Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, kimeonya kuwa kitawachukulia hatua watu watakaomhujumu Mbunge wa jimbo hilo, Deo Filikunjombe (CCM), katika utekelezaji wa mradi wa umeme unaofadhiliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Chadema kata ya Kilindo wilayani Ludewa, Edgar Kyulla, wakati wa uzinduzi wa mradi huo utakaogharimu Sh. milioni 200.
Mradi huo wa umeme unatekelezwa na kampuni za Renewable Energy Technology Development (Retdco) na Kilondo Investment.
Mradi huo unaojengwa kwenye maporomoko ya mto Kilondo, utazalisha umeme wa kilowati 50 kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa kijiji cha Kilondo na baadaye Nsele.
Kyulla alisema wakazi wa Ludewa wanatambua kwamba mradi huo utakaolifanya eneo hilo kupata umeme kwa mara ya kwanza, umefanikiwa kupitia jitihada binafsi za Mbunge Filikunjombe (pichani).
Chadema ambacho awali hakikuwa na nguvu kubwa Ludewa, kimefanikiwa kushinda viti kadhaa vya wenyeviti wa vijiji na vitongoji na hivyo kujiongezea nguvu zake jimboni humu.
"Mnayajua makeke yangu, ninawaonya wote watakaojaribu kumhujumu Filikunjombe katika utekelezaji wa mradi huu, ikibidi tutawachapa viboko kwa maana maendeleo haya hayana uhusiano wowote na itikadi bali ni kwa manufaa ya kizazi chetu," alisema.
Naye Filikunjombe alisema Chadema ni chama cha Watanzania wanaopaswa kuheshimiwa, lakini suala la kushika dola na kuchagiza maendeleo ya nchi, linabaki kuwa la CCM.
"Tuwaheshimu, tuwapende hawa wenzetu (Chadema) lakini tuhakikishe kwamba CCM inaendelea kushika dola na kuiletea nchi maendeleo," alisema.
Hata hivyo, alisema jukumu hilo linapaswa kufanywa na wote wenye dhamana ya kuutumikia umma katika maeneo yao.
Filikunjombe aliwataka wakazi wa kata hiyo kushiriki kikamilifu katika kuchangia nguvu za umma kuwasaidia wataalam wanaoujenga mradi huo.
Kiongozi wa Kilondo Investment, Eric Mwambeleko, alisema mradi huo uliwasilishwa Rea ukakataliwa kutokana na vigezo kadhaa, ndipo Filikunjombe alipoingilia kati na kufanikisha kupatikana kwa fedha za mradi huo. Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Retdco, Wakati Ramadhan, alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita.
Credit: Chadema blog
0 comments:
Post a Comment