Vunjo Yageuka Uwanja wa Sinema ya Mbatia na Mrema...

JIMBO la Vunjo mkoani Kilimanjaro, limegeuka ‘steji’ ya sinema ya kuwania ubunge kati ya Mbunge wa sasa, Mwenyekiti wa Chama cha TLP, Agustino Mrema na mpinzani wake katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Siku ya Alhamisi jioni wiki hii, ilikuwa zamu ya Mrema kuonesha uwezo wake katika kutetea jimbo hilo hata kabla ya Uchaguzi Mkuu, pale alipoomba nafasi ya kuwasilisha maelezo binafsi kwa kuzingatia Kanuni ya 50 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ambayo maelezo yote yalikuwa dhidi ya Mbatia.
Ijumaa jioni, ikawa zamu ya Mbatia na yeye naye akatumia kanuni hiyo hiyo, kuwasilisha maelezo binafsi ambayo yote, yalikuwa majibu kwa Mrema. Huku wote wakiweka wazi kuwa ni wagombea wa jimbo hilo, kila mmoja alitumia namna anayojua kujenga hoja kuonesha udhaifu wa mwenzake, wakitumia masuala yenye mguso kwa jamii ya ugonjwa, kifo na maadili kujipigia debe.
*Ugonjwa
Mrema katika kujenga hoja yake, alianza kuweka hadharani hali yake ya afya kwa kutaja magonjwa yaliyokuwa yakimsumbua na kusisitiza kwamba sasa yuko vizuri kiafya. Alimtuhumu Mbatia kwamba anafanya kampeni mapema kwa kuwaambia wananchi kwamba Mrema ni mgonjwa wa Ukimwi.
“Napenda kulihakikishia Bunge lako, wananchi wa Jimbo la Vunjo na Mheshimiwa Mbatia ajue kuwa, afya yangu ni njema na sina Ukimwi; Nilikuwa na saratani ya mapafu na hivi sasa nimepona,” alisema Mrema.
Mbunge huyo ambaye aliwasilisha ripoti ya madaktari ya vipimo vyote, alivyofanyiwa hospitalini kuonesha kwamba hana Ukimwi na saratani, alisema alianza kuugua ugonjwa wa kisukari tangu mwaka 1982.
Alisema mwaka juzi alirudi India kwa ajili ya vipimo na kugundulika ana saratani ya mapafu, ambapo madaktari walimpa matibabu aliyotumia kwa mwaka mmoja. “Mheshimiwa Spika napenda kukutaarifu na kulitaarifu Bunge lako kwamba, ripoti ya madaktari juu ya afya yangu imetoka na ninayo hapa,” alisema na kusoma maelezo yaliyo kwenye nakala ya vipimo alivyoambatanisha na taarifa yake ikisema hakuwa na tatizo.
Aidha, alisema akiwa nchini humo (India) Desemba 18 mwaka jana, alifanyiwa kipimo cha Ukimwi na kugundulika hana virusi vya ugonjwa huo. Kwa mujibu wa Mrema, wakati akiwa India, Mbatia na wapambe walikuwa wakihamasisha wananchi wa jimboni kwake asipewe ubunge kwa kigezo cha ugonjwa.
Akijibu hoja hiyo kwa kutumia ugonjwa, Mbatia alisema hajawahi kumnyanyapaa (akijua unyanyapaa ni tatizo la kijamii) Mrema wala mtu yeyote aliyathirika na maradhi ya aina yoyote ikiwamo Ukimwi. “Maelezo yote aliyotoa (Mrema) siyo sahihi na sijawahi na sitawahi kutamka maneno hayo ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania…masuala ya ugonjwa wa aina yoyote ni masuala binafsi na hivyo si busara kwa mtu ambaye hana idhini ya mhusika kuyazungumzia,” alisema Mbatia.
*Kifo
Katika kujenga hoja zao, wote walitumia dhana ya kifo ambayo ina mvuto wake katika jamii, kwa kuwa ni kitu kinachohuzunisha na kuogopewa, na hivyo kinaweza kushawishi kwa namna yoyote.
Mrema katika tuhuma zake kwa Mbatia, alisema aliwaambia watu kuwa ana Ukimwi na kwamba wakati wowote anakufa. “Mbatia anatumia maneno haya ya uongo kama mtaji wa kisiasa, kwani anajua ikiwa nitakuwa hai, hawezi kupata ubunge wa Jimbo la Vunjo ndiyo maana anawaeleza kuwa nitakufa muda wowote kwa kuwa nina Ukimwi,” alisema Mrema.
Mbatia mbali na kukanusha, katika suala la kifo alilizungumzia kwa namna yake. Kwanza alisema kauli hiyo ya Mrema imeigusa familia yake na kuipa uchungu, ikizingatiwa kwamba anaye mtoto ambaye kutokana na athari za ugonjwa wa Ukimwi, alipoteza wazazi wake wote, jambo lililosababisha achukue hatua za kumuasili apate upendo na malezi.
*Kugombea
Mrema katika suala la kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, alikuwa wazi; “Nitaendelea kufanya kazi zangu za ubunge katika Jimbo la Vunjo na nataka niwahakikishie kuwa nitagombea tena ubunge, ili kuhakikisha namaliza kazi zangu nilizokwisha kuzianza kuzitekeleza.”
Mbatia yeye katika kutangaza nia, hakwenda moja kwa moja, akasema si sahihi baadhi ya viongozi walioko madarakani, kudai kwamba wana hati miliki ya maeneo wanayoyaongoza. “Bali wenye hati miliki ni Watanzania wenyewe.” Akasisitiza kuwa mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu, Watanzania wachague viongozi wenye uwezo, wacha Mungu, wakweli na wenye kuchukia propaganda, ubaguzi, chuki, ubinafsi na ufisadi.
*Siasa na maadili
Katika kuonesha kuwa kiini cha maelezo binafsi ni siasa za kuwania jimbo hilo kabla ya muda rasmi wa kuanza kampeni, Mrema alihoji; “Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, kipindi au muda wa kampeni bado haujafika na Bunge halijavunjwa, sasa inatokeaje Mheshimiwa Mbatia aanze kampeni na tena za kunidhalilisha wakati anajua mimi ndiye Mbunge halali wa Jimbo la Vunjo?”
Mbatia yeye katika kujibu hoja hiyo alisema; “mimi ni muumini wa siasa safi na sina utaalamu wa propaganda (akijua kuwa Mrema kasomea propaganda nchini Yugoslavia) kama zilizozungumzwa jana (juzi) na Mrema.
Kwa kiasi fulani naamini kuzeeka siyo kukua, naamini kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa.” ‘Akajifagilia’; “Mimi sina uadui na mtu yeyote akiwemo Mrema, ninamheshimu kama mzee wangu hivyo kimaadili nisingeweza kumkosea nidhamu kwa kiwango hicho alichoeleza hapa bungeni. Nimezaliwa na kukuzwa kwenye familia ya wacha Mungu.”
*Ukaribu na Rais, Spika
Mrema akijua kuwa Mbatia ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, na huenda hiyo ikawa moja ya kete yake ya kugombea ubunge, aliamua kueleza ukaribu wake na Rais Jakaya Kikwete katika ugonjwa wake.
Mrema alisema alianza kuugua ugonjwa wa kisukari tangu mwaka 1982 na kwamba mwaka 2009, Rais Kikwete ndiye alimpeleka India kwa matibabu.
Alimtaja pia Spika wa Bunge, Anne Makinda, kuwa alimpeleka tena India Desemba 17 mwaka jana kwa ajili ya uchunguzi kujua hali yake kiafya inavyoendelea kwa ujumla.

CHANZO: HABARI LEO
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment