Mbunge Kagasheki Amtaja Waziri Mkuu Mizengo Pinda Kuwa Ndiye Aliyekuza Mgogoro wa Bukoba

Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Khamis Kagasheki amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ndiye aliyekuza mgogoro wa Bukoba uliosababisha madiwani wa halmashauri kushindwa kufanya vikao, akidai kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali ameshindwa kuchukua hatua. Pinda hakuweza kupatikana, lakini msemaji wake alisema Waziri Mkuu ameshalishughulikia suala hilo kwa kiasi kikubwa.
Tuhuma hizo za Kagasheki ni za nadra kwa mbunge huyo wa chama hicho tawala kuelekeza kwa mtendaji mkuu wa Serikali na mmoja wa wajumbe wa vikao vya juu vya CCM.
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa tuhumu hizo wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili wiki iliyopita, akisisitiza kuwa ni makosa kuutazama mgogoro huo kuwa ni kati ya yake na meya na akataka ijulikane kuwa kinachoendelea Bukoba ni suala la wizi.
Mgogoro huo wa kisiasa, ambao umedumu kwa takriban miaka miwili na unaotishia kugawanyika kwa CCM, umekolezwa na kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zimezuia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na umekuwa ukihusishwa na vita vya ubunge baina ya Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupata nafasi ya kuzungumzia suala hili. Hakuna unafiki hapa, hili nitalisimamia mahali popote na nitalisema mahali popote kuwa Pinda, ndiye tatizo katika mgogoro huu ulioinyima Bukoba maendeleo,” alisema Kagasheki.
“Lakini hiyo hainizuii kusema kuwa Tamisemi ndiyo tatizo, ingawa waziri wake ni Hawa Ghasia. Pinda ndiye msimamizi na bungeni alisema Amani siyo meya tena, lakini hakuna lililofanyika hadi leo na wananchi wanakosa maendeleo,” aliongeza akirejea kauli ya Pinda bungeni kuwa meya huyo alijiuzulu halafu siku chache baadaye Amani akaibuka na kukanusha habari za kuachia kiti cha umeya.
Alisema kuwa awali wakati mgogoro huo unafukuta, uongozi wa juu CCM uliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) kwenda Bukoba, naye akaenda kufanya utafiti, akamaliza na akatoa kila kitu.
Kagasheki alieleza: “ Nilikwenda katika kikao cha CCM, Pinda yupo ndani ya chama, kikaagiza madai hayo yafanyiwe kazi, lakini mpaka leo Takukuru hawajafanya chochote. Ndiyo maana nasema, Pinda akija kuomba kura (za urais) Bukoba, pale mjini, hali ni ngumu kwelikweli, atapata shida sana.
“Huu siyo mgogoro, ni wizi wa fedha na ripoti ya CAG ipo wazi lakini wahusika walio chini ya Waziri Mkuu hawataki kuifanyia kazi…Jambo hili lisipofanyiwa kazi, lazima itakuwa ajenda katika Uchaguzi Mkuu.”
Mbunge huyo wa Bukoba Mjini alisisitiza akisema: “Unajua kuna vitu vinaumiza, maana vile siyo vitu vyangu ni taarifa ya CAG na kwa kweli huyu CAG aliyeondoka ungekuwa unamuuliza ukweli, angekwambia amegundua mambo mengi ndani ya Serikali ambavyo hayafanyiwi kazi. Wizi usio na kifani, upotevu wa fedha na jambo zuri ni kuwa ile kazi aliyokuwa akafanya CAG ipo kikatiba.”
Alisema kuwa CCM ilitoa maelekezo na kupitia Serikali ikayapeleka Tamisemi, lakini hadi sasa hakuna pendekezo hata moja la CCM wala CAG lililofanyiwa kazi, lakini Waziri Mkuu yupo kimya.
“Tunapozungumzia Tamisemi, tunazungumzia Waziri Mkuu, bahati nzuri yeye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Uamuzi wa Kamati Kuu, Pinda hakufanya hata moja na hapo ndipo mgogoro ukapamba moto,” alidai.Alitoa mfano wa jinsi wananchi wa Bukoba wanavyokosa maendeleo kutokana na mgogoro huo akisema kuwa kwa msaada wa Rais Jakaya Kikwete, Benki ya Dunia ilitoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa maji katika jimbo hilo, lakini mradi haujatekeleza kwa sababu hakuna vikao vya baraza la madiwani vinavyofanyika huku Tamisemi ikiwa kimya.
“Yapo mengi, lakini sasa tupo katika mazungumzo na Tamisemi kuomba watusaidie kupata fedha za huo mradi wa maji kabla ya mwaka wa fedha haujaisha na fedha kurudishwa kwa wafadhili,” alisema.
Akizungumzia tuhuma hizo, Irene Bwire, msemaji wa Pinda, alishangaa kwamba vyombo vya habari vinaandika habari hizo kwa upendeleo na kuongeza kuwa Waziri Mkuu alishashughulikia suala hilo kwa kiasi kikubwa.
Alisema Pinda alidiriki hata kuchukua wahariri wa habari kwenda nao Bukoba kwa ajili ya kushuhudia jitihada zake za kutatua mgogoro huo na kwamba mengi ameshayafanya. Bwire alitaka baadaye apelekewa maswali, lakini hakupatikana.
Oktoba mwaka jana, Waziri Pinda alikwenda Kagera na katika kikao chake na viongozi wa mkoa aliwataka kutumia busara kumaliza mgogoro huo kwa kuwa unakwamisha shughuli nyingi za maendeleo, ukiwamo mradi wa maji ambao ulifadhiliwa Sh18 bilioni na Benki ya Dunia, lakini haujatekezwa kwa sababu ni lazima matumizi hayo yaidhinishwe na Baraza la Madiwani.
Katika kikao hicho, Pinda alisema ni viongozi wa mkoa wakubaliane kufuta kesi zilizopo mahakamani ili kazi za kusaidia wananchi zifanyike.
Alisema anaumizwa na hali ya viongozi wa mkoa kukosa uchungu kwa wakazi wa manispaa hiyo wa kukosa maendeleo kwa ajili ya mtu mmoja, ambaye amefungua kesi mahakamani kuzuia shughuli za manispaa.
Katika mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera wa wakati huo, Fabian Masawe alimweleza Pinda kuwa shughuli za kisiasa zinakwamisha maendeleo na kwamba hadi wakati huo kulikuwa na kesi tatu mahakamani, ambazo zina zuio.
Alizitaja kesi hizo kuwa ni Namba 02/2014 iliyofunguliwa na Amani ya kutaka Mkurugenzi wa manispaa amtambue kuwa ni meya iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Bukoba na ambayo hakimu ametoa zuio la shughuli za halmashauri lilitolewa. Amani pia alifungua kesi Mahakama dhidi ya CAG na Mwanasheria Mkuu akitaka mambo kadhaa yaliyomo kwenye taarifa ya ukaguzi, yaenguliwe.
Kesi nyingine imefunguliwa na Yusuf Ngaiza na wenzake watano dhidi ya Chifu Kalumuna na Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba wakipinga kuvuliwa udiwani.
Akizungumzia mgogoro huo ulivyoanza, Kagasheki alisema: “Ule mgogoro siyo wangu, wala siyo suala la mgogoro, ni suala la wizi. Sisi Watanzania ni mahodari wa kubadilisha maneno.”
Alisema anashangazwa na wanaomtaja kuwa ana mgogoro na meya huyo wa Bukoba na kukumbusha kuwa Meya Amani ni mtu ambaye Serikali ilishamwondolea uraia, hivyo hakuwa na nafasi yoyote ndani ya CCM wala Serikali.“Ni mfanyabiashara na kilichotokea ni kuwa sisi watu wa Bukoba tulisema tunahitaji maendeleo. Mimi ndiyo nilikuwa kinara wa kutaka Amani atusaidie, wenzangu wote walikataaa, wakasema huyu mtu ana rekodi mbaya na kwamba ndiyo maana alinyang’anywa uraia na hivyo hafai. Nikapambana akawa diwani, alipopata udiwani ikabaki kazi ya madiwani kumpitisha, nikawashawishi kuwa ‘jamani, huyu ni mfanyabiashara atatusaidia’, kweli akapita akawa Meya.
“Mimi ningekuwa na ubaya na Amani? Aliyemleta pale ni mimi, nitakuwa mtu wa ajabu sana au kichaa, nimlete mtu halafu baada ya miezi sita nimkatae. Lakini kutokana na agenda yake nyingine tofauti na ile tuliyomchagulia, alichofanya akaamua kuwanunua viongozi.”
Aliongeza kusema: “Akamtumia Mkuu wa Mkoa, katibu na mwenyekiti wa CCM mkoa wakati huo, wakakubaliana kujenga soko jipya, uamuzi ambao ulipingwa na baadhi ya madiwani. Mimi nikatengwa na nilipomuuliza Amani, ugomvi ukaanzia katika mambo ya miradi.
“Sasa walichofanya wakaamua kuwafukuza wale madiwani waliokuwa wanapinga na kutetea haki za matumizi ndani ya halmashauri kwa madai kuwa ni madiwani wa Kagasheki, uamuzi uliopingwa na chama (CCM) na kuamua kuwarejesha.”
Alisema kutokana na kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro huo, maendeleo hayawafikii wananchi wa Bukoba, hali aliyosema inawasababishia mateso makubwa.
Mgogoro ulivyoibuka
Fukuto la kuwapo kwa mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Bukoba lilianza November 24, 2012 kwenye Uwanja wa Mayunga baada ya Balozi Hamisi Kagasheki kumtuhumu Amani kuiingiza manispaa kwenye miradi ya ufisadi.
Huo ulikuwa mwanzo wa mgawanyiko ndani ya chama hata Serikali kwa kuwa miradi ya ubadhirifu iliyonyooshewa kidole kwa harufu ya ufisadi, utekelezaji wake ulikuwa mikononi mwa taasisi za Serikali ukiwamo mradi wa upimaji wa viwanja kupitia Mfuko wa Dhamana na Uwekezaji UTT.
Kilichofuata ni kampeni ya kumng’oa Amani kwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani, mchakato uliosimamiwa na viongozi wa CCM wa ngazi ya wilaya kwenye Ukumbi wa St Francis chini ya uenyekiti wa Yusuph Ngaiza.
Mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili umesababisha hata viongozi wa kitaifa kupata kigugumizi kufanya mikutano ya hadhara mjini Bukoba kwa kutokuwa na majibu ya kuridhisha makundi yenye uhasama.
Credit: Mwananchi
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment