TCRA Yawaangukia Viongozi wa Dini Matumizi ya Mawasiliano

Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuwaelimisha waumini namna ya matumizi salama ya vyombo vya mawasiliano ili kuondokana na matumizi mabaya ya vyombo hivyo.

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma, wakati wa kutoa elimu ya mawasiliano kwa viongozi mbalimbali wa dini jijini Dar es Salaam juzi.

Viongozi hao wa dini ni wa kutoka Baraza la Amani linalojumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo.

Aidha, Profesa Nkoma alisema miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu imeongezeka kwa kasi na kuzidi matumizi ya benki.

Alisema sababu ya kutoa elimu kwa viongozi hao wa dini ni kuwaeleza namna ambavyo mamlaka hiyo inavyofanya kazi na namna ya kutoa elimu kwenye nyumba za ibada ili kudhibiti matumizi mabaya ya mawasiliano.

“Tumeona ni vyema tukatoa elimu ya mawasiliano kwa viongozi wa dini ili kushirikiana nao katika kupunguza matumizi mabaya ya mawasiliano ikiwamo ya simu za mikononi na mitandao ambayo imekuwa ikiwaathiri Watanzania wengi,” alisema.

Kuhusu matumizi ya simu za mkononi na mitandao, alisema yamekua kwa kasi na kwamba hadi sasa kadi milioni 30 za simu zinamilikiwa na watu mbalimbali nchini.

Profesa Nkoma alisema kiwango hicho kinaongezeka kila mwaka na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2020, idadi hiyo itafikia milioni 50.

Kuhusu uzimaji wa mfumo wa analojia, alisema hadi mwezi ujao, itakuwa imezimwa nchi nzima na Tanzania inaongoza kwa kuhamia kwenye mfumo wa digitali ukilinganisha na nchi zote za Afrika.

Chanzo: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment