Chadema Wamtaka Rais Kikwete Kumtimua DC Chato

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mkuu wa wilaya ya Chato, mkoani Geita, kwa madai ya kukiuka kwa makusudi Katiba ya nchi aliyoapa kuilinda.

Aidha, kimemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, kumtimua kazi Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Chato (OCD), Alex Mukama, kwa madai ya kujiingiza kwenye siasa za kukilinda chama tawala badala ya kulinda raia na mali zao.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Katibu wa Chadema Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, alisema Rais Kikwete anatakiwa kutengua uteuzi wa mkuu wa wilaya hiyo, Rodrick Mpogolo, kwa sababu amekuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi kutokana na kuamuru Jeshi la Polisi kuwapiga na kuwakamata viongozi wa chama hicho na kuwafungulia mashitaka.

Alisema hatua hizo zimekuwa zikichukuliwa kwa kivuli cha agizo la Rais Kikwete la ujenzi wa maabara na kudai viongozi wa Chadema 55 wakiwamo wenyeviti wa vijiji na vitongoji 26 wamekamatwa na polisi na kufunguliwa kesi za kuwazuia wananchi kuchangia ujenzi huo.

Ludomya alisema mkuu huyo wa wilaya amekiuka Katiba, Ibara ya 146 (1), inayoeleza madhumuni ya kuwapo kwa serikali za mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, alipotafutwa kuzungumzia malalamiko hayo, alisema anatekeleza agizo la Rais Kikwete la ujenzi wa maabara nchini na kwamba ameagiza kukamatwa viongozi hao kwa kuwa wanawazuia wananchi kuchangia kiwango kilichoamriwa na kamati za maendeleo ya kata (WDC).

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, alipotakiwa kuzungumzia malalamiko dhidi yake, alisema hizo ni changamoto katika utendaji wa kazi zake na kutaka malalamiko hayo yaelekezwe kwa jeshi la polisi siyo kwake.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment