Wakati Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar akisubiri Sheria ya Kura ya Maoni iwasilishwe kwenye chombo hicho Machi kwa ajili ya kuridhiwa, CUF imesema haipo tayari kuhalalisha sheria yoyote itakayotumika kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Kauli hiyo imekuja baada ya wanaharakati na wanasheria kulalamika kuwa Sheria ya Kura ya Maoni imeanza kutumika kinyume na Katiba ya Zanzibar kwa kuwa haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi tangu ilipotungwa na kupitishwa na Bunge la Muungano mwaka 2013.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho alikiri juzi kuwa sheria hiyo bado haijaridhiwa kwenye chombo hicho cha kutunga sheria kama kifungu cha 132.1 cha Katiba ya Zanzibar kinavyotaka, lakini akaongeza kuwa anatarajia itapitishwa mwezi Machi na mchakato wa Kura ya Maoni kuendelea kama ilivyopangwa.
Jana mkurugenzi wa uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Salim Bimani Abdallah aliiambia Mwananchi kuwa wawakilishi kutoka chama chake hawapo tayari kuhalalisha sheria yoyote itakayotumika kupitisha Katiba Inayopendekezwa kwa sababu haikutokana na maoni ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Alisema kwamba CUF, chama kikuu cha upinzani Zanzibar, itaendelea kutetea na kulinda msimamo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wa kususia mchakato mzima wa Kura ya Maoni hadi Serikali itakapokubali kuandika Katiba inayozingatia matakwa ya wananchi wake.
Aidha alisema kwamba Spika na viongozi wenye dhamana wasipate shida ya kupeleka sheria hiyo kwenye Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuridhiwa wakati Wajumbe wa CUF wakiwa tayari wamejipanga kugoma kuridhia Sheria hiyo kwa maslahi ya Zanzibar na wananchi wake.
“Hatupo tayari kupitisha sheria ya kuja kuhalalisha katiba mbovu ambayo haikutokana na maoni ya wananchi wake,” alisema Bimani.
Hatua hiyo ya CUF inawekwa kikwazo kingine katika hatua za mwisho za ukamilishwaji wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba ambao umekumbwa na vizingiti vingi. Tayari Bunge la Muungano limeshataka maelezo kuhusu mwenendo wa mchakato huo baada ya kuwapo kwa taarifa za uwezekano wa kukwama kutokana na sababu kadhaa, zikiwamo za vifaa vitakavyotumika kuandikisha wapigakura na fedha.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Spika Kificho alikiri kuwa Sheria ya Kura ya Maoni haiwezi kuanza kutumika kabla ya kuwasilishwa kwenye Baraza la Wawakilishi kwa mujibu wa kifungu cha 132(1)(2) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kinachotaka sheria inayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo haihusu Muungano na inatakiwa itumike Zanzibar, lazima ipitishwe na Baraza la Wawakilishi.
Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi (CCM), Awadhi Salmin Awadhi alisema kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Sheria ya Kura ya Maoni inahitaji kuwasilishwa Barazani kabla ya kuanza kutumika, lakini akasema kuwa wawakilishi kutoka CUF hawana ubavu wa kuzuia sheria hiyo kuridhiwa kutokana na utaratibu wake.
Alisema kwamba kwa mujibu wa Katiba, sheria hiyo inahitaji kuwasilishwa mezani baada ya kupitishwa na Bunge na wala haihitaji kujadiliwa na kupitishwa na kuwataka viongozi dhamana kupeleka sheria hiyo kabla ya kupigwa kwa Kura ya Maoni.
“Kama Waziri wa Sheria na Katiba hatagoma kuwasilisha sheria hiyo, atalazimika kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kushindwa kutetea shughuli za serikali kinyume na kiapo chake,” alisema Salmin Awadhi.
Credit: Mwananchi
Credit: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment