Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe na Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, wameweka hadharani mali, maslahi na madeni, ambazo zitawekwa wazi kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na tovuti ya chama ili wananchi wasome.
Akihutubia mamia ya wananchi wakati wa uzinduzi wa chama hicho, Zitto alianza kwa kuweka hadharani mali zake mbele ya mwanasheria wa chama na kudai kwa undani zitawekwa kwenye mtandao ili kila mwananchi ajisomee.
Kabla ya kusaini fomu hiyo, Zitto alisema Watanzania wananyanyapaliwa na kupuuzwa huku uchumi kushikiliwa na wachache na kwamba kwa sasa ni muda wa uchumi shirikishi kwa wananchi kuwawajibisha viongozi wao.
Alisema wananchi waikatae Katiba inayopendekezwa kwa kuwa imeshindwa kuwa na mfumo wa kuwajibisha na uwajibikaji kwa viongozi wa umma.
Alisema Tanzania inapoteza kiasi cha Sh. bilioni 490 kutokana na ushuru wa forodha huku kiasi cha Sh. trilioni mbili kila mwaka kikipotea kutokana na misamaha ya kodi, fedha ambazo zingetatua matatizo ya watanzania.
Awali, Mwenyekiti wa chama hicho, Anastazia Mghwira, alisema nia ya chama hicho ni kuhakikisha Taifa kwanza, sasa, leo na kesho ili kurejesha heshima ya Mtanzania ya undugu na kujali.
Mghwira alisema ni mara ya kwanza kwa chama cha siasa kuongozwa na mwanamke na kwamba chini ya uongozi wake watahakikisha tafsiri za rasilimali za Taifa inaonekana katika maisha ya Mtanzania wa kawaida.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Samson Mwigamba, alisema kwa kipindi cha miezi saba chama hicho kimejiimarisha na kupata wenyeviti 13 wa mitaa, vijiji 13, vitongoji 67 na wajumbe wa serikali za mitaa na vijiji 250, hivyo kushika nafasi ya tano kati ya vyama 22 vya siasa.
Mhasisi wa chama hicho, Prof. Kitila Mkumbo, alisema moja ya matatizo ya vyama vingi vya siasa ni kuchanganya uongozi wa chama na dola, na kwamba vyama vyenye akili kama ACT kinakuwa na kiongozi wa chama na viongozi wengine.
Alisema ndani ya chama hicho cheo siyo jambo la msingi sana bali muhimu ni majukumu na kwamba moja ya kazi kubwa ya kiongozi mkuu ni kutangaza ilani ya chama na kuwasilisha taarifa kwa Mwenyekiti.
Alisema ndani ya chama hicho iwapo kiongozi atagombea nafasi ya uongozi na kushindwa atakuwa akijieleza ndani ya kamati kuu na akishindwa kutoa sababu za msingi atapigiwa kura ya kutokuwa na imani naye.
Chanzo: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment