Rais wa Ujerumani Aacha Gumzo, Aenda Zanzibar kwa Kutumia Boti

Ziara ya rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck imeacha mjadala mzito kisiwani hapa kutokana na kitendo chake cha kutumia usafiri wa boti kuja Unguja na kutembea kwa miguu hadi Hoteli ya Serena ya Zanzibar.
Rais huyo, akiwa na mwenyeji wake, Dk Ali Mohamed Shein, alikuwa akitembea mitaa ya Mji Mkongwe, huku akisalimiana na wananchi waliokuwa pembeni ya barabara kushuhudia ujio wake.
Tofauti na viongozi wengi wa juu, Rais Gauck alisafiri kutoka Dar es Salaam kwa kutumia boti ya Kilimanjaro 4 na kuwasili saa 5:30 asubuhi. Alipokewa na mwenyeji wake, Shein pamoja na wananchi wakiwamo na wanafunzi.
Baada ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum la heshima, kiongozi huyo alianza kutembea huku akisalimia wananchi na wengine kudiriki kuwashika mikono.
Akiwa katika ulinzi wa kawaida, alipita mitaa ya Malindi, Mizigani na Forodhani ambako wananchi walikuwa wamejipanga pembeni huku wakicheza ngoma ya Beni. Siku hiyo maduka yalifungwa kutokana na sababu za kiusalama.
Mbali na hatua hiyo Wafanyabiashara wa Forodhani walitakiwa kufunga biashara zao siku moja kabla ya mgeni kuwasili na mitaa hiyo kufanyiwa usafi mkubwa, hasa kwenye barabara zote alizopita pamoja na ufukwe wa Forodhani.
Wachukuzi wa mizigo kwenye Bandari ya Malindi walipata pigo baada ya kuzuiwa kutekeleza majukumu hadi kiongozi huyo alipoondoka kuelekea Hoteli ya Serena.
Mfanyabiashara Ahmed Mwinyi  Muhamad (29) Mkazi wa Bububu alisema kitendo cha Rais Gauck kutumia usafiri wa gharama nafuu, kimewavua nguo viongozi wa Afrika ambao hutumia usafiri ghali bila ya kuwapo sababu za msingi.
Alisema kitendo cha kiongozi huyo kusalimiana na wananchi kwa kuwapa mikono kinaonyesha upendo na kuwa karibu na watu bila ya kujali wadhifa wake na kuwataka viongozi wengine kufuata nyayo zake.
“Tatizo kubwa viongozi wetu wanawahitaji wananchi wakati wa uchaguzi, wakipata huwezi kuwasogelea wala kuwaona na ukifanya mchezo utachezea virungu,” alisema Muhamad.
Katibu mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu alisema Rais Gauck amewatukana kisayansi viongozi wa Afrika kutokana na kusafiri na wasaidizi wake kwa boti.
Alisema viongozi wa Afrika wakipata madaraka, hutumia magari ambayo hutembea kwa mwendo wa kasi na vioo vya giza na wakati mwingine kuhatarisha hata usalama kwa wapita njia
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment