Waislamu na kuwabagua wasiokuwa Waislamu , Taasisi hizo 11 ni Wahabi hivyo maoni yao hayawakilishi waislamu wengi, kuwa umepotoshwa makusudi ukiwa na lengo la hadaa kwa Waislamu.
“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na Serikali wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na Taasisi hizo 11, ambayo kama yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama ya Kadhi inakidhi matakwa ya Sheria za Kiislamu na wajibu wake kama mamlaka ya kutoa na kutenda haki, ”alisema Shekhe Katimba.
Nae Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jumuia hizo Mzee Mwinyikai, alisema kuwa katika Muswada unaoendelea kujadiliwa kwa madai ya kupatikana Mahakama ya Kadhi Mufti amepewa jukumu la kuteua makadhi na kutengeneza kanuni za Uendeshaji wa Mahakama ya Kadhi ili hali Mufti sio chombo cha kisheria.
Alisema hakuna sheria inayounda ofisi ya Mufti isipokuwa uwepo wake unategemea katiba ya BAKWATA, hivyo Mahakama ya Kadhi uwepo wake utategemea uwepo wa Katiba ya Bakwata inayounda ofisi ya Mufti. Kukiwa na mgogoro wa kikatiba Bakwata athari yake itaikumba na Mahakama ya Kadhi. Hakuna duniani mtu ambaye ofisi yake haiundwi na sheria kisha sheria ikampa mtu huyo madaraka ya kuunda chombo chenye mamlaka ya kisheria kama Mahakama.
“Serikali inalijua hili lakini imefanya makusudi kwa kusukumwa na nia yake ya kutopenda kuona Waislamu wanakuwa na Mahakama ya Kadhi ya ukweli na yenye meno inayoweza kuamua kwa haki migogoro na matatizo yake, madai ya kwamba Bakwata ni baba na Taasisi nyingine ni watoto hayana ukweli na ndiyo maana hata Kamati ya Bunge haikutoa mwaliko kwa Bakwata pekee , ”alisema Mwinyikai.
Katika taarifa ya Jumuia hizo iliyosainiwa na Shekhe Abdallah Bawazir ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Hay Atul-Ulamaa, ilisema kuwa muswada unaojadiliwa ili kupatikana Mahakama ya Kadhi ni kiini macho kwa sababu una baadhi ya mambo yatakayoleta mgogoro kati ya waislamu na waislamu ikiwamo kutoa hiyari kwa mtu kufungua shauri katika Mahakama ya Kadhi au ya Serikali
jambo hili limekusudiwa kuifanya Mahakama ya Kadhi iwe butu na kutoa mwanya wa kutokea mgongano baina ya Mahakama ya Kadhi na mahakama za kawaida ikiwa kila upande katika mgogoro utaamua kufungua shauri katika mahakama tofauti.
Alifafanua Muswada huo unaitaka Mahakama ya Kadhi ijiendeshe yenyewe bila kupata fedha kutoka Serikalini kitu ambacho hakiwezekani ,jambo ambalo halijawahi kutokea sehemu yeyote duniani chombo kama mahakama kujiendesha chenyewe.
“Zipo mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo zinaendeshwa kwa pesa za serikali ambazo ni kodi za Watanzania wote. Mfano ni kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi, Biashara kwa nini mahakama itakayotafsiri sheria za Kiislamu iwe nongwa?, ”ilisema na kuhoji taarifa hiyo.Kwa upande wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shura ya Maimamu Wilaya ya Kinondoni Chambo Ally alisema kuwa , Serikali inatakiwa kupeleka muswada Bungeni wa kujadili kuwapo Mahakama ya Kadhi badala ya kurekebisha vifungu vya Sheria kama wanavyojaribu kufanya sasa.
Akijibu tuhuma zilizoelekezwa kwa Baraza la Waislamu Tanzania ‘BAKWATA’ Mufti Mkuu wa Tanzania, Shehe Issa Shaaban Simba alisema kuwa hana cha kubishana wala kuchangia katika hilo kwa sababu Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba Sheria na Utawala iliziita Taasisi zote za Kiislamu ikiwamo na hizo 11 na kila moja ikatoa maoni yake ya nini kifanyike ili kuboresha muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Alisema wao kama Bakwata waliungana na Serikali na kukubaliana nini kitoke, kibaki, kiboreshwe, hivyo na hizo taasisi nyingine ule ndiyo ulikuwa wakati wao wa kukubali, kukataa, kutoa mapendekezo, kujadili, kama hawakufanya hivyo hakuna haja ya kupigizana kelele au kubishana.
“Sioni haja ya kubishana, kila Taasisi ilitoa maoni yake mbele ya Kamati, bado haijakutana na kutoa maamuzi, haijapeleka chochote kikajadiliwe Bungeni, nafikiri kuna haja ya kusubiri kusikia watasema nini, ”alisema Mufti Simba.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Ummy Mwalimu, alisema kuwa hawezi kulizungumzia hilo kwa sasa hadi itakapotolewa taarifa rasmi.
“Siwezi kulizungumzia hilo kwa sasa, subiri taarifa rasmi kuhusiana na Mahakama ya Kadhi, usiwe na wasi itatolewa wakati wa kufanya hivyo ukifika, ”alisema Mwalimu.
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment