Siku tano baada ya kuzuiwa kufanya mkutano wa hadhara kwa madai ya tishio la ugaidi, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba jana alihutubia wananchi eneo la Manzese jijini Dar es Salaam bila kuwapo kwa ulinzi wa Jeshi la Polisi.
Mkutano wa jana wa Profesa Lipumba, ambaye alijikuta kwenye matatizo na Jeshi la Polisi baada ya kupigwa, kutiwa mbaroni na baadaye kufunguliwa mashtaka Jumanne iliyopita, jana ulitawaliwa na amani na ulidumu kwa takriban saa mbili kwenye eneo hilo la Manzese ambalo kwa kawaida huwa na utitiri wa watu.
Profesa Lipumba alikutwa na kadhia hiyo wakati akielekea Zakhem, Mbagala ambako alidai kuwa alikuwa akienda kushawishi wananchi watawanyike kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara.
Katika tukio hilo, mwenyekiti huyo wa CUF alikamatwa pamoja na wafuasi 32 na baadaye kufunguliwa mashtaka ya kula njama, kufanya maandamano na kukusanyika bila ya kibali. Vitendo hivyo vya polisi vilisababisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kusitisha shughuli zake na kuamua kujadili tukio hilo, bila ya kujali kuwa lilikuwa likiingilia shughuli za mhimili mwingine wa nchi.
Katika mkutano wa jana, hakukuwa na polisi waliovalia sare kama ilivyo kawaida kwenye mikutano ya hadhara ya kisiasa, hasa ya vyama vikubwa vya upinzani, ambayo hulindwa na askari wenye silaha na jana jukumu hilo lilifanywa na kikosi cha ulinzi cha chama hicho cha Blue Guards.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema hafahamu kuhusu suala hilo kwa kuwa yuko nje ya eneo lake la kazi.
“Hilo silijui kwani nipo nje ya Dar es Salaam hivyo siwezi kulizungumzia,” alisema Kamanda Wambura, ambaye alieleza kuwa yuko Dodoma ambako kulikuwa na mkutano wa maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi uliomalizika jana.
Naibu Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Abdul Kambaya alilieleza gazeti hili baada ya mkutano huo kuwa barua ya kuitaarifu polisi kuhusu mkutano huo ilipelekwa Alhamisi na wakapata majibu ya jeshi hilo siku iliyofuata, tofauti na ilivyokuwa kwenye mkutano wa Jumanne ambao uliombewa kibali Januari 22, lakini inadaiwa majibu yalitoka Januari 27 asubuhi.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe alilieleza Bunge kuwa CUF iliomba kibali Januari 26 ikitaka kufanya maandamano na mkutano Januari 27 na kwamba walikutana na viongozi wa mkoa wa chama hicho na kukubaliana kuyasimamisha.
Akihutubia wananchi jana, Profesa Lipumba alisema: “Kuna tatizo kubwa, kuna ombwe la uongozi. Kama Serikali kupitia kwa Chikawe inadiriki kusema uongo bungeni, ni hatari na mimi ninawaambia kuwa kila mwaka, tutaadhimisha mauaji hayo yaliyotokea Zanzibar (Januari 26 na 27 mwaka 2001).”
“Chikawe kusema kwamba kama uamuzi wa polisi haukuwa sahihi tungekata rufaa kwake, ni makosa kwani sisi tunaongozwa na sheria ya vyama vya siasa hivyo hii ni ishara ya Serikali kuamua kuendesha nchi kibabe jambo ambalo hatuwezi kulikubali.”
Profesa Lipumba, ambaye leo atafanya mkutano wa hadhara Mtaa wa Kigogo-Mkwajuni jijini Dar es Salaam aliongeza kusema: “Haya wanayoyafanya mwisho wake ni Oktoba mwaka huu kwani Ukawa tukichukua nchi, tutahakikisha tunalifanyia marekebisho makubwa Jeshi la Polisi ili lilinde watu na siyo kuwaua na kuwajeruhi wananchi.”
Profesa Lipumba akisema katika mkutano huo uliokuwa na lengo la kuwahamasisha Watanzania kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa, alisema mchakato ni mbovu na wananchi wajiandae kuikataa.
“CCM na Serikali yake imeuhujumu mchakato huu hivyo kuwaonyesha kuwa yale maoni mliyoyatoa mbele ya tume mnayataka, itakapofika Kura ya Maoni pigeni hapana,” alisema Profesa Lipumba huku akishangiliwa.
Mwenyekiti wa Vijana wa CUF, Hamidu Bobali alisema: “Tulikuwa tunajua adui yetu ni CCM, sasa na Jeshi la Polisi limekuwa adui wetu wa pili. Natoa wito kwa vijana wenzetu kuwa wao wana bunduki, risasi sisi tunatakiwa kujitetea kwani bila hivyo tutaangamia.”
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya alisema uhuru huu tulionao ulitafutwa na wazee wetu si Chikawe. Machifu wetu walinyongwa, waliuwawa, Waarabu kipindi wanatafuta uhuru wao walipigwa, yanayotukuta leo ni kama yaliyotokea wapi.”
“Mimi nilipigwa baada ya kuamua kumtetea Profesa Lipumba, nchi hii mtu akiamua kutuchinja atafanya na aliyenipiga spana kichwani (alipigwa kichwani na kushona nyuzi nane) namfahamu na kwa kuwa alikusudia kuniua basi na akashindwa sasa namweleza tutakutana mtaani,” alisema Kambaya
Chanzo: Mwananchi
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment